Malkia Elizabeth aahidi kushughulia madai ya Harry na Meghan
10 Machi 2021Katika taarifa iliyotolewa na Kasri la Buckingham hapo jana, Malkia Elizabeth alisema familia nzima imehuzunishwa na ukubwa wa changamoto walizokumbana nazo Harry na Meghan katika miaka michache iliyopita, na kuongeza kuwa masuala yalioibuliwa, hasa kuhusu rangi, yanatia wasiwasi.
Taarifa hiyo ilisema wakati baadhi ya kumbukumbu zinaweza kutofautiana, bado zinachukuliwa kwa uzito na zitashughulikiwa na familia kwa faragha.
Soma pia: Meghan Markle aungwa mkono kuibuwa ubaguzi kwenye Ufalme wa Uingereza
Kasri ya Buckingham limekabiliwa na shinikizo kubwa kujibu madai yaliyotolewa na wanandoa hao katika mahojiano na mtangazaji maarufu wa Marekani Oprah Winfrey siku ya Jumapili, ambayo yaliibua mzozo ambao haujawahi kushuhudiwa tangu wakati wa marehemu mama yake Harry, Diana katika miaka ya 1990.
Meghan, ambaye mama yake ni mwenye asili ya Afrika na baba mzungu, pia alizungumzia namna alivyoingiwa na mawazo ya kujiua, lakini alikosa msaada wowote wakati akiwa ndani ya familia ya kifalme.
Tuhuma za Harry na Meghan zinatilia mkazo namna ambavyo imekuwa vigumu kwa taasisi hiyo ya ufalme inayohudumiwa kwa fedha za walipakodi, ambayo inafuatisha mizizi yake katika historia ya miaka 1,000 ya historia ya England na Uingereza, kujirekebisha na kwendana na ulimwengu wa sasa na uchunguzi wa vyombo vya habari.
Clinton alaani ukatili wa magazeti ya udaku
Mke wa rais wa zamani wa Marekani ambaye pia alikuwa waziri wa mambo ya nje na mgombea urais wa chama cha Democratic mwaka 2016, Hillary Clinton, alisema mahojiano ya Harry na Meghan yalikuwa yanasikitisha kutazama, na kwamba magazeti ya udaku ya Uingereza yalimtendea kwa unyama Meghan
Soma pia: Uamuzi wa Harry na mkewe Meghan waumiza familia ya kifalme
"Unyama wao katika kumuandama Meghan ulikuwa wa kuchukiza. Na ukweli kwamba hakupata msaada zaidi kutoka kwa Malkia, kwamba jibu lilikuwa, tuyaweke tu kwenye karatasi na kujifanya kama vile hayakutokea au yataisha, inamisha tu kichwa. Binti huyo hakuwa tayari kuinamisha kichwa chake. Unajua hii ni 2021 na alitaka kuishi maisha yake. Alitaka kushiriki kikamilifu na alikuwa na kila haki ya kutumainia hilo."
Uchunguzi ulioendeshwa na shirika la YouGov kwa watu 4,656 baada ya mahojiano hayo kurushwa kwenye televisheni nchini Uingereza siku ya Jumatatu, ulionesha kuwa karibu theluthi moja walihisi wanandoa hao walitendewa isivyo haki, kiwango sawa na wale wanaofikiria kinyume.
Madai ya Harry na Meghan yamefananishwa na bomu linalodondoshwa kwenye familia maarufu zaidi nchini Uingereza, na moja ya taasisi zinazoheshimika zaidi nchini humo.
Chanzo: Mashirika