1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel yalaaniwa kimataifa

14 Aprili 2024

Nchi mbalimbali duniani zimelaani mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel usiku wa jumamosi, zikionya kwamba mashambulizi hayo yanatishia kuyumbisha zaidi hali ya usalama katika kanda ya Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4ejsg
Mzozo kati ya Israel na Iran
Makombora yakionekana mjini Amman Jordan baada ya Iran kuanzisha mashambulizi makubwa ya droni na makombora dhidi ya Israel:14.04.2024Picha: Video Obtained by REUTERS

Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi kuipatia Israel msaada wowote unaohitajika baada ya kufanya mkutano wa dharura na maafisa wake wakuu wa usalama.   

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amelaani mashambulizi hayo aliyoyaita ya "yasiyo na umakini", ambayo amesema yanahatarisha kuzusha mivutano na kuyumbisha usalama katika eneo hilo. Sunak amesisitiza kuwa kwa mara nyingine Iran imedhihirisha kuwa na nia ya kuanzisha  machafuko katika ardhi yake.

Mkuu wa maswala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema mgomo huo ni "ongezeko lisilo na kifani na tishio kubwa kwa usalama wa kikanda" katika ujumbe kwenye X.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Robertson S. Henry/REUTERS

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani mashambulizi hayo makubwa yaliyoanzishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya Israel. Guterres amesikitishwa na hatari ya mzozo kutanuka katika eneo zima, huku akitoa wito kwa pande zote kuepuka hatua yoyote ambayo inaweza kusababisha makabiliano makubwa ya kijeshi huko Mashariki ya Kati.

Soma pia: Iran yarusha mamia ya droni, makombora kuelekea Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameonya kwamba shambulio hilo litakuwa na athari kubwa na kuitaka Tehran kusitisha mara moja hatua hiyo. Baerbock amesema wanalaani shambulio linaloendelea na ambalo linaweza kulitumbukiza eneo zima katika machafuko, huku akiongeza kuwa Berlin itasimama imara na Israel.

Miito ya kutoka kila pembe ya dunia

Wizara ya mambo ya nje ya Cairo imeelezea wasiwasi wake mkubwa kutokana na kuongezeka kwa uhasama na kutoa wito kwa pande zote kujizuia. Taarifa ya wizara hiyo pia imeonya juu ya hatari ya  kutanuka kwa mzozo wa kikanda , na kwamba Misri itawasiliana moja kwa moja na pande zote kwenye mzozo huu ili kujaribu kudhibiti hali hiyo.

Kwa upande wake wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia imetoa taarifa ikielezea pia wasiwasi wake kufuatia kuongezeka kwa makabiliano ya kijeshi na kutoa wito kwa pande zote kujizuia kwa kiwango cha juu na kuliepusha eneo hilo na watu wake kutokana na hatari ya vita. Saudia imeendelea kwa kulihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua jukumu lake la kudumisha amani na usalama kote duniani.

Ndege ya kivita ya Israel F-15
Ndege ya kivita chapa F-15 ya Israel ikijiandaa kuruka ili kuharibu droni zilizorushwa na IranPicha: Israel Defense Forces/Handout via REUTERS

Wizara ya mambo ya nje ya China imezitaka pia pande zote kujizuia, ikiyataja mashambulizi hayo kama "matokeo ya hivi punde ya mzozo wa Gaza" na kuhimiza kutekelezwa kwa azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka usitishwaji mapigano na kusisitiza kuwa "mzozo huo lazima ukomeshwe sasa". China imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, hasa nchi zenye ushawishi, kuchukua jukumu lenye tija kwa ajili ya amani na utulivu wa ukanda huo. 

Soma pia:  Iran yaikamata meli ya Israel licha ya onyo la Biden

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Stephane Sejourné amesema: "Iran kuamua kuchukua hatua hiyo ambayo haijawahi kushuhudiwa, inadhihirisha kuwa taifa hilo limefikia kiwango kipya katika vitendo vyake vya uvunjifu wa amani na sasa inakabiliwa na hatari ya kuongezeka kwa makabiliano ya kijeshi".

Miito kama hiyo imetolewa pia na viongozi kutoka Uhispania, Canada, Urusi, Argentina na hata Ukraine. Jumuiya ya kujihami NATO imelaani pia mashambulizi hayo ya Iran dhidi ya Israel.

Israel yasifu mafanikio yake ya kiulinzi 

Israel | Daniel Hagari- Msemaji wa Jeshi la Israel IDF
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel Daniel HagariPicha: dts Nachrichtenagentur/IMAGO

Israel imesifu mafanikio yake ya kiulinzi baada ya kudungua asilimia 99 ya mamia ya makombora na droni zilizorushwa na Iran, katika shambulizi ambalo halijawahi kushuhudiwa la Iran dhidi ya taifa hilo.

Msemaji wa jeshi la Israel IDF, Daniel Hagari amesema hii leo kwamba Iran ilirusha makombora na droni zaidi ya 300, lakini imefanikiwa kuyaharibu kwa zaidi ya asilimia 99. Amesema makombora kadhaa ya masafa marefu yalifika Israel na kusababisha uharibifu kwenye kambi ya jeshi la anga.

Iran imefanya shambulizi hili jana Jumamosi, chini ya wiki mbili baada ya shambulizi lililodhaniwa kufanywa na Israel nchini Syria na kuwaua majenerali wawili wa Iran katika jengo la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus.

Soma pia: Biden aitahadharisha Iran kutoishambulia Israel

Ni shambulizi la kwanza la moja kwa moja la kijeshi kufanywa na Iran dhidi ya Israel licha ya mvutano wa miongo kadhaa tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.

Israel imesema inapima kikamilifu kuhusu jibu lake baada ya mashambulizi hayo huku Rais wa Iran Ebrahim Raisi akionya siku ya Jumapili kwamba watalipiza kisasi kwa hatua kubwa ikiwa Israel itajibu mashambulizi hayo.

Viongozi wa G7 kujadili shambulio la Iran 

Uingereza | Mawaziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo wa G7 mjini  Liverpool
Mawaziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo wa G7 walipokutana mjini Liverpool, Uingereza: 12.12.2021Picha: Olivier Douliery/AP Photo/picture alliance

Italia ambayo kwa sasa inashikilia urais wa kupokezana wa kundi la mataifa saba yaliyostawi zaidi kiviwanda (G7), imeitisha mkutano kwa njia ya video alasiri ya siku ya Jumapili ili kujadili mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel.

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni ameelezea wasiwasi wake mkubwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, na kusema kwamba mashambulizi hayo yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa katika kanda hiyo na kwamba wanaendelea kuwajibika ili kuepuka hali hiyo.

Soma pia: Israel katika hali ya tahadhari kufuatia kitisho cha Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani amesema anatumai kuwa serikali ya Israel itajizuia katika majibu yake na kwamba Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi kuwa kundi la G7 litatoa majibu yaliyoratibiwa ya kidiplomasia kufuatia mashambulizi hayo ya droni na makombora.

Kundi la G7 linazijumuisha Marekani, Canada, Italia, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Japan. Mawaziri wa mambo ya nje wa G7 wanatarajiwa kukutana Aprili 17 hadi 19 kwenye kisiwa cha Capri nchini Italia.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanatazamiwa pia kukutana baadaye Jumapili baada ya Israel kulitaka Baraza hilo kulaani shambulizi la Iran  na kushinikiza kuwa Walinzi wa Mapinduzi wa Iran watambuliwe kama kundi la kigaidi.

(Vyanzo: APE/DPAE / RTRE/AFP)