Mvutano kati ya Congo na Rwanda wapamba moto
14 Juni 2022Shutuma hizo kutoka kwa msemaji wa jeshi la serikali katika mkoa wa Kivu Kaskazini jenerali Syl-vain Ekenge, zimekuja saa kadhaa baada ya mji wa Bunagana kuangukia mikononi mwa waasi wa M23. Jenerali Ekenge amesema Wanajeshi wa Rwanda wameamua safari hii kukiuka mamlaka ya mipaka ya Congo kwa kuukalia mji wa mpakani wa Bunagana akisema hatua hiyo ni sawa na uvamizi.
Hadi sasa hapajakuwa na majibu yoyote kutoka Rwanda kuhusiana na taarifa hiyo, lakini serikali hiyo imekuwa ikikanusha vikali shutuma kwamba inawaunga mkono waasi wa M23. Wapiganaji wengi wa kundi hilo ni wacongo walio na asili ya kabila la Tutsi, na rais wa Rwanda Paul Kagame anatokea kabila lilo hilo.
DRC yadai askrai 500 wa Rwanda wameingia nchini mwake
Mji wa Bunagana uliodhibitiwa na kundi hilo upo umbali wa kilomita 60 kutoka Kaskazini Mashariki mwa Goma ambao ni muhimu kwa mashirika ya kimataifa ya msaada pamoja na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani MONUSCO.
Mji huo wa Bunagana pia upo karibu na mpaka na Uganda na ni eneo muhimu la kupitishia misaada inayoingia Congo kutoka China. Kwa upande wake msemaji wa polisi nchini Uganda Fred Enanga alisema jana Jumatatu kwamba zaidi ya wanajeshi 100 wa congo wanaokimbia mapigano ya waasi walivuka mpakani na kujisalimisha kwa maafisa wa Uganda.
Amesema wanajeshi hao wa Congo sasa watapelekwa mjini Rutshuru mji mwengine wa Congo uliopo upande wa Mashariki na ulio karibu na mpaka wa Uganda.
M23 watoa wito wa mazungumzo ya ana kwa ana na serikali ya DRC
Hapo jana Jumatatu msemaji wa kundi la M23 Willy Ngoma alitoa wito kwa rais wa DRC Felix Tshisekedi kuanzisha mara moja mazungumzo ya moja kwa moja na kundi hilo akisema wameukamata mji wa Bunagana ili kutoa njia salama kwa raia kurejea nyumbani baada ya kutoroka ghasia zilizokuwepo hivi karibuni.
Mahusiano kati ya Rwanda na Congo yameingia doa kwa miongo kadhaa sasa. Rwanda inadai Congo illiwapa hifadhi watu wa kabila la Hutu wanaodaiwa kutekeleza mauaji ya kimbari yaliotokea nchini humo mwaka 1994 yna kusababisha mauaji ya watutsi 800,000 pamoja na wahutu waliojaribu kuwasaidia watutsi.
DRC yaishutumu Rwanda kwa shambulio la mizinga
Mataifa hayo jirani yamekuwa pia yakishutumiana kwa kuunga mkono makundi tofauti ya waasi. Mwishoni mwa mwezi uliopita, Jeshi la Rwanda liliwashutumu wanajeshi wa Congo kwa kuwajeruhi raia wake kadhaa katika mashambulizi ya mpakani.
Kundi hilo la M23 lilipata tena umaarufu zaidi ya muongo mmoja uliopita baada ya wapiganaji wake kuuteka mji wa Goma mji mkubwa uliopo Mashariki mwa DRC unaopakana na Rwanda. Baada ya makubaliano ya amani wengi wa wapiganaji wa kundi hilo walijumuishwa katika jeshi la kitaifa.
Baadae mwaka huu kundi hilo likaibuka tena upya na kuanza mashambulizi dhidi ya jeshi la Congo likisema serikali hiyo imeshindwa kuweka ahadi zake.
Chanzo: afp, Reuters