Marekani yasema kuna mafanikio mazungumzo ya nyuklia na Iran
29 Desemba 2021Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Ned Price amewaambia waandishi habari mjini Washington kwamba kuna ishara ya kusonga mbele kwa mazungumzo ya mjini Vienna lakini akasita kusema ni kwa umbali gani ushara za mafanikio zinaonekana.
Price amefafanua kwamba kwa Washington mafanikio kwenye mazungumzo ya mjini Vienna ni kuona Iran inatimiza kwa vitendo sharti la kutotanua shughuli zake za nyuklia lakini kwa bahati mbaya hilo bado halijafikiwa. Kadhalika ameongeza kwamba kwa thathmini ya Marekani mazungumzo hayo yangali yanakwenda kwa mwendo wa kobe.
Duru ya nane ya mazungumzo juu ya mpango tata wa nyuklia wa Iran ilianza jana mjini Vienna katika juhudi za karibuni kabisa za kuunusuru mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 kati ya dola hiyo ya uajemi na mataifa yenye nguvu duniani.
Shaka shaka za mataifa ya Ulaya kwenye mazungumzo ya Vienna Iran yasema ina matumaini makubwa
Wajumbe wa mataifa ya Ulaya wanaoshiriki mazungumzo hayo wamesema licha ya mafanikio kadhaa yanayojitokeza, suala la Iran kupunguza shughuli zake za nyuklia ni muhimu sana iwapo Tehran ina nia ya dhati ya kuunusuru mkataba huo wa nyuklia.
Wanadiplomasia hao wanazungumzia jinsi mradi wa nyuklia wa Iran unavyokaribia kupindukia viwango vinavyokubaliaka chini ya masharti ya mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.
Wametahadharisha zimesalia wiki chache pekee za kufikia makubaliano ya maana mjini Vienna kabla mkataba huo haujapoteza umuhimu wake.
Wanadiplomasia waokutana wanajaribu kuishawishi Marekani kurejea kwenye mkataba huo baada ya kujitoa mwaka 2018 huku wakiitaka Iran kuheshimu masharti ya makubaliano hayo ili kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.
Iran yasema ina matumaini makubwa ya kupatikana makubaliano
Hata hivyo Iran yenyewe imezungumzia matumaini makubwa ya kupatikana makubaliano katika duru ya mazungumzo inayoendelea.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Hossein Amirabdollahian amesema "Tunaamini kwamba ikiwa kila upande utaendelea na duru hii ya mazungumzo kwa nia njema, kufikia mkataba mzuri kwa pande zote inawezekana na tunaweza kutimiza lengo hilo. Na iwapo tutaona utayari na nia njema ya upande wa pili katika duru zinazofuata, mkataba thabiti unawezaka kupatikana haraka"
Kiwingu kikubwa kinachozingira mazungumzo ya mjini Vienna ni wasiwasi wa nchi za magharibi kuwa Iran inayacheza shere kwa kupoteza muda huku ikiendelea na mradi wake wa nyuklia kwa kuongeza akiba kubwa ya madini ya urani iliyorutubishwa.
Mashaka kama hayo yanaelezwa pia na Israel iliyo hasimu mkubwa wa Iran ambapo waziri mkuu wake Naftali Bennett amewarai wanadiplomasia wa magharibi kuwa macho na kile anachokitaja kuwa hila za Jamhuri hiyo ya Kiislamu.