1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yaendelea na zoezi la kuhesabu kura

26 Februari 2023

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Nigeria baada ya uchaguzi wa Jumamosi wenye ushindani wa kihistoria kati ya wagombea watatu wanaowania urais wa taifa hilo linaloongoza kwa idadi ya watu barani Afrika.

https://p.dw.com/p/4NzZb
Nigeria | Auszählung Wahlen
Picha: Sunday Alamba/AP Photo/picture alliance

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Nigeria baada ya uchaguzi wa Jumamosi wenye ushindani wa kihistoria kati ya wagombea watatu wanaowania urais wa taifa hilo linaloongoza kwa idadi ya watu barani Afrika.

Karibu watu milioni 90 walipiga kura zao katika uchaguzi huo ambao kwa sehemu kubwa ulikuwa wa amani, licha ya visa vya vurugu hapa na pale, na hitilafu za kiufundi zilizochelewesha upigaji kura hadi saa za usiku.

Katika mji wa kaskazini wa Kano, vifaa vya kupigia kura viliwasili katika kituo kimoja masaa matano baada ya muda rasmi wa kuanza zoezi la uchaguzi.

''Upigaji kura unaendelea baada ya muda wa mwisho uliotangazwa,'' alisema Kabiru Sani, mpigakura aliyezungumza na shirika la habari la AFP, na kuongeza kuwa ''tulichelewa kuanza, na hatutaruhusu kunyimwa haki yetu ya kikatiba.''

Soma pia:Nigeria yapiga kura kuchagua rais na bunge

Kulingana na taarifa ya Tume Huru ya Uchaguzi nchini Nigeria, INEC, vibanda kadhaa vya kupigia kura viliharibiwa na kuporwa, na mashine za kusoma vitambulisho ziliibiwa katika baadhi ya majimbo mengine.

Aidha, tume hiyo imesema uchaguzi unafanyika leo Jumapilikatika vituo 141 kwenye jimbo la Bayelsa la kusini mwa Nigeria, baada ya vurugu zilizojitokeza.

Hata hivyo, kwa Nigeria ambayo siku za nyuma iliandamwa na visa vya vurugu na mivutano ya kikabili, uchaguzi huu unaoenekana kufanyika kwa amani na utulivu.

Matumaini ya Wanaijeria katika sanduku la kura

Baada ya mihula miwili ya Rais Muhammadu Buhari, Wanigeria wengi wanayo matumaini kuwa  mrithi wake atafanikiwa zaidi katika kukabiliana na matatizo ya kiusalama, ukosefu wa ajira  na umasikini unaoongezeka nchini mwao.

Nigeria | Wahltag
Wapiga kura Nigeria wakikamilisha haki yao ya kidemocrasiaPicha: Uwais Abubakar Idris/DW

Kinyang'anyiro kikali kipo baina ya meya wa zamani wa Lagos, Bola Tinubu mwenye umri wa miaka 70 anayegombea kwa tiketi ya chama cha APC, na mpinzani wake wa muda mrefu, Atiku Abubakar mwenye miaka 76 kutoka chama cha PDP, ambaye ni mara yake ya sita kutupa kete yake kuelekea wadhifa huo mkubwa zaidi wa uongozi wa taifa.

Lakini kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999, mgombea wa tatu, Peter Obi wa chama cha Labour anaonekana kuupa changamoto udhibiti wa vyama hivyo viwili, akiendesha kampeni yake chini ya kauli mbiu ya mageuzi.

Soma pia:Uchaguzi Mkuu kufanyika Nigeria licha ya uhaba wa fedha

Watu walikusanyika katika makundin nje ya vituo vya kupiga kura majini Lagos na kwingineko, wakati maafisa wa uchaguzi walipokuwa wakihesabu kwa mikono na kutangaza idadi ya kura, kabla ya kuzipeleka katika makao makuu.

''Tumemaliza kuhesabu, lakini tunatakiwa kuhakikisha kuwa matokeo yanaingizwa katika mfumo,'' alisema Chizoba Ohuoha, afisa wa TEHAMA aliyekuwa akifuatilia upigaji kura katika kituo kimoja mjini Lagos.

Kuwepo kwa wagombea watatu wanaopewa nafasi ya kupata kura nyingi kunawafanya baadhi ya wachambuzi kutabiri uwezekano wa duru ya pili ya uchaguzi, ikiwa hakuna mgombea hata mmoja atakayepata kiwango cha kura kinachohitajika kupata ushindi wa moja kwa moja.

Kupatikana mrithi wa rais Buhari.

Ili kushinda urais wa Nigeria, mgombea anapaswa kupata kura nyingi zaidi kuliko wapinzani wake, na kujikusanyia angalau asilimia 25 ya kura katika majimbo 24 kati ya 36 yanayounda shirikisho la Nigeria.

Nigerias Präsident Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: Julien de Rosa/ Pool/REUTERS

Ikiwa hakuna mgombea hata mmoja atakayekidhi vigezo hivyo, duru ya pili itaandaliwa katika muda wa siku 21 baina ya wagombea wawili waliopata kura nyingi zaidi. Hadi sasa hakuna uchaguzi wa Nigeria uliowahi kuingia katika duru ya pili.

Mwenendo wa uchaguzi huu wa Nigeria unafuatiliwa kwa karibu katika kanda ya Afrika Magharibi, ambako mapinduzi ya kijeshi nchini Mali, Burkina Faso na Guinea, na kuongezeka kwa uasi wa makundi ya itikadi kali vimeyumbisha mchakato wa demokrasia.

Soma pia:Nani atakuwa Rais mpya wa Nigeria?

Rais Muhammadu Buhari ambaye ni mkuu wa zamani wa jeshi, anaondoka baada ya mihula miwili madarakani. Wakosoaji wake wanasema alishindwa kutimiza ahadi yake ya kuifanya Nigeria nchi yenye amani zaidi.