Marekani na Ujerumani zafikia muafaka wa mradi wa gesi
22 Julai 2021Mataifa hayo mawili yamekubaliana kuisadia Ukraine na kuiwekea vikwazo Urusi ikiwa itatumia ugavi wa nishati kupata ushawishi wa kisiasa wa kijiografia. Taarifa ya mataifa hayo imesema Marekani na Ujerumani zimeungana katika dhamira yao ya kuiwajibisha Urusi kwa ushari wake na shughuli za uovu, kwa kuiwekea vikwazo na kutumia nyenzo nyingine. soma Marekani yaendelea kuiandama Ujerumani juu ya Nord Stream 2
Wamesema iwapo Urusi itajaribu kutumia nishati kama silaha au kufanya vitendo vya uvamizi dhidi ya Ukraine, Ujerumani itachukuwa hatua kwa ngazi ya kitaifa na kushinikiza hatua thabiti kwa ngazi ya Ulaya, ikiwemo vikwazo, kupunguza uwezo wa Urusi kuuza barani Ulaya katika sekta ya nishati, ikiwemo gesi na sekta nyingine muhimu kiuchumi.
Sehemu ya makubaliano
Kama sehemu ya makubaliano hayo, Ujerumani imekubali kuwekeza nchini Ukraine na kuhakikisha Moscow na Kyiv zinarefusha makubaliano ya upitishaji wa gesi. Zaidi ya hayo, Ujerumani na Marekani zitawekeza kiasi cha dola bilioni moja katika Mfuko wa Kijani ili kukuza miundomibu ya kimazingira ya Ukraine, inayojumlisha nishati jadidifu na viwanda vinavyohusika, kwa lengo la kuboresha uhuru wa nishati wa Ukraine. soma Ujerumani yaishutumu Marekani kwa vikwazo vya mradi wa gesi
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesifu makubaliano hayo akiyataja kuwa yenye manufaa. Amesema Ujerumani imerejea kusimamia malengo ya pamoja na ushawishi pamoja na Marekani kuhusu sera ya Urusi na sera ya nishati.
Makubaliano hayo yanawakilisha mabadiliko katika msimamo wa Marekani, ambayo kwa muda mrefu imepinga bomba hilo litakalosafirisha gesi kutoka mkoa wa Arctic nchini Urusi hadi Ujerumani kupitia Bahari ya Baltic.
Urusi inaweza kuikatia Ukraine ugavi wa nishati
Marekani ina wasiwasi kwamba Urusi inaweza kuikatia Ukraine ugavi wa nishati au mataifa mengine kama njia ya chokochoko kwa urahisi zaidi kwa kutumia bomba hilo, kwa sababu litaongeza uwezo wake wa kuuza nje kwa mataifa mengine ya Ulaya huku ikiyakwepa mataifa ya upitishaji yalio karibu na mipaka yake.
Ukraine na Poland zote zinapinga ujenzi wa bomba la Nord Stream 2, ambalo zinahofia litadhoofisha usalama wa nishati wa Ulaya na kupelekea kupotea kwa mapato kama mataifa ya kupitisha gesi ya Urusi. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilikanusha ripoti kwamba Ukraine ilionywa dhidi ya kukosoa makubaliano hayo, ikisema mmoja ya makansela wake alikuwa anazitembelea Kyiv na Warsaw wiki hii kuziarifu kuhusu makubaliano hayo.
Ikulu ya Marekani, White House pia ilitangaza jana Jumatano kwamba Rais Joe Biden atamkaribisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika ikulu hiyo Agosti 31.