1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ammwagia sifa Modi ziarani India

Angela Mdungu
24 Februari 2020

Rais wa Marekani Donald Trump na waziri mkuu wa India Narendra Modi wameoneshana ukarimu  kwa kumwagiana sifa hii leo mbele ya umati wa raia wa India, wakihakikishiana kuendeleza uhusiano mzuri kati ya mataifa hayo.

https://p.dw.com/p/3YKte
Indien | Donald Trump auf Staatsbesuch in Indien
Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Ni baada ya Rais Donald Trump kuwasili nchini humo na kuhutubia katika uwanja wa mchezo wa kriketi uliohudhuriwa na maelfu ya watu mjini Ahmedabad.

Trump amemwaga sifa kwa uongozi wa modi akisema wa mara ya kwanza katika historia, kila kijiji cha India kina umeme na raia wengi zaidi wa India sasa wameunganishwa na huduma ya intaneti. Ameongeza kuwa kasi ya ujenzi wa barabara kuu nchini humo imeongezeka mara mbili kuelekea kaya milioni 70 zaidi.

 Trump alitoa hotuba hiyo mbele ya takribani raia 100,000 waliokuwa wakimshangilia katika uwanja wa mchezo wa kriketi wa mji anakotokea waziri mkuu Narendra Modi. Trump amehutubia mbele ya umati mkubwa zaidi katika mkutano wa kisiasa kuwahi kushuhudiwa na waziri mkuu huyo katika maisha yake ya siasa. 

Indien | Donald Trump auf Staatsbesuch in Indien
Rais Donald Trump akihutubia maelfu ya watu mjini Ahmedabad, IndiaPicha: Reuters/A. Drago

 Ni katika ziara ya saa 36 za ziara ya Trump nchini India ambapo alianza hotuba yake kwa kutangaza kuwa Marekani inaipenda na kuiheshimu India na kuwa nchi yake itaendelea kuwa rafiki mwaminifu kwa watu wa India.

Mvutano wa kibiashara kati ya India na Marekani kujadiliwa?

Rais huyo wa Marekani anaizuru India wakati kukiwa na mvutano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili, India ikiwa nchi ya tano kwa uchumi mkubwa duniani. Mvutano huo uliibuka baada ya utawala Trump kuongeza ushuru kwa bidhaa za chuma na aluminium kutoka India.  Katika ziara yake ya Inchini humo Trump ameahidi makubaliano mazuri ya biashara na kuipatia nchi hiyo silaha bora zaidi za kijeshi duniani. Anatarajiwa kuhitimisha ziara yake kesho Jumanne katika mji mkuu New Delhi atakapozungumza na waziri mkuu Modi.

Huku ziara hiyo ikiendelea, polisi nchini India wametumia mabomu ya gesi kutawanya kundi la maelfu ya waandamanaji wanaopinga sheria tata ya uraia na wale wanaoiunga mkono walipokabiliana katika mji mkuu New Delhi mapema leo. Mji huo umekuwa kituo cha maandamano dhidi ya sheria hiyo tata kwa takribani miezi miwili sasa.