Netanyahu aapa kuushambulia mji wa Rafah
30 Aprili 2024Netanyahu ametoa kauli hiyo licha ya mshirika wake mkuu Marekani kudhihirisha wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kutekelezwa hatua hiyo.
Waziri huyo Mkuu wa Israel ambaye ameapa kulitokomeza kabisa kundi la Hamas baada ya shambulio lao la Oktoba 7, amewaambia familia za baadhi ya mateka ambao bado wanashikiliwa huko Gaza kwamba kamwe hawatositisha vita kabla ya kufikia malengo yao yote na kupata ushindi kamili dhidi ya kundi hilo.
Onyo hiyo imetolea saa chache kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kuwasili Israel katika ziara yake ya hivi punde ya kujaribu kutafutia suluhu mzozo huu wa Mashariki ya Kati. Akiwa nchini Jordan, Blinken ametoa wito wa kuongezwa maradufu kwa juhudi za kuwasilishwa misaada huko Gaza.
Hofu ya raia wa Kipalestina
Taarifa za uwezekano wa kushambuliwa mji wa Rafah ambao unawahifadhi watu zaidi ya milioni moja waliokimbia mapigano katika sehemu zingine za ukanda wa Gaza, zimezusha hofu miongoni mwa raia kama anavyoelezea Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwasaidia Wapalestina UNRWA, Philippe Lazzarini :
" Kimsingi wafanyakazi wetu wanatueleza kwamba kuna hali ya wasiwasi mkubwa iliyotanda huko Gaza kwa sababu swali ambalo kila mtu anajiuliza ni ikiwa kutakuwa au la mashambulizi ya kijeshi, Na uwezekano wa mashambulizi hayo yatategemea ikiwa wiki hii kutafikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Watu bado hawajatakiwa kuondoka Rafah, lakini kuna hisia kwamba, ikiwa hakuna mpango wa makubaliano wiki hii, basi operesheni hiyo inaweza kutokea wakati wowote."
Soma pia: Netanyahu atishia kuishambulia Rafah
Kauli hiyo ya Benjamin Netanyahu imetolewa wakati kundi la Hamas bado linatafakari na linasubiriwa kutoa jibu kuhusu mpango wa hivi punde zaidi wa makubaliano ya usitishwaji mapigano kwa siku 40, uliopendekezwa katika mazungumzo ya mjini Cairo na wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar.
Mpango huo unahusisha pia kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina. Afisa wa Israel amesema nchi hiyo itasubiri hadi 'Jumatano usiku' jibu la Hamas kuhusu pendekezo hilo la usitishaji mapigano huko Gaza.
Vuguvugu la kuwaunga mkono Wapalestina
Katika hatua nyingine, kumeshuhudiwa kwa muda wa wiki kadhaa sasa maandamano makubwa ya kuwaunga mkono Wapalestina katika vyuo vikuu kote nchini Marekani na kwingineko, ikiwa ni pamoja na nchini Ufaransa na Lebanon.
Wakati harakati za diplomasia zikiendelea, Israel imefanya mashambulizi katika miji ya Khan Yunis na Rafah, huku jeshi la Israel likithibitisha kuwa ndege zao za kivita zilishambulia ngome za magaidi katikati mwa ukanda wa Gaza.
(Vyanzo: Mashirika)