Tetemeko Uturuki: Majengo dhaifu yalivyochangia vifo vingi
9 Februari 2023Matetemeko mengine ya ukubwa sawa na huo yameshuhudia idadi ya chini zaidi ya vifo. Kwa mfano vifo vilivyosababishwa na matetemeko mtawalia ya mwaka 2014 na 2015 nchini Chile, yaliyokuwa na ukubwa wa 8.2 na 8.3, havikuzidi 15. Ni zipi sababu za uharibifu mkubwa kiasi hicho safari hii?
Majengo ya zamani hayajasanifiwa kuhimili tetemeko
Picha za vidio kutoka miji ya karibu na kitovu cha tetemeko hilo zimeonyesha aina ya uporomokaji wa majengo ambao baadhi wanauita gole - unaotokea wakati jengo zima linapoporomoka, kila ghorofa juu ya nyingine. Nafasi ya kunusurika kwa mtu katika jengo lililoporomoka namna hii ni ndogo sana.
Soma pia: Idadi ya vifo yapindukia 17,000 baada ya tetemeko la ardhi katika mpaka kati ya Uturuki na Syria
Majengo ya ghorofa yanayoshuhudia uharibifu wa namna hii mara nyingi yanakuwa ya zamani yenye viwango dhaifu, anasema Mehdi Kashani, Profesa mshiriki wa miundo na uhandisi wa matetemeko ya ardhi katika chuo kikuu cha Southampton, cha nchini Uingereza.
Jengo la ghorofa lina sakafu na madirisha, milango na matundu mengine mahali ambapo ukuta halisi ungekuwa imara ili kuweza kustahamili tetemeko la ardhi. Pale moja ya ghorofa hizi inapokuwa kwenye sakafu ya chini, jengo zima linaweza kuporomoka na ghorofa hiyo.
Ingawa baadhi ya majengo katika maeneo yanayokumbwa na tetemeko la ardhi kwenye mpaka wa Uturuki na Syria sasa yamejengwa ili kustahimili mitetemeko ya ardhi, mengi yalijengwa kabla ya ubunifu wa ujenzi unaohimili matetemeko kuanzishwa.
Kashani anasema kanuni za msingi zilianza kutengenezwa miaka ya 1960 na 70, hivyo si za zamani sana.
Anasema tetemeko la ardhi la Kobe nchini Japan mwaka 1995 lilitoa mchango mkubwa katika kubadilisha mambo mengi yaliyokwenda mrama na kupelekea utafiti zaidi.
Hivyo kimsingi, mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, ndipo zilipoanza kubadilika kanuni nyingi ujenzi kwenye maeneo ya matetemeko.
Kanuni za tetemeko ni miongozo ya namna ya kujenga katika maeneo yalio karibu na eneo la tetemeko. Majengo yanayojengwa bila kufuata miundo ya kuhimili tetemeko yalikuwa hasa hatarini wakati wa tetemeko la Jumatatu.
Soma pia: Erdogan akiri changamoto kwenye shughuli za uokozi
Kashani anasema majengo ya zamani zaidi yanaweza kukarabatiwa ili kuhimili matetemeko -- na hii imetokea Japan na Chile, ambako matetemeko hutokea mara kwa mara.
Hata hivyo, anasema hii inahitaji fedha nyingi na utashi wa kisiasa, na hivyo haitokei kila mahala inakopaswa kutokea.
Tetemeko lilikuwa la kina kifupi
Lakini uharibifu hautokani tu na muundo wa jengo. Nguvu za tetemeko la ardhi pia zilikuwa kubwa. Kulingana na Kashani, tetemeko hilo lilikuwa la kina kifupi.
Hii ina maana kwamba mshtuko wa kugongana kwa visahani vya tektoniki ulitokea karibu na tabaka la dunia, na kufanya athari kuwa na nguvu zaidi kuliko ikiwa mshtuko ungetokea ndani zaidi ardhini na kuchukua muda mrefu kufika kwenye tabaka la dunia.
"Ni kama wimbi katika bahari", Kashani anasema. Mawimbi makubwa sana yatamwangusha mara moja mtu aliye kwenye chombo lakini mawimbi hayo yakishapita baharini kwa umbali wa kutosha, yatakuwa na athari ndogo.
Iwe tetemeko ni la kina kifupi au kirefu, inasaidia kueleza kwa nini baadhi ya matetemeko yenye ukubwa mdogo ikilinganishwa na mengine yanasababisha uharibifu mkubwa zaidi.
Soma pia: Tetemeko la ardhi na mwelekeo wa uchaguzi nchini Uturuki
Kashani anataja tetemeko la Bam lililotokea nchini Iran mwaka 2003, ambalo licha ya kuwa na ukubwa wa 6.3, ambao katika mazingira mengine, limesababisha vifo vichache, tetemeko hilo la kina kifupi liliuwa zaidi ya watu 25,000.
Miundo in umuhimu zaidi kuliko vifaa
Kashani anasema vifaa siyo sehemu muhimu zaidi ya kuhakikisha uwezo wa jengo kustahimili tetemeko, lakini muundo ni muhimu zaidi.
Kwa mfano, anasema kwa mchoro sahihi, zege inaweza kutoa msingi mzuri wa kulilinda jengo la madhara ya tetemeko.
Lakini jengo lililosanifiwa vibaya linaweza kuporomoka kama yale yaliyochukuliwa kwenye vidio zinazotoka Uturuki na Syria.
Kwa sasa miundo ya tetemeko inaruhusu majengo kustahmili matetemeko makubwa zaidi bila kuporomoka au kuanguka, hali ambayo inawanusuru watu walio karibu.
Lakini bado yanapata uharibifu mdogo, hali ambayo Kashani anasema ina uwezekano wa kuboreka katika miaka ijayo.
Katika miezi inayofuata, watafiti watasafiri katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko nchini Uturuki na Syria kuchunguza majengo yake.
Watajaribu kupata ufahamu wa sababu gani ziliyawezesha yale ambayo hayakuporomoka kusalia wima.
Imeandikwa kwa lugha ya Kiingereza na Clare Roth.