Maoni: Miaka 75 ya uhuru India
15 Agosti 2022Siku zilizopita, mzee mmoja wa Kijerumani aliniuliza swali ambalo nimebaki nalo hadi leo. Mzee huyo aliyekuwa na umri wa miaka 70 alisema, ''Nakumbuka nilipokuwa shule, tuliambiwa kwamba India ilikuwa ni nchi ya dunia ya tatu, nchi masikini ambayo inahitaji msaada wetu. Hivyo, tulichanga pesa na kuzituma huko kama msaada.''
Akiwa na sura ya udadisi aliendelea kusema, ''leo ninasoma kwenye magezeti kwamba India ni kituo kikuu cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Je nyinyi Wahindi mlitumia pesa zetu zote za msaada kununua kompyuta?'' Swali hilo linaweza kuwa la kuchekesha, lakini ni kiashiria tosha kwamba sura ya India imebadilika katika kipindi cha miongo saba iliyopita.
Sio miaka mingi iliyopita ambapo India ilionekana na mataifa ya Magharibi na picha za watu wanaocheza na nyoka, ng'ombe wakitembea mitaani na watu wanaopanda kwenye migongo ya tembo. Hata hivyo, miaka 75 iliyopita India imeweka alama katika nyanja ya teknolojia, mawasiliano ya simu, kilimo nauzalishaji wa nishati kwa kuzitaja chache tu. India ina zaidi ya watumiaji milioni 750 wa mtandao wa intaneti, jambo ambalo linaonesha pia jinsi nchi ilivyoendelea haraka katika enzi ya kidijitali.
Ushawishi unaokuwa wa India
India leo inafanya kazi kubwa kuwa mzalishaji mkubwa wa nishati mbadala duniani. Katika lengo lake la kuwa nchi yenye nguvu kubwa ulimwenguni, India inakuza uhusiano wa kibiashara na mataifa ya Mashariki na Magharibi. Hakuna ubishi kuwa jumuia ya kimataifa inaitazama India kwa matarajio makubwa leo, kuliko ilivyowahi kuwa nayo.
Vita vya Urusi nchini Ukraine ni kichocheo kikuu cha matarajio hayo yanayokuwa. India inaibuka kama nchi inayozidi kuwa mchangiaji muhimu katika jukwaa la dunia. Kwa sasa India inashika nafasi ya tano kwa kuwa na uchumi mkubwa zaidi duniani kulingana na pato la taifa na ya tatu kwa ukubwa kwa kununua kiasi sawa cha bidhaa na huduma katika kila nchi.
Kwa msimamo wake wa kutofungamana na upande wowote, sera za kigeni za India zinaleta matokeo mazuri, lakini ndani kwenyewe India ina kazi kubwa ya kufanya. Serikali ya India inadai itakuwa na uchumi wa dola bilioni 5 ifikapo mwaka 2025. Lakini bila ya kuwa na mageuzi makubwa kiuchumi, inaweza kubaki ndoto ya mbali kwa demokrasia kubwa zaidi duniani.
Mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira, mgawanyiko wa kijamii na kiuchumi, masuala ya lugha na dini ni changamoto kubwa ambazo nchi hiyo inakabiliana nazo miaka 75 baada ya kupata uhuru wake. Mvutano kati ya Wahindu na Waislamu umezidi kuongezeka katika miaka minane iliyopita.
Kufanya chaguo sahihi
Inaleta wasiwasi kwamba India ilishika nafasi ya 150 kati ya nchi 180 kwenye Faharasa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ya mwaka 2022, iliyochapishwa na Waandishi Habari Wasio na Mipaka. Zaidi ya hayo, India ilishika nafasi ya 101 kati ya nchi 116 katika Faharasa ya Njaa Duniani ya mwaka 2021. Takribani asilimia 25 ya watoto nchini India wanakabiliwa na utapiamlo na zaidi ya milioni 190 wanalala kila siku bila kula.
Katika miongo saba iliyopita India imetumia nguvu na rasilimali nyingi kushughulikia masuala ya usalama na nchi jirani kama vile Pakistan kwa upande mmoja na China upande mwingine. Hakuna shaka kwamba hili haliwezi kupuuzwa. Zaidi ya nusu ya wakaazi wa India wana chini ya umri wa miaka 25. Nchi italazimika kuhakikisha elimu, ajira na furaha inapatikana kwa vijana wake. Bila mabadiliko hayo, inaweza kuchukua miaka 75 mingine kabla ya India haijafikia lengo lake la kuwa nchi yenye nguvu kubwa duniani.
(DW)