Hatimaye Ruto aahidi kukomesha utekaji raia
28 Desemba 2024Vyombo vya usalama kwenye taifa hilo la mashariki mwa Afrika vimekuwa vikituhumiwa kwa kuwashikilia makumi ya watu kinyume na sheria tangu yafanyike maandamano ya kuipinga serikali yaliyoandaliwa na vijana katika miezi ya Juni na Julai.
Matukio ya hivi karibuni kabisa ya watu kutoweshwa kwa nguvu yamekuwa yakiwahusu vijana wa kiume wanaomkosowa Rais Ruto mitandaoni, huku makundi ya haki za binaadamu yakitupilia mbali madai ya polisi inayokanusha kuhusika na yakitowa wito wa hatua kuchukuliwa kwa haraka.
Soma zaidi: Wajuwe watuhumiwa wanne wanaotakiwa na ICC kwa vurugu za Kenya
Akizungumza na umati wa watu katika mji wa Homa Bay ulio magharibi mwa Kenya siku ya Ijumaa (Disemba 27), Rais Ruto aliahidi kuchukuwa hatua za kukomesha utekaji nyara huo lakini pia akiwaambia wazazi "wabebe dhamana" ya kuwalea watoto wao.
"Tutakomesha utekaji nyara ili vijana wetu waishi kwa amani," alisema kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kenya.
Kwenye hotuba yake kwa taifa ya mwezi Novemba, Ruto aliwahi kulizungumzia suala hilo, akilaani matumizi ya nguvu yaliyochupa mipaka na hatua zozote zilizo nje ya sheria, lakini pia alisema kwamba watu wengi wanaoshikiliwa walikamatwa kihalali kutokana na kuhusika na uhalifu.
Polisi yashutumiwa
Ghadhabu imekuwa ikiongezeka nchini Kenya, na kumeshuhudiwa maandamano ya hapa na pale kupinga kutekwa kwa vijana.
Polisi imekanusha kuhusika na matukio hayo lakini wanaharakati wanahoji kukosekana kwa hatua za uchunguzi kwa visa vya watu wanaotoweka katika mazingira ya kutatanisha.
"Ikiwa kweli polisi hawahusiki, wanapaswa kuchunguza na kuwashitaki wale waliohusika haraka," kilisema Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK).
Soma zaidi: Hasira zaongezeka Kenya kuhusiana na utekaji wa wakosoaji
Mapema mwaka huu, shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) lilisema kwamba utafiti wake uligunduwa kuwepo kwa kikosi kimoja kilichoundwa na maafisa kutoka vyombo mbalimbali vya usalama.
Kauli ya Ruto ilitolewa baada ya kauli ya hivi karibuni aliyekuwa makamu wake wa rais, Rigathi Gachagua, aliyetuhumu kwamba kuna kikosi maalum cha siri kinachohusika na matukio ya watu kupotea.
"Kuwateka na kuwauwa hawa watoto sio suluhisho... Hii ni serikali ya kwanza kwenye historia ya nchi hii kuwaandama watoto kwa njia za ukatili," alidai Gachagua.
Maandamano ya kupinga utekaji
Siku ya Ijumaa, maandamano yalifanyika kwenye mji wa kaskazini mashariki, Embu, ambako kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 24 aitwaye Billy Mwangi alipotea mwishoni mwa wiki.
Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Kenya (KNCHR) ilisema siku ya Alkhamis (Disemba 26) kwamba watu 82 walichukuliwa katika mazingira ya kutatanisha na watu wasiojulikana na waliokuwa wamebeba silaha tangu mwezi Juni, ambapo 29 kati yao hawajaonekana hadi sasa.
Soma zaidi: Mamlaka Kenya zakanusha kuwateka wakosoaji wa serikali
Kamisheni hiyo iliwaorodhesha watu wengine saba waliotekwa tangu tarehe 17 Disemba. Wawili katika hao - Mwangi na Peter Muteti - walichukuliwa muda mfupi baada ya kutuma picha zilizobuniwa kwa teknolojia ya akili bandia zikimuonesha Ruto amekufa.
Idara ya Mahakama ya Kenya ilisema wiki hii kwamba "utekaji nyara hauna nafasi kwenye sheria na ni kitisho kwa haki za raia."
Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa X siku ya Alkhamis, idara hiyo ilivitaka "vyombo vya usalama na pande zote zinazohusika kufuata sheria ili kulinda haki na uhuru wa kimsingi wa raia."
Chanzo: AFP