1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMalawi

WHO: Kipindupindu chaua zaidi ya watu 1,200 nchini Malawi

16 Februari 2023

Shirika la Afya Ulimwenguni limefahamisha Alhamisi (09.02.2023) kuwa mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu katika historia ya Malawi umesababisha vifo vya takriban watu 1,210 na kuonya kuwa nchi jirani ziko hatarini.

https://p.dw.com/p/4Nbo5
Malawi Cholera
Picha: DW

Taifa hilo la kusini mwa Afrika limekuwa likipambana na mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu kuwahi kushuhudiwa, huku takriban visa 37,000 vimeripotiwa tangu Machi 2022.

Maambukizi yaliyothibitishwa tayari yameripotiwa kuvuka mpaka hadi Msumbiji, wakati WHO ikisema kuwa kulingana na tathmini yake, kuna hatari zaidi ya kuenea kwa ugonjwa huo ndani ya Malawi na katika nchi nyingine jirani.

WHO imesema katika taarifa yake kwamba maambukizi ya kipindupindu sasa yanaendelea katika wilaya 27 kati ya 29 za Malawi, huku nchi hiyo ikishuhudia ongezeko la asilimia 143 la idadi ya wagonjwa mwezi uliopita ikilinganishwa na Desemba mwaka jana.

WHO ilionya katika taarifa kuwa kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi yaliyoshuhudiwa mwezi uliopita, hofu ni kwamba mlipuko huo utakithiri kusipokuwepo hatua madhubuti.       

Lakini shirika la afya la Umoja wa Mataifa lilisema kuwa mlipuko nchini Malawi unatokea wakati kukiwa na ongezeko la milipuko ya kipindupindu duniani kote, ambayo imesababisha uhaba wa chanjo, vipimo na matibabu.

Baadhi ya visa 80,000 vya kipindupindu viliripotiwa katika bara la Afrika katika kipindi chote cha mwaka 2022.    

Hali kuwa mbaya zaidi:

Malawi Cholera
Wanawake wakichota maji katika mto Lilongwe, MalawiPicha: DW

WHO imebaini kuwa ikiwa hali ya sasa inayokua kwa kasi itaendelea, inaweza kuzidi idadi ya maambukizi ya mwaka 2021, ambao ulikuwa mwaka mbaya zaidi wa kipindupindu barani Afrika kwa karibu muongo mmoja.

Tangu kuanza kwa mlipuko huo,  Malawi  imeendesha kampeni mbili kubwa za chanjo, lakini kutokana na uhaba wa vifaa, imetoa dozi moja tu kati ya dozi mbili zinazopendekezwa za chanjo kipindupindu.   

Mwezi Novemba, Malawi ilipokea awamu ya pili ya takriban dozi milioni tatu kutoka kwa Umoja wa Mataifa, na mwezi uliopita msemaji wa wizara ya afya aliliambia Shirika la habari la AFP kuwa dozi zote zimetumika.

Soma zaidi: WHO: Kipindupindu kimeuwa zaidi ya watu 1,200 Malawi

Aidha, WHO ilisema kwamba asilimia 96.8 ya watu wanaoishi katika jamii zilizo katika hatari kubwa ya kuambukizwa kipindupindu zilipewa chanjo hiyo.

Zaidi ya chanjo, WHO imebaini kuwa, miongoni mwa hatua zingine, juhudi zinaendelea ili kuboresha mazingira na upatikanaji wa maji safi, huku kampeni ya nyumba hadi nyumba ikiendelea katika jamii na wilaya zilizoathirika.    

Kipindupindu, ambacho husababisha kuharisha na kutapika, huambukizwa kutoka kwa bakteria ambao kwa ujumla hupitia kwenye chakula au maji yaliyochafuliwa.

WHO inasema kuna hatari ya kuendelea kuongezeka kwa idadi ya maambukizi katika mlipuko wa Malawi, na kwamba hali hii inaweza kuenea zaidi kimataifa. 

Mataifa mengine hatarini

Verleihung des Virchow-Preises für Globale Gesundheit - Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Carsten Koall/dpa/picture alliance

Kulingana na WHO, nchi ya Zambia ambayo ni jirani ya Malawi pia imeshuhudia idadi kadhaa ya maambukizi sambamba na mataifa kama Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Kenya, Nigeria na Somalia.

WHO imesema milipuko ya sasa ya kipindupindu barani Afrika inatokea wakati bara hilo likikabiliwa na hali mbaya ya hali ya hewa, migogoro, na pia huduma za afya zilizoelemewa.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, shirika la afya la Umoja wa Mataifa pia lilionya kwamba hatari ya mlipuko wa kipindupindu duniani ilikuwa "juu sana" kutokana na milipuko mingi inayoendelea katika maeneo mbalimbali.  

Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatano kwamba kwa sasa kuna nchi 23 duniani zinazokumbwa na milipuko ya kipindupindu, huku nchi nyingine 20 zilizo jirani zikiwa hatarini.

Tedros alionya kuwa kwa jumla, zaidi ya watu bilioni moja duniani kote wako katika hatari ya moja kwa moja ya kuambukiwa ugonjwa wa kipindupindu.