Mkutano wa COP27 kufungua pazia nchini Misri
6 Novemba 2022Zaidi ya wawakilishi wa nchi 200 duniani wanakusanyika kwenye mji huo kujaribu kwa mara nyingine kutafuta majibu ya jinsi ya kushughulikia taathira za Mabadiliko ya Tabianchi katika wakati ulimwengu unakabiliwa na vita na mzozo mkubwa wa kiuchumi.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo shirika la Hali ya Hewa la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kutoa ripoti yake ya kila mwaka itakayoangazia viwango vya hali ya hewa na matukio makubwa yaliyotokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani katika kipindi cha mwaka 2022.
Kuelekea mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametahadharisha kuwa sayari ya dunia inaelekea katika hali isiyorekebishika ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amewahimiza viongozi watakaohudhuria mkutano huo kuuweka ulimwengu katika njia sahihi ya kupunguza gesi zinazochafua mazingira na kutimiza ahadi zao za ufadhili kusaidia nchi maskini kuelekea matumizi ya nishati safi.
Guterres amesema mkutano huo utakaohudhuriwa na mashirika pamoja na nchi 198, sharti uwe mahali pa kujenga upya azma inayohitajika kuzuia sayari kutumbukia kwenye hatari ya tabia nchi.
Tarajio kubwa la mkutano huo ni kuwa na nia ya wazi ya kisiasa kupunguza kwa haraka gesi chafu zinazosababisha ongezeko la joto angani.
Guterres amesema katika wiki chache zilizopita, ripoti zimeonesha taswira ya kusikitisha kwamba gesi chafu zinazidi kuongezeka katika viwango vya juu badala ya kupungua angalau kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030.
Kiwango ambacho wanasayansi wamesema sharti kitimizwe ndipo angalau athari za tabia nchi zipunguzwe.
Uingereza kutoa ahadi ya kuachana na nishati chafuzi
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ambaye ni miongoni mwa viongozi wa ulimwengu watakaohudhuria mkutano wa COP27 humo Sharm el-Sheikh anatarajiwa kutoa ahadi ya nchi yake kuongeza kasi ya kuhamia kwenye nishati jadidifu. Ahadi hizo atazitangaza atakapolihutubia jukwaa la COP27 mnamo siku ya Jumatatu.
Sunak alifikia uamuzi wa dakika za mwisho wa kuhudhuria mazungumzo hayo ya masuala ya mazingira baada ya hapo kabla kutangaza kwamba angeyapa kisogo. Hilo lizusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanaharakati wa mazingira na wanasiasa wa upinzani nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa ofisi yake, Sunak atawatanabahisha wanasiasa na wafanyabiashara vigogo kwamba Uingereza itafanya kazi na washirika wake wa kimataifa kuharakisha mchakato wa kuhamia kikamilifu kwenye matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira. Ataeleza kwamba uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umefanya hitaji hilo kuwa muhimu zaidi na la haraka kwa Uingereza.
Uingereza ilikuwa mwenyeji wa mkutano uliotangulia wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP26 huko mjini Glasgow na waziri mkuu Sunak atalitumia jukwaa la COP27 kuyarai mataifa kutimiza ahadi walizotoa wakati wa mkutano uliopita.
Steinmeier aelezea mashaka yake kuelekea COP27
Katika hatua nyingine rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameonyesha mashaka yake juu ya kiwango gani cha hatua kinachoweza kuafikiwa katika mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabia nchi-COP27 .
Wasiwasi huo unatokana na hali ya mivutano ya kisiasa duniani. Akizungumza siku ya Jumamosi katika mjadala kuhusu sera za mazingira kwenye mji wa Korea Kusini wa Busan amesema ulimwengu unaingia katika kipindi cha migogoro.
Hata hivyo, Steinmeier ameongeza kusema kuwa kupigwa hatua katika mazungumzo hayo ni jambo muhimu kabisa, hata kama mazingira yake sio ya kutia moyo sana.