Putin asaini sheria ya kuinyakua asilimia 15 ya Ukraine
5 Oktoba 2022Duru kutoka bunge la Urusi mjini Moscow zimethibitisha kuwa Rais Putin amesaini sheria ya kikatiba inayozitambua jamhuri zilizojitangaza za Donetsk na Ruhansk, pamoja na mikoa ya Kherson na Zaporizhzhia kuwa sehemu ya Urusi.
Soma zaidi:Bunge la Urusi laidhinisha unyakuzi wa majimbo manne ya Ukraine
Urusi iliyanyakua maeneo hayo ya mashariki mwa Ukraine baada ya ilichokinadi kama kura ya maoni katika sehemu inazozikalia. Ukraine pamoja na nchi za magharibi ziliipinga kura huyo, zikiitaja kuwa ya kulazimisha na inayokwenda kinyume na sheria ya kimataifa.
Maeneo haya mapya yanayodaiwa kuingizwa ndani ya Urusi, pamoja na rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi mwaka 2014, ni asilimia 22 ya eneo zima la Ukraine.
Sehemu ya Urusi milele na milele
Katika sherehe za kusaini mkataba wa muungano baina ya Urusi na maeneo hayo Ijumaa iliyopita, Rais Putin alisema kamwe Urusi haitayaachia kurudi kuwa sehemu ya Ukraine, licha ya kwamba Urusi ilisaini makubaliano ya Budapest ya mwaka 1994 ya kuitambua mipaka ya kimataifa ya Ukraine baada ya kuvunjia kwa uliokuwa Umoja wa Kisovieti.
Soma zaidi: Urusi yajiandaa kuyanyakua rasmi maeneo ya Ukraine
Hayo yanajiri wakati wanajeshi wa Ukraine wakiripotiwa kupiga hatua kubwa katika operesheni ya kuzikomboa sehemu zinazokaliwa na Urusi katika mkoa wa Kherson, wakivilazimisha vikosi vya Urusi kuzipa kisogo ngome ambazo wamezijenga tangu mwezi Machi.
Katika hotuba yake usiku wa kuamkia leo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema katika muda wa wiki moja tu, miji na vijiji vipatavyo 12 vimerejeshwa mikononi mwa Ukraine.
Nchi za magharibi zaongeza shinikizo dhidi ya Urusi
Marekani imetangaza msaada mpya wa kijeshi kwa Ukraine, unaojumuisha mifumo minne ya makombora aina ya Himars, mizinga 32 pamoja na shehena kubwa ya vipuri na risasi, kwa azma ya kuviwahi vikosi vya msaada vitakavyotumwa na Urusi.
Soma zaidi:''Kura ya maoni" kukamilika kwenye maeneo ya Ukraine
Afisa wa mkoa wa Kherson aliyewekwa na Urusi, Kirill Stremousov amesema leo kupitia shirika la habari la Urusi, TASS, kwamba wanajeshi wa Ukraine hawasongi mbele tena, na kuongeza kuwa vikosi vya Urusi vilikuwa vikijikusanya kuwarudisha nyuma.
Katika taarifa nyingine kuhusiana na mzozo huu, Jamhuri ya Czech ambayo ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya, imearifu kuwa umoja huo umekubaliana juu ya awamu ya vikwazo vipya dhidi ya Urusi, kuhusiana na hatua ya nchi hiyo ya hivi karibuni kuyanyakua maeneo ya Ukraine.
Vyanzo: rtre, afpe,ape