1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hizbullah, Israel washambuliana vikali

20 Septemba 2024

Kundi la wanamgambo nchini Lebanon,la Hezbollah limesema limevurumisha makombora yapatayo 140 kuelekea kaskazini mwa Israel, na kuyalenga maeneo kadhaa ya kimkakati ikiwa ni pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga.

https://p.dw.com/p/4kud8
Kfar Kila | Israel Lebanon
Moshi ukifuka baada ya mashambulizi ya Israel kwenye kijiji cha Kfar Kila kusini mwa Lebanon.Picha: Karamallah Daher/REUTERS

Haya yanajiri siku moja baada ya kiongozi wa Hizbullah, Hassan Nasrallah, kuapa kulipiza kisasi kwa mashambulizi yaliyofanywa kupitia miripuko ya vifaa vya mawasiliano yaliyosababisha vifo vya watu 37.

Wakati huo huo, chanzo kilicho karibu na Hizbullah kimeeleza kuwa mashambulizi ya leo ya Israel mjini Beirut yamemuua kamanda mkuu wa kikosi maalum cha  operesheni za kundi hilo, Ibrahim Aqil, aliyekuwa amechukua nafasi ya Fuad Shukr aliyeuawa pia mwezi Julai.

Soma zaidi: Israel yauwa watu wawili kusini mwa Lebanon

Umoja wa Mataifa umezitaka nchi wanachama kuendeleza juhudi za kuzuia kutanuka kwa mzozo huo.

"Katibu Mkuu na maafisa waandamizi na hasa wawakilishi mashinani wamekuwa wakifuatilia kwa karibu hali ilivyo katika maeneo ya kusini mwa Lebanon na kaskazini mwa Israel. Mratibu Maalum wa Lebanon Jeanine Hennis-Plasschaert, amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na wahusika wote na kuwahimiza kujizuia na utulivu pamoja na kuunga mkono juhudi za kidiplomasia ili kukomesha ghasia hizi haraka sana. Ni muhimu kwa nchi wanachama kutumia ushawishi wao katika kuepusha kutanuka kwa mzozo." Alisema Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.