Rais Sata aondolewa marufuku ya kuingia Malawi
29 Septemba 2011Serikali ya Rais Bingu wa Mutharika ilimkamata Sata hapo mwaka 2007, wakati huo Sata akiwa kiongozi wa upinzani kwa kosa la kuingia Malawi na kumtembelea rais wa zamani wa Malawi. Sata alilazimishwa kuingia kwenye gari, akaendeshwa kilomita kadhaa kabla hajatupwa mpakani na kuambiwa kamwe asingeliruhusiwa kuingia Malawi maishani mwake.
Msemaji wa Rais Mutharika, Hetherwick Ntaba, amesema kwamba sasa Sata hachukuliwi tena kuwa ni mgeni asiyetakiwa nchini Malawi, kwa vile tayari ni kiongozi wa nchi.
Interpol yatoa hati ya kumkamata Saadi Gaddafi
Polisi ya Kimataifa (Interpol) imetoa hati ya kukamatwa kwa Saadi Gaddafi, mtoto wa kiongozi wa Libya aliyeondolewa madarakani, Muammar Gaddafi.
Taarifa iliyotolewa na Interpol hii leo kutoka makao makuu yake, Lyon, Ufaransa, imesema kuwa serikali mpya ya Libya imeomba hati ya watu wanaotafutwa sana duniani dhidi ya Saadi, kwa tuhuma za kupata mali kwa kutumia nguvu na vitisho vya kijeshi alipokuwa akiliongoza Shirikisho la Mpira wa Miguu la Libya.
Saadi alikimbilia nchini Niger mapema mwezi huu. Mahala alipo baba yake bado hapajuilikana.
Wapinzani kugomea uchaguzi Misri
Heshima ya uchaguzi wa mwanzo wa Misri, tangu kuondoshwa madarakani Hosni Mubarak, imeingia katika hali ya wasiwasi leo baada ya muungano unaoongozwa na Chama cha Udugu wa Kiislamu kutishia kuususia uchaguzi huo.
Taarifa iliyotolewa jana usiku na Muungano wa Kidemokrasi ilisema wanachama wake hawatasimama katika uchaguzi wa mwezi Novemba, endapo ibara inayobishaniwa katika sheria mpya ya uchaguzi haitarekebishwa.
Muungano huo unaipinga Ibara ya Tano ya Sheria ya Uchaguzi, ambayo inavipiga marufuku vyama vya kisiasa kupigania thuluthi moja ya viti vya bunge ambavyo vimetengwa kwa watetezi wanaojitegemea wenyewe.
Ibara hiyo imeshapingwa na zaidi ya vyama 20 vya kisiasa ambavyo vinasema inaweza kuwarejesha bungeni watu waliokuwemo katika utawala wa zamani.
Muungano huo wa kidemokrasi unajumuisha vyama vya Udugu wa Kiislamu na kile cha kiliberali cha Wafd.
Risasi zarushwa Cameron
Watu wenye silaha waliovalia sare za kijeshi wameshambulia daraja kuu la Wouri katika mji wa kibiashara wa Douala, nchini Cameron, wakimtaka Rais Paul Biya ajiuzulu.
Afisa mmoja wa usalama amesema kuwa mmoja wa washambuliaji hao alikuwa amebeba bango lenye ujumbe huo kwa Rais Biya.
Bado idadi ya washambuliaji hao haijafahamika na viongozi wa serikali hawakupatikana mara moja kutoa maelezo.
Cameroon inaingia kwenye uchaguzi mkuu hapo tarehe 9 Oktoba na Rais Biya anatarajiwa kushinda tena. Rais Biya ameliongoza taifa hilo la Afrika ya Magharibi kwa karibuni miaka 30 sasa na mwaka 2008 alibadilisha katiba ili kumruhusu kuendelea kutawala.
Televisheni moja nchini humo imesema kuwa baadaye vikosi vya usalama vililidhibiti daraja la Wouri na kwamba washambuliaji hao wamekimbia.
Mwanamke wa Kiafrika apata Nishani Mbadala ya Nobel
Mwanasheria wa kike kutoka Chad ametunukiwa Nishani Mbadala ya Nobel kwa mchango wake katika utetezi wake wa haki za binaadamu.
Mwanamke huyo, Jacqueline Moudeina, mmoja wa wanasheria wa kwanza wa kike nchini Chad, anatambuliwa kwa jitihada zake za kupigania kupandishwa kizimbani kwa aliyekuwa rais wa zamani wa Chad, Hissen Habre.
Wengine waliotunukiwa nishani hiyo ni mkunga wa kike nchini Marekani, Ina May Gaskin, mfanyabiashara wa Kichina aliyewekeza kwenye nishati ya jua, Huang Ming, na jumuiya inayopingana na uporaji wa ardhi unaofanywa na mataifa na makampuni makubwa katika nchi na jamii na masikini duniani, GRAIN.
"Gaddafi yuko mpakani mwa Algeria"
Watawala wapya wa Libya wanasema kwamba wanaamini kiongozi wa nchi hiyo aliyeondoshwa madarakani, Muammar Gaddafi, analindwa na wakaazi wa jangwani karibu na mpaka wa Libya na Algeria. Wafuasi wa Gaddafi wanajaribu kurudisha mashambulizi katika mji aliozaliwa kiongozi huyo wa Sirte.
Wakati huo huo, serikali mpya ya Libya imesema hapo jana kwamba itashirikiana na serikali ya Scotland katika uchunguzi wa mkasa wa kuripuliwa kwa ndege kwenye anga ya Lockerbie hapo mwaka 1988.
Waziri wa Sheria wa serikali ya mpito ya Libya amesema kwamba watawatoa mashahidi kwa ajili ya mahojiano endapo Scotland itaomba.
Msimamo huu mpya ni kinyume na ule uliotolewa mapema wiki hii, ambapo serikali ya mpito ya Libya ilisema kwamba inachukulia kuwa kesi ya Lockerbie ilikuwa imemalizika.
Ndege ya Shirika la Ndege la Pan Am iliripuka kwenye anga ya Lockerbie, Scotland, Disemba 1988 na kuuwa watu 270, wengi wao wakiwa Wamarekani. Mtu pekee aliyehukumiwa kutokana na kesi hii, raia wa Libya, Abdil-Basit al-Megrahi, aliachiliwa miaka miwili iliyopita kwa sababu za kibinaadamu.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji