1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na Saudi Arabia zakubaliana kurejesha uhusiano

6 Aprili 2023

Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Saudi Arabia wamekutana mjini Beijing lesiku ya Alhamisi na kutangaza kwamba nchi zao zimerejesha uhusiano wa kidiplomasia.

https://p.dw.com/p/4PlcS
China Peking | Treffen der Außenminister von Iran und Saudi-Arabien | Hossein Amir-Abdollahian und Prinz Faisal bin Farhan Al Saud
Picha: Iran's Foreign Ministry/WANA/REUTERS

Mkutano kati ya mawaziri hao wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na mwenzake wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan ni wa kwanza kwa wajumbe wakuu wa nchi hizo mbili kufanyika katika kipindi cha zaidi ya miaka saba.

Mazungumzo hayo yaliyosimamiwa na China, Iran taifa la Kiislamu lenye kuegemea madhehebu ya Shia na Saudi Arabia inayoegemea madhehebu ya Sunni zilikubaliana mwezi uliopita kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia baada ya miaka mingi ya uadui kati yao. Nchi zote hizo mbili zinashindana kwa ushawishi wa kisiasa na kijeshi katika kanda ya Mashariki ya Kati.

Kushoto: Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia,Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud. Kulia: Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian.
Kushoto: Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia,Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud. Kulia: Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian.Picha: Iran's Foreign Ministry/WANA/REUTERS

China imepongeza tamko la mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia na Iran kuhusu kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning aliuambia mkutano wa waandishi wa Habari kwamba pande hizo mbili zimeonyesha nia ya kuboresha uhusiano kulingana na makubaliano yaliyofikiwa mjini Beijing mwezi uliopita.

Soma pia:Je, Mwanamfalme wa Saudia ananyoosha mkono wa amani?

Amesema China inapongeza na kuthamini uimarishaji unaoendelea wa uhusiano kati ya Saudi Arabia na Iran na kwamba China iko tayari kuendelea kutekeleza jukumu la upatanishi na kuziunga mkono pande hizo mbili ili ziendelee kuaminiana na kuendeleza ujirani mwema. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China ameongeza kuserma kwamba nchi yake itaendelea kuchangia hekima yake kwa ajili ya usalama, utulivu na maendeleo ya Mashariki ya Kati.

Soma pia:Rais wa Iran kumtembelea Mfalme wa Saudi Arabia katika jitihada za kuimarisha mahusiano

Katika kanda fupi iliyorushwa na kituo cha televisheni serikali ya China CCTV, viongozi hao wa Saudi Arabia na Iran walionekana wakisalimiana kwa bashasha na kubadilishana hati za maelewano zilizotiwa saini mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China Qin Gang.

Waziri wa mambo ya Nje wa China Qin Gang katikati ya mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudi Arabia.
Waziri wa mambo ya Nje wa China Qin Gang katikati ya mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudi Arabia.Picha: Iranian Foreign Ministry/AFP

Saudi Arabia na Iran zimesema katika taarifa ya pamoja kwamba zitazindua mipango ya kufungua tena balozi na balozi ndogo kwenye nchi zao ndani ya kipindi cha miezi miwili kilichoainishwa katika makubaliano ya mwezi uliopita. Nchi hizo mbili pia zitaendelea kuratibu na kutafuta njia za kupanua ushirikiano wao, ikiwa ni pamoja na kurejesha safari za ndege na kurahisisha visa kwa raia wao.

Vyanzo: DPA/RTRE