Mwanamke wa Kichina akamatwa Ujerumani kwa ujasusi
1 Oktoba 2024Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkuu wa Ujerumani, mshukiwa huyo kwa jina la Yaqi X anatuhumiwa kutowa taarifa alizozipata wakati akiifanyia kazi kampuni moja ya usafirishaji katika uwanja wa ndege wa Halle mjini Leipzig, kwa mtu anayefanya kazi idara ya ujasusi ya China.
Mtu huyo ambaye pia ni raia wa China kwa jina Jian G naye pia amefunguliwa mashtaka.
Soma zaidi: Hali ya usalama nchini Ujerumani bado ni tete, majasusi
Wakati wa kukamatwa kwake, Jian G alikuwa akifanya kazi kama msaidizi wa mbunge wa Bunge la Ulaya, Maximilian Krah, ambaye ni mwanachama wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD.
Wasiwasi umekuwa ukiongezeka katika mataifa ya Ulaya Magharibi katika kipindi cha hivi karibuni kuhusiana na madai kwamba China inaendesha zoezi la udukuzi katika kanda hiyo.