Zaidi ya 75 waandamanaji wauawa Iran
27 Septemba 2022Idadi hiyo ni kulingana na mashirika ya wanaharakati, lakini serikali ya Iran inasema waliokufa ni 41 tangu siku ya Jumamosi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanajeshi wa vikosi vya usalama, wakati taifa hilo likiwa limegubikwa na wimbi kubwa la maandamano ambayo hayajashuhudiwa katika kipindi cha karibu miaka mitatu.
Maandamano yaliendelea jana usiku na waandamanaji wakija na aina mpya ya kuandamana, wakijikusanya kwenye makundi madogo madogo ili polisi wasiweze kuwadhibiti.
Soma Zaidi:Kifo cha msichana Mahsa chazusha maandamano makubwa Iran
Katika mji mkuu wa jimbo la Kurdistan Sanandaj anakotokea Amini, wanawake waliparamia magari na kuchana hijabu mbele ya umati uliokuwa ukishangilia, hii ikiwa ni kulingana na picha zilizochapishwa na kundi la haki za binaadamu la IHR lenye makao yake Oslo.
Kulingana na shirika hilo, karibu watu 76 wameuawa kufuatia hatua kali. Mkurugenzi wa IHR Mahmood Amiry-Moghaddam ameiomba jumuiya ya kimataifa kwa pamoja kuchukua hatua madhubuti za kusimamisha mauaji na mateso dhidi ya waandamanaji.
Soma Zaidi: Watu 31 wauawa kwenye maandamano nchini Iran
Maafisa wamesema jana Jumatatu kwamba zaidi ya watu 1,200 wamekamatwa ambao ni pamoja na wanaharakati, mawakili na waandishi wa habari. Karibu waandishi wa habari 20 wamekamatwa, hii ikiwa ni kulingana na kamati ya kuwalinda waandishi wa habari.
Ofisi ya Umoja wa mataifa ya haki za binaadamu imesema ina wasiwasi mkubwa na muendelezo wa hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya waandamanaji nchini Iran na kushtushwa zaidi na baadhi ya viongozi wanaowatusi waandamanaji, amesema msemaji wa shirika hilo, Ravina Shamdasani mapema leo.
"Sisi kwenye ofisi ya haki za binaadamu, tuna wasiwasi mkubwa jinsi vikosi vya usalama vinavyoshughulikia maandamano nchini Iran pamoja na kuzuia mawasiliano ya simu za mezani, za mkono, intaneti na mitandao ya kijamii. Maelfu wanaandamana kote Iran wakiipinga serikali kwa takriban siku 11. Vikosi vya usalama vimejaribu kuyazima wakati mwingine kwa risasi za moto." Alisema Shamdasani.
Katika hatua nyingine, bunge la Iran limeonyesha mgawanyiko mkubwa juu ya hatua hizo dhidi ya waandamanaji. Kulingana na shirika la habari la serikali, IRNA mchana wa leo, mbunge Zohreh Sadat Lajevardi amesema maandamano haya ya sasa yameandalia na maadui wa Iran na kutoa mwito wa hatua kali zaidi kwa waandamanaji.
Soma Zaidi: Mhafidhina Ebrahim Raisi ashinda kura ya urais Iran
Tofauti na yeye, mbunge kutoka kamati ya mambo ya ndani Jalah Rashidi Kuchi amesema kwa kuwa serikali inashindwa kushughulikia mambo ukamilifu, ni dhahiri mambo yatasimama. Amesema hakua haja ya kulaumiana, machafuko na undumilakuwili wa kisiasa, kwa kuwa hayo hayawezi kuleta suluhu ama kulipeleka taifa hilo mbele.
Mbunge Mahmoud Nabavian, mwenye misimamo mikali amewatupia maneno makali wanawake waliovua hijabu akiwafanisha na makahaba. Matamshi makali ya mbunge huyo wa Tehran yalitofautiana na kiongozi wa juu wa kidini Ayatollah Hossein Nouri Hamadani, ambaye siku ya Jumapili aliiomba serikali kuwasikiliza watu.
Maandamano haya yalichochewa na kifo cha msichana wa miaka 22, Mahsa Amini baada ya kukamatwa na polisi wanaosimamia maadili kwa kosa la kukiuka kanuni za mavazi na kufariki Septemba 16 kutokana na sababu ambazo bado hazijulikani.
Minong'ono inazidi kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na maandamano zaidi.
Mashirika: AFPE/RTRE/DPAE