Iran yawataka wageni kuheshimu sheria
10 Oktoba 2022Kauli hiyo ya serikali inakuja wakati uongozi wa juu wa kisiasa nchini humo ukiitisha mkutano wa dharura, unaowajumuisha rais, spika wa bunge na mkuu wa muhimili wa mahakama.
Kikao hicho kilichozungumzia kwa kina juu ya maandamano yanayoingia wiki yake ya nne nchini humo, huku idadi ya waliokwishapoteza maisha ikipindukia 70, kwa mujibu wa mashirika ya haki za binaadamu.
Tamko la pamoja la viongozi hao watatu lililotolewa Jumapili (Septemba 9) baada ya mkutano wao liliwataka watu kulinda umoja wa kitaifa na kusimama pamoja dhidi ya kile walichosema ni 'hujuma za maadui' wa mfumo wa Kiislamu.
Iran imekumbwa na maandamano kwa wiki kadhaa sasa kufuatia kifo cha msichana wa miaka 22,Mahsa Amini, ambaye alikuwa anashikiliwa na polisi ya maadili mjini Tehran kwa kukiuka sheria za mavazi ya wanawake.
Televisheni za serikali zadukuliwa
Jioni ya Jumamosi (Septemba 8), maandamano yaliwafikia watazamaji wa televisheni baada ya chanelo mbili za serikali kudukuliwa, wakati wa taarifa za habari, na kurushwa picha za marehemu Mahsa na pia wanawake wengine waliokufa kwenye maandamano hayo.
Kundi la wanaharakati liitwalo Edaalate Ali lilidai kuhusika na udukuzi huo, ambao pia ulichapisha picha za watu walioziba sura zao.
Mamlaka nchini Iran zinadai kuwa Mahsa Amini alikufa kutokana na maradhi ya moyo na sio mateso ya polisi, kama wanavyodai waandamanaji. Lakini tangu kifo hicho, kumekuwa na maandamano makubwa ndani na nje ya Iran dhidi ya utawala wa Iran na hasa dhidi ya ulazima wa kuvaa hijabu.
Vyombo vya usalama vimejibu maandamano hayo kwa ukandamizaji mkubwa, ambapo Shirika la Haki za Binaadamu la Norway linasema zaidi ya watu 70 wameshauwa, wakiwemo watoto 19.
Tehran yaishutumu Magharibi
Hata hivyo, serikali ya Iran inayashutumu mataifa ya Magharibi kwa maandamano hayo, wakizitaja hasa Marekani na Israel na wale inaowaita kuwa ni wasaliti wa Iran walioko nje ya nchi.
Hapo jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Majid Mirahmadi, alitangaza kuwa maandamano yamemalizika, akisema kwamba amani na utulivu umerejea kwa sehemu kubwa kuliko maeneo machache tu.
Lakini picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha maandamano hayo yakiendelea kwenye maeneo kadhaa ya nchi.
Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba kila ishara inaonesha kuwa vyombo vya usalama nawaandamanaji wako tayari kutumia hata silaha kutimiza malengo yao.
Wengi wanahofia maandamano haya kugeuka kuwa uasi wa umma dhidi ya dola hiyo ya Kiislamu nchini Iran.