1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fico na Putin wakutana Moscow kuijadili Ukraine

23 Desemba 2024

Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico alifika Urusi kwa mazungumzo na rais Vladimir Putin yaliyojikita juu ya masuala ya usambazaji wa gesi asilia ya Urusi na matumaini ya kumalizika kwa vita kati ya Urusi na Ukraine.

https://p.dw.com/p/4oVUk
Russland Moskau 2024 | Slowakischer Premier Fico trifft Präsident Putin im Kreml
Picha: Artyom Geodakyan/TASS/IMAGO

Robert Fico alifanya ziara ya kushtukiza mjini Moscow siku kadhaa baada ya kukosa kuafikiana na serikali ya Ukraine juu ya njia ya kupitisha gesi ya Urusi kupitia nchi hiyo kuelekea Slovakia, huku rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy  akisema hana nia ya kuongeza muda wa mkataba uliopo sasa unaomalizika mwishoni mwa mwaka huu.

Amesema Putin ameashiria nia ya kuendelea kuipa Slovakia na mataifa ya Magharibi nishati ya gesi, lakini hilo halitawezekana kufuatia msimamo huo wa Zelensky, huku akisema hilo pamoja na hatua ya rais wa Ukraine kuunga mkono vikwazo dhidi ya mpango wa nyuklia wa Urusi, linaendelea kuiathiri Slovakia kifedha na kuhatarisha uzalishaji wa umeme katika mitambo ya nyuklia nchini Slovakia, jambo ambalo halikubaliki.

Putin afanya mazungumzo ya nadra na Waziri Mkuu wa Slovakia

Mapema wiki hii katika mkutano wa viongozi wa Ulaya uliofanyika mjini Brussels ambako Zelensky pia alialikwa, Fico alijaribu kupata tamko tofauti juu ya msimamo huo wa Ukraine bila mafanikio. Waziri Mkuu huyo wa Slovakia ni kiongozi wa tatu katika Umoja wa Ulaya kuitembelea Moscow kwa mazungumzo na Putin tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka 2022. Kansela wa Austria Karl Nehammer alikuwa huko mwezi Aprili mwaka 2022 huku Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban akiitembelea Moscow mwezi Julai mwaka huu.

Jeshi la Ukraine ladungua droni 47 za Urusi

Ndege za kivita
Jeshi la anga la Ukraine limesema limedungua droni 47 kati ya 72 za Urusi zilizorushwa Ukraine.Picha: Teri Schultz/DW

Msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov alithibitisha kukamilika kwa mazungumzo hayo na kusema viongozi hao wawili hawatotoa tamko la pamoja, lakini walijadili pia hatua ya uwepo wa wanajeshi wa Urusi, Ukraine, matumaini ya kumalizika vita baina ya mataifa hayo na mahusiano ya Slovakia na Urusi ambayo Fico alisema anapanga kuyaimarisha zaidi. Gesi asilia ya Urusi bado inasafarishwa kuelekea baadhi ya nchi za Ulaya, ikiwemo Slovakia, kupitia Ukraine kwa mujibu wa makubaliano ya miaka mitano yaliyotiwa saini kabla ya vita.

Huku hayo yakiarifiwa jeshi la anga la Ukraine limesema limedungua droni 47 kati ya 72 za Urusi zilizorushwa Ukraine. Katika taarifa yake kupitia mtandao wa Telegram jeshi hilo limesema droni nyengine 25 hazikufika katika maemeo yalikolengwa.

Russia yaigusa pabaya Ukraine, Kyiv yajibu mapigo

Kwengineko Kamandi kuu ya jeshi la Korea Kusini imesema zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Korea Kaskazini wameuwawa au kujeruhiwa katika vita vya Urusi nchini Ukraine. Idadi hiyo mpya inafuatia ripoti iliyotolewa na taasisi ya kijasusi ya Seoul iliyosema wanajeshi 100 wa Korea Kaskazini wameuwawa tangu walipoingia kuisadia Urusi katika vita hivyo mwezi Desemba. Korea Kaskazini na Urusi ziliimarisha mahusiano yao ya kijeshi tangu Moscow ilipoivamia Ukraine. Makubaliano ya ulinzi wa pamoja yalisainiwa mwezi Juni na kuanza kufanya kazi mwezi huu.

Vyanzo: DW Page, reuters,afp