1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump, Harris wapambana kwenye mdahalo

11 Septemba 2024

Wagombea wa urais wa Marekani, Kamala Harris wa chama cha Democratic na Donald Trump wa Republican wamepambana kwenye mdahalo wa televisheni usiku wa kuamkia leo kiasi miezi miwili kabla ya uchaguzi wa Novemba 5.

https://p.dw.com/p/4kULC
Marekani, Philadelphia | Mdahalo wa Trump-Harris
Wagombea wa urais wa Marekani, Kamala Harris wa chama cha Democratic (Kulia) na Donald Trump wa Republican wakati wa mdahalo.Picha: Win McNamee/Getty Images

Mdahalo huo wa kwanza baina yao umefanyika huko Philadelphia na kuyaweka mezani masuala muhimu ya uchaguzi wa Novemba ikiwemo uchumi, usalama wa mipaka na uhamiaji, sheria za utoaji mimba, mzozo wa mashariki ya kati, vita vya Ukraine pamoja na masuala mengine ya kimataifa.

Suala la kwanza kabisa ilikuwa uchumi ambapo Harris alizungumzia historia ya maisha yake ya kukulia ndani ya familia ya kipato cha kati akiwaahidi wapigakura kwamba mpango wake wa uchumi utasaidia familia za aina hiyo. Amesema atazisaidia biashara ndogo na za kati pamoja na kupunguza kodi kwa familia za kipato cha wastani.

Hoja hizo zilipingwa mara moja na Trump aliyeutalumu utawala wa rais Joe Biden na Harris -- ambaye amekuwa makamu wake -- kwa kuuharibu uchumi. Trump amesema kiwango cha mfumuko wa bei kwa sasa nchini Marekani kinatisha na kujitapa kwamba alipokuwa madarakani kati ya mwaka 2017 hadi 2021 aliimarisha uchumi wa taifa hilo.

Harris alijibu akisema mpango wa Trump tangu mwanzo hadi sasa ni kuwanufaisha wafanyabiashara wakubwa na ikiwa atashinda itakuwa ni "janga kwa watu wa kipato cha kati na masikini".

Utoaji mimba wasalia moja ya masuala yanayowagawa Wamarekani 

Moja ya mandamano ya kutaka utoaji mimba uwe haki ya kikatiba.
Utoaji mimba wasalia moja ya masuala yanayowagawa Wamarekani.Picha: FREDERIC J. BROWN/AFP

Suala tete la utoaji mimba pia lilijadiliwa wakati wa mdahalo. Kamala Harris ambaye amefanya suala la huduma za afya hasa haki za wanawake kutoa mimba kuwa ajenda muhimu za kampeni yake, alimkosoa Trump kwa msimamo wake kuhusu uavyaji mimba.

"Mtu hahitaji kuiweka kando imani yake kukubali kwamba serikali na Donald Trump hawapaswi kumwambia mwanamke nini anaweza kufanya na mwili wake," alisema Harris.

Kwenye majibu yake Trump amewatuhumu wanachama wa Democratic kwa na "misimamo laini mno ya kiliberali" akaidai baadhi yao wanaunga mkono utoaji mimba hata wakati wa kujifungua.

Trump amejinasibu kuwa na uwezo wa kumaliza vita vya Ukraine na kukomesha wimbi la wahamiaji.

Hoja hiyo ilifafanuliwa mara moja na mmoja ya waongozaji mdahalo aliyesema hakuna jimbo nchini Marekani linaloruhusu kuua mtoto akishazaliwa.

Mizozo ya Ukraine na ule wa Mashariki ya Kati yajadiliwa kwenye mdahalo 

Ama kuhusu suala la mzozo wa Urusi na Ukraine ambao unaendelea kwa zaidi ya miaka miwili, Trump amesema ataumaliza ndani siku chache tu ikiwa atachaguliwa. "Kama ningekuwa rais, mzozo huo usingetokea, Urusi isingethubutu kamwe, ninamfahamu (Rais wa Urusi Vladimir) Putin vizuri. Aingethubutu," alisema Trump.

Harris kwa upande wake amesema washirika wa Marekani ndani ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO wanashukuru kwamba Trump siye rais wa Marekani kwa sababu "vinginevyo, Putin angekuwa ameketi mjini Kyiv na macho yake yakitizama sehemu nyingine za Ulaya, (tena) kwa kuanza na Poland."

Amemkabili Trump akimwita mwanasiasa mwongo, anayependa ukaribu na viongozi "madikteta"

Hali ya Ukanda wa Gaza
Hali ya Ukanda wa Gaza.Picha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Kwenye mzozo wa mashariki ya kati, Trump amesema kundi la Hamas lisingemudu kuishambulia Israel iwapo angekuwa rais kwa sababu alipokuwa madarakani alifanikiwa kuifilisi Iran ambayo inatajwa kuwa mfadhili mkubwa wa makundi ya wanamgambo ikiwemo Hamas na Hezbollah la Lebanon.

Harris amesema ikiwa atashinda atashinikiza kupatikana mkataba wa kusitisha vita, na kwamba sera yake ni kuundwa mataifa mawili ya Israel na Palestina yatakayofanya mambo yake kwa amani. Wote wawili wameonesha msimamo wa kuendelea kuisaidia Israel ili kujilinda.

Vibweka na hamaki vyajitokeza mpambano wa Harris na Trump

Mdahalo wa usiku wa kuamkia leo ulishuhudia pia vibweka na matamshi ya kuwaacha mdomo wazi wapiga kura.

Mdahalo wa Trump-Harris
Donald Trump.Picha: Win McNamee/Getty Images

Wakati mmoja Trump alisikika akisema wahamiaji wanaoingia kupitia mpaka wa kusini wa Marekani wamefurika kiasi wameanza kuiba mbwa na paka kwenye maeneo wanayofikia na kuwafanya kitoweo.

Kulikuwa vile vile na kutupiana vijembe na kudoboana. Harris alifanikiwa mara kadhaa kumfanya Trump ahamaki ikiwa ni pamoja na pale aliposema wafuasi wa rais huyo wa zamani huondoka mapema kwenye mikutano yake ya kampeni kwa uchovu na kutoridhika na hotuba zake.

Hoja hiyo inaonesha ilimwingia rohoni Trump aliyeonesha dhahiri amekasirika na alimjibu Harris kuwa rikodi ya mikutano yake ni ya kihistoria kuliko ya mgombea huyo wa Democratic.