1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yajiandaa kuyanyakua rasmi maeneo ya Ukraine

30 Septemba 2022

Urusi inatazamiwa leo kuyanyakua rasmi maeneo manne ya Ukraine baada ya kumalizika kile ilichokiita "Kura ya Maoni".

https://p.dw.com/p/4Ha1p
Russland | Wladimir Putin
Picha: Gavriil Grigorov/POOL/TASS/dpa/picture alliance

Rais wa Urusi Vladimir Putin anatarajiwa kuandaa sherehe katika ukumbi wa kifahari wa Kremlin ili kutangaza unyakuzi wa Urusi wa karibu asilimia 15 ya ardhi ya Ukraine, ikiwa ni unyakuzi mkubwa zaidi kushuhudiwa barani Ulaya tangu enzi za utawala wa Hitler.

Unyakuzi wa maeneo ya Ukraine yanayokaliwa na Urusi ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhzhia umelaaniwa na Mataifa ya Magharibi na hata kimataifa.

Unyakuzi huu rasmi unatarajiwa kufanyika baada ya kukamilika kile ambacho Urusi imekiita "Kura ya Maoni" ambayo nchi za Magharibi zinasema ni udanganyifu uliotendeka kwa vitisho vya mtutu wa bunduki na katika maeneo yanayokaliwa kimabavu na Urusi.

Maafisa wa Urusi, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov, wamebainisha tishio la matumizi ya silaha za nyuklia ili kuyalinda maeneo wanayopanga kuyanyakua huku Ukraine ikiapa kuwa itayakomboa maeneo yake yote.

Soma zaidi: ''Kura ya maoni" kukamilika kwenye maeneo ya Ukraine

Hatua yalaaniwa kimataifa

UN-Generalsekretär Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: Xie E/XinHua/dpa/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitaja hatua hiyo kuwa ni "hatari" na ukiukaji wa mkataba wa Umoja wa Mataifa:

" Ili kuwa wazi, Urusi ni moja ya wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama na inashiriki jukumu maalum la kuheshimu mkataba wa Umoja wa Mataifa. Uamuzi wowote wa kuendelea na unyakuzi wa mikoa ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhzhia ya Ukraine hautakuwa na thamani yoyote kisheria na unastahili kulaaniwa. Unakinzana na mfumo wa sheria za kimataifa. Unakinzana na yale yote ambayo jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuyatetea. Unakinzana na madhumuni na kanuni za Umoja wa Mataifa. Ni matokeo ya hatari. Uamuzi huo hauna nafasi katika ulimwengu wa kisasa na haupaswi kukubaliwa."

Soma zaidi: 'Kura ya maoni' ya Urusi yatwaa majimbo manne ya Ukraine

Mashambulizi yaua watu 23 Ukraine

Ukraine | Russischer Angriff auf einen zivilen Autokonvoi in Saporischschja
Matokeo ya shambulio la Urusi dhidi ya msafara wa kuwahamisha watu karibu na jiji la Zaporizhzhia, Ukraine, Septemba 30, 2022.Picha: Pavel Nemecek/CTK/dpa/picture alliance

Wakati hayo yakiripotiwa,Ukraine na Urusi zimeshtumiana leo kuhusika na mashambulizi huko Zaporizhzhia na kusababisha vifo vya watu takriban 23.

Msafara huo uliokuwa umebeba raia na vifaa ulishambuliwa karibu na mji wa kusini mwa Ukraine unaokaliwa na vikosi vya Urusi wa Zaporizhzhia.

Gavana wa Mkoa wa Zaporizhzhia Oleksandr Starukh amesema shambulio hilo limeendeshwa na majeshi ya Urusi na hivo kusababisho vifo vya watu 28, ambao wote ni wakazi wa eneo hilo.

Naye Vladimir Rogov, Afisa anayeiunga mkono Kremlin akiilaumu Kiev kwa uchochezi na kukanusha kuwa jeshi la Urusi lilihusika na shambulio hilo.

Eneo la kiwanda cha Zaporizhzhia, lililokuwa na wakazi 700,000 kabla ya vita, liko chini ya udhibiti wa Ukraine lakini limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya Urusi.

Aidha, shirika la habari la serikali ya Urusi limebaini kuwa Afisa aliyeteuliwa na Moscow huko Kherson, eneo la kusini mwa Ukraine linalodhibitiwa na Urusi, ameuawa katika mashambulizi ya vikosi vya Kiev.