1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin: Urusi ina hifadhi ya kutosha ya mabomu ya mtawanyiko

Angela Mdungu
16 Julai 2023

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema nchi yake ina shehena ya kutosha ya mabomu ya mtawanyiko ya kujibu mashambulizi ikiwa Ukraine itatumia silaha kama hizo kuwashambulia wanajeshi wake wanaopigana Ukraine.

https://p.dw.com/p/4TxtM
Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: ALEXEY BABUSHKIN/SPUTNIK/AFP

Rais Putin ameyasema hayo katika mahojiano yaliyochapishwa leo na televisheni ya taifa leo Jumapili. Ameongeza kuwa, bado Urusi haijatumia aina hiyo ya silaha licha ya kuwa na uhaba wa aina mabomu kwa kiasi fulani.

Itakumbukwa kuwa, Ukraine ilianza kupokea mabomu tata ya mtawanyiko kutoka Marekani, hali ambayo imesababisha wasiwasi kutokana na athari za muda mrefu zinazotokana na matumizi ya mabomu hayo kwa raia. Sehemu ya aina hiyo ya mabomu yanayoshindwa kulipuka papo hapo, yanaweza kusababisha hatari miongo mingi baadaye hasa kwa watoto.

Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch na majeshi ya Ukraine yameituhumu Urusi kuwa tayari inatumia mabomu ya mtawanyiko kwenye uwanja wa mapambano. Mabomu hayo, yamepigwa marufuku kutumika kwa karibu nchi 100.

Soma zaidi: Mkataba wa mabomu ya mtawanyiko kutiwa saini Oslo

Nchi hizo ni zile zilizotia saini azimio la Oslo la mwaka 2008. Hata hivyo Urusi na Marekani siyo sehemu ya mkataba huo. Makundi ya haki za binadamu yamelaani uamuzi wa Marekani wa kuipatia Ukraine mabomu hayo.

Mabomu ya mtawanyiko
Mabomu ya mtawanyikoPicha: MOHAMMED ZAATARI/AP/picture alliance

Licha ya lawama hizo, Rais wa Marekani Joe Biden alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa "mgumu mno" lakini akasisitiza kuwa Ukraine inahitaji mabomu ya ziada ili kuijaza tena hifadhi yake iliyopungua.

Katika hatua nyingine, Urusi imesema kwamba imezidungua takriban droni 10 kwenye mji wa Sevastopol katika rasi ya Crimea ambayo iliinyakua tutoka kwa Ukraine mwaka 2014.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imeeleza kwamba jeshi la ulinzi wa anga liliziangusha ndege mbili zisizo na rubani na kuzizima nyingine tano.

Shambulizi la droni lililofanywa kwenye mtambo wa mafuta Crimea April 29,2023
Shambulizi la droni lililofanywa kwenye mtambo wa mafuta Crimea April 29,2023Picha: MIKHAIL RAZVOZHAEV/TELEGRAM/REUTERS

Wizara hiyo imeongeza kuwa, jeshi lake liliharibu droni za majini na kuzima shambulio ambalo halikusababisha majeruhi wala uharibifu.

Kumekuwepo na mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani katika rasi ya Crimea ambayo jumuiya ya kimataifa haiitambui kuwa sehemu ya Urusi. Mara kadhaa, Ukraine imekuwa ikisema inapanga kuirejesha tena rasi hiyo chini ya himaya yake.