1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Mzozo wa DR Kongo wavutia idadi inayoongezeka ya washiriki

22 Februari 2024

Majeshi ya kikanda, mamluki wa Ulaya na wanamgambo wa ndani wote wanapambana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda nchini DR Congo. DW inachambua makundi yanayoshirki katika mzozo huo unaozidi kuwa mkali kila uchao.

https://p.dw.com/p/4ckt0
Waasi wa M23 nchini DR Kongo
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema waasi wa Kongo wa M23 wanafanya kazi kama jeshi la kawaida.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/File/picture alliance

Eneo lenye milima na msitu la Mashariki mwa Kongo linalopakana na nchi kadhaa, kwa miaka mingi limekuwa likitumiwa kama ngome na makundi kadhaa yenye silaha. Katika wakati vita vimechachamaa kwenye eneo hilo, mikoa yenye utajiri wa madini ya eneo hilo la Mashariki nayo pia imegeuka kuwa uwanja wa vita wa nchi kadhaa zikiwemo Rwanda, Burundi na Uganda, pamoja na  vikosi vya kikanda kutoka mataifa matatu ya jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika.

Wakati huo huo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda zimo katika mzozo mkali. Kila mmoja anamlaumu mwenzake kwa kuunga mkono makundi mbalimbali yenye silaha katika majimbo ya mashariki mwa Kongo ya Kivu Kaskazini na Kusini, Ituri, na Tanganyika.

Vurugu zinazopamba moto, pamoja na mchanganyiko wake tete wa waasi, wanamgambo, vikosi vya serikali na kikanda, wakandarasi binafsi wa kijeshi na walinzi wa ndani, kila mmoja akiongozwa na maslahi na manung'uniko tofauti, inazidisha hofu kwamba mapigano yanaweza kusambaa katika mpaka wa Kongo. Haya ndiyo baadhi ya makundi yanayoshiriki mzozo huo:

M23 na makundi mengine ya silaha

Zaidi ya makundi 250 ya wapiganaji wenye silaha ya ndani ya Kongo na mengine 14 ya wapiganaji wa kigeni yanaendesha mapambano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2023 chini ya mpango wa serikali wa kuwapokonya wapiganaji silaha na kuwajumuisha katika maisha ya kawaida, unaofahamika kama mpango wa P-DDRCS.

Soma pia: UN yawawekea vikwazo waasi wa Kongo huku mapigano yakiendelea

Kati ya makundi ya wapiganaji yaliyoko mashariki mwa Kongo, M23 au vuguvugu la March 23 ndilo kundi maarufu kuliko yote. Na kundi hilo ambalo limehodhiwa zaidi na Watutsi linasema linapambana kuwatetea Wakongomani wenye asili ya Kitutsi dhidi ya kubaguliwa na dhidi ya makundi yenye misimamo mikali kama vile wanamgambo wa kihutu kutoka Rwanda FDLR.

Karte DR Kongo Kiswahili Freies Bildformat

Kwa muda mrefu rais Paul Kagame wa Rwanda amekuwa akilitazama kundi hilo la FDLR kama kitisho kwa taifa lake.

Baada ya kukaa kimya kwa miaka kadhaa, M23 ilianza kuibuka tena mwishoni mwa 2021. Tangu wakati huo, imekua ya kutisha zaidi. M23 inazidi kujiendesha kama jeshi la kawaida, badala ya kundi lenye silaha" na inajivunia "nguvu ya kijeshi na vifaa vya hali ya juu," kulingana na wataalam wa Umoja wa Mataifa.

Hivi karibuni, mapigano kati ya M23 na wanajeshi wa Kongo yameongezeka, huku waasi hao wakisonga mbele kwa kasi kuelekea Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, katika siku chache zilizopita.

"Familia nzima iliogopa sana hadi tukaamua kuondoka jijini," mkazi wa Goma Jean de Dieu Kulondwa aliambia DW.

Familia yake inaongeza kwa zaidi ya watu milioni 5.5 waliokimbia makazi yao mashariki mwa DRC katika janga ambalo ni moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

Ushiriki wa Rwanda katika kundi la M23

Umoja wa Mataifa, Human Rights Watch na waangalizi wengine huru wameainisha msaada wa Rwanda kwa waasi wa M23, "ikiwa ni pamoja na uhamisho wa silaha na risasi, kuwezesha uandikishaji, na hata msaada wa moja kwa moja wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda," unabainisha uchambuzi wa 2023 Taasisi ya amani ya kimataifa ya Global Observatory.

Soma pia: Rwanda yatupilia mbali wito wa Marekani jeshi Kongo

Hivi karibuni, jeshi la Rwanda limeshutumiwa kwa kutumia silaha za kisasa kama vile makombora ya kutoka ardhini hadi angani (SAM) ndani ya Kongo. Waraka ambao haujachapishwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani wa MONUSCO mashariki mwa Kongo, ulionukuliwa na shirika la habari la AFP mapema mwezi Februari, ulibainisha kuwa kutumia mfumo wa simu wa SAM ndani ya nchi hiyo "kunaonyesha kuongezeka kwa migogoro ya kawaida ya nguvu."

Maandamano ya kupinga ukosefu wa usalama yafanyika Goma

Kwa upande mwingine, serikali ya Rwanda inayoongozwa na Watutsi ya Rais Kagame inaishutumu Kongo kwa kuunga mkono kundi la FLDR, adui yake mkuu. Kundi hilo la waasi lilianzishwa na wapiganaji wa Kihutu na familia zilizokimbilia Kongo baada ya mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994, ambayo yalishuhudia karibu Watutsi milioni 1 wakiuawa na Wahutu wenye itikadi kali.

Operesheni ya siri ya Burundi nchini Kongo

Wanajeshi 1,000 wa Burundi wanaripotiwa kuwa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini kama sehemu ya operesheni ya siri. Shirika la habari la Reuters, likinukuu ripoti ya ndani ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na shirika hilo la habari, lilisema wanajeshi hao wa Burundi walifika DRC Oktoba 2023 na wanapigana wakiwa wamevalia sare za jeshi la Kongo.

Hii ni tofauti na vikosi vya Burundi vilivyotumwa rasmi mashariki mwa DRC kama sehemu ya jeshi la kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambalo lilijiondoa mnamo Desemba 2023 baada ya Rais wa Kongo Felix Tshisekedi kukataa kurudisha mamlaka yake.

Wanajeshi wa Burundi wanaripotiwa kupambana zaidi na waasi wenye silaha wenye makao yake nchini Kongo wanaoipinga serikali ya Burundi, kama vile wanamgambo wa RED-Tabara, ambao wanahusika na mashambulizi dhidi ya Burundi na ambao Burundi inaishutumu Rwanda kwa ufadhili na mafunzo.

Soma pia: Kitisho cha waasi wa M23 chazidi kuukabili mji wa Goma

Chini ya makubaliano ya nchi mbili yaliyotiwa saini mwaka wa 2021, serikali ya Kongo inalipia gaharama za kikosi hichi cha siri cha Burundi, kinachosemekana kugharimu dola 5,000 kwa mwezi kwa kila mwanajeshi wa Burundi.

"Kwa kuiunga mkono DRC, Burundi inajisaidia yenyewe, kwani inasaidia kuwaondoa waasi wa RED-Tabara," mwanasayansi wa siasa wa Kongo Christian Moleka aliiambia DW. Wakati huo huo, Burundi inasaidia "kukata ushawishi ambao Rwanda, kupitia wanamgambo wanaounga mkono Watutsi, wanaweza kutumia kwa vuguvugu la RED-Tabara."

Vita vya M23 vinaathiri pia wakazi wa Bukavu

Uganda katika operesheni ya pamoja dhidi ya wanamgambo wa ADF

Wanajeshi wa Uganda wamekuwa wakipigana mashariki mwa DRC tangu 2021 kama sehemu ya operesheni ya pamoja ya kusambaratisha kundi la wanamgambo wa Allied Democratic Forces (ADF) lenye mafungamano na ISIS. Kundi la ADF, lililoorodheshwa kuwa kundi la kigaidi na Marekani na Uganda, lilianzia Uganda katika miaka ya 1990 lakini sasa linaendesha shughuli zake kutoka Kivu Kaskazini na kufanya mashambulizi nchini Uganda na Kongo.

Titeca kutoka Chuo Kikuu cha Antwerp nchini Ubelgiji aliiambia DW, kuongeza operesheni hiyo ya pamoja kati ya vikosi vya Kongo na Uganda kumekuwa na ufanisi hasa katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Majeshi ya kikanda ya Afrika na mamluki wa Ulaya

Wakati Rais Tshisekedi alipokitimua kikosi cha kanda ya Afrika Mashariki mnamo Desemba 2023, aliwakaribisha mara moja wanajeshi kutoka Afrika Kusini, Malawi na Tanzania chini ya ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Katikati ya Februari, seŕikali ya Afŕika Kusini ilisema kuwa wanajeshi wake wengine 2,900 walikuwa wakiandaliwa kwa ajili ya operesheni ya SADC, ambayo ina mamlaka hadi Desemba 2024.

Makampuni mawili binasfi ya kijshi pia yana takriban wanajeshi 1,000 huko Goma. Ya kwanza Agemira iliyosajiliwa Bulgaria, inaendeshwa na raia wa Ufaransa na inajumuisha wanajeshi waliostaafu wa Ufaransa. Agemira imepewa kandarasi ya matengenezo ya ndege kwa jeshi la Kongo.

Waathiriwa wa ghasia nchini Kongo
Mwanamke huyu alijeruhiwa katika mapigano kati ya M23 na vikosi vya washirika wa Kongo katika mkoa wa Sake, karibu na GomaI.Picha: Moses Sawasawa/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Ya pili, Congo Protection, inasimamiwa na Mromania ambaye ni mwanajeshi wa zamani wa Kigeni la Ufaransa na huajiri wanajeshi wa zamani wa Ulaya Mashariki. Wakati Congo Protection imepewa kandarasi ya kutoa mafunzo kwa vitengo vya jeshi la Kongo, wanajeshi wake pia wamesimamia vituo vya ulinzi pamoja na wakufunzi wake wa jeshi la Kongo wakati iliposhambuliwa na waasi, kulingana na wataalam wa UN.

Wanamgambo wa ndani waongeza mchanganyiko

Mnamo 2022, Tshisekedi alitoa wito kwa vijana wa kiume na wa kike mashariki mwa Kongo kuunda vikundi vya tahadhari kupigana dhidi ya M23. Mwishoni mwa mwaka jana, amri ya serikali ilihalalisha uwepo wa wanamgambo ndani ya jeshi lake.

Soma pia:Hofu yaongezeka Kongo baada ya M23 kudhibiti mji unaonganisha Goma na Bukavu

Ilileta pamoja vikundi vya kujilinda vya ndani na washirika wenye silaha pamoja katika muungano unaojulikana kama Wazalendo - na kuwapa msaada wa kijeshi na kifedha. Hata washiriki wa kundi la wanamgambo wanaohofiwa wa FLDR wameripotiwa kujiunga.

Mchambuzi wa masuala ya usalama mwenye makao yake nchini Uganda David Egesa alisema kutoa silaha kwa makundi kupambana na M23 huenda ikasaidia katika muda mfupi lakini akaonya kuwa hilo linaweza pia kuimarisha makundi ya wanamgambo.

"DR Kongo inaweza kuruhusu wanamgambo kufanya kazi pamoja dhidi ya M23 kwa busara. Lakini mchezo huo unaweza, kwa muda mrefu, kuwatia moyo wanamgambo," Egesa aliliambia Shirika la Anadolu, shirika la habari la Uturuki. "Ni hali ya hatari."

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW