Rais Putin afanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa China Li
22 Agosti 2024Akizungumza jana kwenye mkutano wao uliofanyika Ikulu ya Kremlin, Putin alisema juhudi zinazofanywa na serikali za nchi hizo mbili za kuukuza uhusiano wa kibiashara zinazaa matunda.
Mkutano huo ulifanyika wakati Urusi ikipambana kudhibiti uvamizi uliofanywa na jeshi la Ukraine katika mkoa wa Kursk ambao sasa uko katika wiki yake ya tatu.
Na usiku wa kuamkia leo, Moscow ilikabiliwa na mojawapo ya mawimbi makubwa kabisa ya mashambulizi ya droni kuwahi kufanywa kwenye mji huo mkuu wa Urusi tangu kuanza kwa mgogoro wa Ukraine.
Soma pia:Waziri Mkuu wa China kuzuru Urusi na Belarus
Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema mifumo yake ya ulinzi wa angani ilidungua droni 45 zilizorushwa kutokea Ukraine. Droni 11 kati yao ziliharibiwa katika eneo la Moscow.
Ripoti za habari za Urusi hazikuonesha ikiwa Putin na Li waliujadili mgogoro wa Ukraine. China inajaribu kujiweka kama nchi isiyoegemea upande wowote katika mzozo wa Ukraine, lakini inaungana na Urusi katika msimamo wake wa kiadui dhidi ya nchi za Magharibi.