Rais Lula wa Brazil ziarani nchini Marekani
10 Februari 2023Lula atakutana na Biden baada ya mkutano na Seneta Bernie Sanders na wabunge kadhaa wa Kidemokrasia. Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil imebaini kuwa miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa katika ziara hiyo ni uungaji mkono kwa demokrasia, haki za binadamu pamoja na mazingira.
Brazil ina shauku kuona nchi zaidi zikichangia kunako Fuko laAmazon lililoanzishwa na Ujerumani na Norway ili kusaidia ulinzi wa misitu ya mvua na miradi ya maendeleo endelevu. Serikali ya Marekani inatarajia kujiunga na fuko hilo la kimataifa la kupambana na ukataji miti katika msitu wa Amazon nchini Brazil, na mchango wa Marekani katika fuko hilo unatarajiwa kutangazwa wakati wa mkutano kati ya Biden na Lula.
Wiki hii, Brazil ilisisitiza ahadi yake ya kulinda msitu wa mvua wa Amazon kwa kuanzisha operesheni dhidi ya wachimbaji haramu wa dhahabu ambao wameharibu uhifadhi wa kiasili wa Yanomami kaskazini mwa nchi hiyo.Lula amesafiri hadi Washington akiambatana na Waziri wa Mazingira Marina Silva, ambaye anatarajiwa kukutana na mjumbe wa hali ya hewa wa Biden John Kerry. Mawaziri wengine waliopo kwenye msafara huo ni yule wa Mambo ya Nje pamoja na waziri wa Fedha.
Soma pia:Polisi Brazil yasambaratisha kambi za wafuasi wa Bolsonaro
Mchango wa Marekani katika Fuko hilo utafufua uhusiano kati ya Brazil na Marekani uliyokuwa umedorora wakati wa utawala wa mtangulizi wa Lula kutoka mrengo mkali wa kulia Jair Bolsonaro, ambaye pia alikuwa mshirika wa Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
Mitazamo ya Lula na Biden kukinzana
Hata hivyo, kuna tofauti za kimtazamo kati ya Biden na Lula kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Michel Arslanian, ambaye ni katibu katika Wizara ya Mambo ya nje ya Brazil, alipoulizwa kuhusu shinikizo la serikali ya Marekani kwa Brasil ili kuiunga mkono Ukraine katika vita yake na Urusi, mwanadiplomasia huyo alisema Brazil daima haitoegemea upande wowote huku ikihimiza mazungumzo ili kufikia amani.
Soma pia: Scholz: Nimefurahi kuona Brazil imerejea katika jukwaa la kimataifaa:
Mkutano wa Lula na Biden unaashiria uungaji mkono kwa taasisi za kidemokrasia za Brazil, ambazo zilikabiliwa na msukosuko kutokana na Bolsonaro kukataa kushindwa katika uchaguzi wa mwezi Oktoba huku wafuasi wake wakivamiwa majengo ya serikali Januari 8, ikiwa ni wiki moja tu baada ya kuapishwa kwa rais Lula da Silva.
Mbali na masuala ya mazingira ya kuulinda msitu wa Amazon na vita vya Ukraine, viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili juhudi za kudumisha demokrasia, ukosefu wa usalama huko Haiti, uhamiaji na mabadiliko ya tabianchi.