Iran haiwashikilii majasusi wanaoifanyia kazi Marekani
22 Julai 2019Mkuu wa huduma za ujasusi wa Iran alisema mapema siku ya Jumatatu (Julai 2) kuwa taifa hilo limegundua mtandao wa majasusi wa Marekani na kuwashikilia wafanyakazi 17 wa shirika la CIA, wote wakiwa raia wa Iran. Baadhi ya wafanyakazi hao huenda wakakabiliwa na hukumu ya kifo.
Tangazo la Iran limekuja wakati kukiwa na mvutano kati ya mataifa hayo mawili, huku Marekani ikitumia nguvu kwa kuiwekea Iran vikwazo, baada ya kujitoa katika mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.
Marekani pia imeongeza wanajeshi wake katika eneo la Ghuba na kuishutumu Iran mara kwa mara kwa uchokozi wa kijeshi.
Afisa mmoja wa Iran alisema CIA iliamua kufanya kazi na raia wa Irankwa kuwa wanaielewa lugha zaidi na wanaweza kufikia mashirika kadhaa kwa urahisi.
Aliongeza kuwa wafanyakazi hao walikuwa wanatumia nyaraka takabadhi feki ili kukwepa kufikiwa na maafisa wa usalama wa Iran.
Afisa huyo aliongeza kuwa wafanyakazi hao walikuwa wameahidiwa kupata visa za Marekani, kadi za kijani, na uraia wa Marekani pamoja na kazi nchini humo, lakini ahadi hizo hazikutekelezwa.
Bado haijabainika ni wafanyakazi wangapi watakaokabiliwa na adhabu ya kifo
Mpaka sasa haijawa wazi ni wafanyakazi wangapi watakaokabiliwa na adhabu ya kifo na ni wangapi wanaohudumu ndani ya serikali ya Iran. "Mengi zaidi juu ya suala hili tutayazungumza baadaye," alisema afisa huyo wakati wa mkutano na waandishi habari.
Mataifa kadhaa ya Ulaya na yale ya Asia pia yanaaminika kushirikiana na shirika la ujasusi la CIA katika operesheni zao na Iran. Mshirika wa Marekani, Uingereza, pia anahusika katika mgogoro unaohusisha meli za mafuta zinazoshikiliwa na mataifa hayo mawili.
Siku ya Ijumaa wiki iliyopita Iran iliizuwiya meli ya mafuta ya Uingereza, Stena Impero, ikisema meli hiyo iliendelea na safari yake bila ya kusimama baada ya kugangana na boti ndogo ya uvuvi.
Majibizano kati ya Uingereza na Iran yalianza mwezi huu wakati meli ya mafuta ya Iran, Grace 1, ilipokamatwa katika eneo la Uingereza la Gibraltar kwa tuhuma za kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria.
Chanzo: dpa