1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yalenga kukabiliana na ushawishi wa China

11 Julai 2024

Viongozi wa NATO wanalenga kuimarisha mahusiano yao na washirika wa bara la Asia ili kukabiliana na ushawishi wa China ambayo wameituhumu kwa kuwezesha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4iBdK
Mkutano wa kilele wa NATO mjini Washington, Marekani
Mkutano wa kilele wa NATO mjini Washington, MarekaniPicha: Nathan Howard/REUTERS

Katika kuhitimisha mkutano wao wa kilele mjini Washington, wanachama wa muungano huo wa kijeshi wenye mataifa 32 wametangaza hatua madhubuti za kuiunga mkono Ukraine, lakini wakatofautiana kwenye baadhi ya mambo.

Mkutano huo wa NATO  wa siku tatu ulioanza Jumanne na utakaohitimishwa leo, uligubikwa kwa sehemu kubwa na mijadala ya masuala ya usalama na pia ulilenga kudhihirisha uungwaji mkono kwa Ukraine katika vita vyake vya kukabiliana na uvamizi wa Urusi.

Mkutano huo ambao ulikuwa unasherehekea pia miaka 75 tangu kuundwa kwa NATO ulifanyika huku kukiwa na sintofahamu ya kisiasa nchini Marekani ambapo Rais Joe Biden anakabiliwa na shinikizo kubwa la kumtaka ajiondoe kwenye kinyang´anyiro cha kuwania urais kwa muhula wa pili kutokana na hali yake ya kiafya.

Kutoka kushoto: Rais Joe Biden, Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg na rais Volodymyr Zelensky
Kutoka kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg na rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Kay Nietfeld/picture alliance/dpa

Baada ya kutumia sehemu kubwa ya mkutano huo kuiimarisha Ukraine kwa kutoa ahadi za msaada zaidi wa kijeshi, ndege za kivita chapa F16, silaha na ufadhili mwingine, Norway imeahidi kutoa dola milioni 92.69 ili kuimarisha ulinzi wa anga wa Ukraine.

Soma pia: Viongozi wa NATO wahitimisha mkutano wao wa kilele huko Marekani

Aidha NATO ilielekeza pia darubini yake eneo la mashariki kwa kufanya mazungumzo na viongozi wa mataifa ya Australia, Japan, New Zealand na Korea Kusini ili kukabiliana na ushawishi unaoongezeka wa China.

Viongozi wa NATO wamesema China haiwezi kuwezesha vita vikubwa zaidi barani Ulaya katika historia ya hivi karibuni bila ya kuathiri vibaya maslahi na haiba yake.

Beijing imejibu mara moja na kuionya NATO kuachana na propaganda ya kile wanachokiita "Kitisho cha China" na kwamba hilo linazusha tu makabiliano na ushindani.

Mivutano I Marais Xi Jinping wa China, Biden wa Marekani na Putin wa Urusi
Kutoka kushoto: Rais wa China Xi Jinping, Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Sergei Guneyev/Pool/picture alliance/Chip Somodevilla/Getty Images/Sergei Guneev/Sputnik/REUTERS

China imekuwa ikinadi kutoegemea upande wowote katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine, lakini imesaidia pakubwa kuokoa uchumi wa Urusi ambayo imetengwa kutokana na vikwazo vya mataifa ya Magharibi. Ukraine kwa upande wake imesema imeridhishwa na matokeo ya mkutano huo.

Soma pia: China yafanya mazoezi makubwa ya kijeshi na Belarus

Kando ya mkutano wa NATO, mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la mataifa saba yaliyostawi kiviwanda ya G7 walikutana pia. Waziri wa mahusiano ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema:

"Nadhani unaweza kuona ushirikiano madhubuti wa G7 na uratibu wetu katika masuala muhimu ya zama hizi, ikiwa bila shaka ni pamoja na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na changamoto zinazoshuhudiwa huko Mashariki ya Kati na kazi yote tunayofanya pamoja kwenye kanda ya Bahari ya Hindi na Pasifiki. Kundi la G7 linaisifu kwa dhati kazi inayofanywa hapa kwenye mkutano wa NATO."

Katika hatua nyingine Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Poland wametia saini makubaliano ya pamoja ili kuanzisha utengenezaji wa makombora ya masafa marefu.

Tofauti zilizoshuhudiwa kati ya wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan akihudhuria mkutano huo wa NATO
Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan akihudhuria mkutano huo wa NATOPicha: Murat Cetinmuhurdar/TUR Presidency/Anadolu/picture alliance

Lakini mbali na hayo kumedhihirika pia misuguano baina ya wanachama wa NATO kuhusiana na masuala kadhaa kama vita vya huko Mashariki ya Kati. Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amemshutumu  Rais wa Marekani Joe Biden  na utawala wake kwamba kwa kuipatia Israel msaada zaidi wa kijeshi, wanashiriki katika kile alichokiita uhalifu wa kivita na ukiukaji wa sheria za kimataifa katika mzozo wa Gaza, huku akitaka Israel iwekewe vikwazo.

Alipoulizwa kuhusu uhusiano mzuri kati ya Uturuki na mataifa ya Urusi, China, kundi la mataifa ya BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO), Erdogan amesema Uturuki inaendesha diplomasia yake kwa kulenga faida kwa pande zote na kwamba haiwezi kuondoa uwezekano wa kushirikiana na taasisi zisizo za kimagharibi.

(Vyanzo: Mashirika)