1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yazidi kuiunga mkono Ukraine

28 Septemba 2023

Jumuiya ya Kujihami ya NATO imesema inaridhishwa na Ukraine kuhimili mashambulizi ya Urusi, huku Moscow ikitangaza kuongeza bajeti ya ulinzi kwa takribani asilimia 70 kukabiliana na kile inachokiita 'vita vya Magharibi'.

https://p.dw.com/p/4WvSB
Stoltenberg in Kiew
Picha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Huku "operesheni maalum ya kijeshi" ya Moscow ikiingia mwezi wake wa ishirini, kila upande umekuwa ukijikita kwenye kununuwa na kukusanya silaha kutoka kwa washirika wao ikionesha kuwa wanajitayarisha kwa mgogoro mkubwa zaidi kuliko ambao umeshajiri hadi sasa.

Tangazo la leo la Urusi limekuja wakati Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa NATO na mawaziri wa ulinzi wa Ufaransa na Uingereza wakiitembelea Kiev, ambapo Rais Volodymyr Zelensky aliwaomba kuipatia nchi yake mifumo zaidi ya ulinzi. 

Soma zaidi: Mataifa ya G7 yaahidi kupeleka silaha kwa muda mrefu kuisaidia Ukraine katika vita vyake na Urusi
Urusi:Tumedungua drone 5 za Ukraine, hakuna madhara

Zelensky aliwaambia washirika wake hao kwamba wanataka kuhakikisha kuwa katika majira yajayo ya kipupwe wanaweza kuilinga miundombinu yao ya nishati na maisha ya watu wao. 

Wakati wa majira kama hayo mwaka jana, Urusi ilizidisha mashambulizi yake dhidi ya miundombinu ya umeme na gesi na matokeo yake mamilioni ya raia walikosa maji na huduma ya kupashia joto nyumba zao.

NATO yaiunga mkono Ukraine

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, alisema kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari kwamba mafungamano kati ya muungano huo wa kijeshi na Kiev yamezidi kuimarika kuliko wakati wowote mwengine.

Stoltenberg in Kiew
Ujumbe wa NATO ukiwa na mazungumzo na wenzao wa Ukraine mjini Kiev.Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP Photo/picture alliance

"Tumeimarisha mafungamano yetu ya kisiasa kwa kiwango ambacho hakikuwahi kufikirika hapo kabla kwa kuanzisha Baraza la NATO na Ukraine, chombo ambacho tunaweza kukitumia kushauriana na kuchukuwa maamuzi makubwa pamoja. Baraza hili tayari limeshakutana kwa masuala muhimu, yakiwemo ya usalama wa Bahari Nyeusi, na litakutana tena hivi karibuni. Maamuzi haya yanamaanisha kwamba sasa Ukraine ipo karibu zaidi na NATO kuliko ilivyokuwa hapo kabla." Alisema Katibu Mkuu huyo wa NATO.

Soma zaidi: Zelenskiy aishukuru Ujerumani, Ufaransa na Uingereza
Watu 11 wauawa katika mashambulizi ya makombora ya Urusi dhidi ya Ukraine katika mji alikozaliwa rais Zelenskyy

Waziri mpya wa ulinzi wa Ukraine, Rustem Umerov, alimwambia mwenzake wa Uingereza, Grant Shapps, kwamba majira ya baridi kali yanakuja lakini wako tayari kwa makubaliano.

Vita vikali majira ya baridi

Ukraine imekuwa mara kwa mara ikiomba silaha zaidi kutoka mataifa ya Magharibi, yakiwemo makombora ya masafa marefu ili kukabiliana na mashambulizi makali kutoka Urusi. 

Stoltenberg in Kiew
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine (kulia) akimkaribisha Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg.Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP Photo/picture alliance

Stolteberg amesema anaridhishwa na jinsi Ukraine inavyotumia silaha ilizopewa kujilinda na kurejesha baadhi ya maeneo yaliyotwaliwa na Urusi, licha ya kukabiliwa na taifa lenye nguvu kubwa zaidi yake.

Soma zaidi: Volodymyr Zelenskiy ashinikiza kupatiwa ndege za kivita
Zelensky ziarani Slovakia kabla ya kuelekea Uturuki

Daima Urusi imekuwa ikisisitiza kwamba haipigani na Ukraine peke yake kwenye vita hivi, bali upande wa Kiev umekuwa ukisaidiwa na mataifa kadhaa ya kigeni, bila ya kuitaja nchi makhsusi kwenye madai yake hayo.

Hata hivyo, inafahamika wazi kuwa mataifa ya Magharibi na washirika wao wamekuwa wakiisaidia Ukraine vifaa, fedha na silaha tangu uvamizi uanze mwezi Februari 2022.

Vyanzo: AFP, Reuters