1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubelgiji na Uholanzi zapiga marufuku ndege kutoka Uingereza

John Juma Mhariri: Sudi Mnette
20 Desemba 2020

Uholanzi na Ubelgiji zimepiga marufuku ndege kutoka Uingereza huku Ujerumani pia ikitafakari kuchukua hatua kama hiyo kufuatia kugunduliwa kwa aina mpya ya kirusi cha corona kinachoenea kwa kasi zaidi.

https://p.dw.com/p/3myVg
Großbritannien Royal British Air Force RAAF
Picha: picture-alliance/dpa

Ujerumani inatafakari kupiga marufuku ndege za abiria kutoka Uingereza na Afrika Kusini ili kuzia kuenea kwa aina mpya ya virusi vya corona ambavyo vinaenea kwa kasi sana na ambavyo vimethibitishwa katika mataifa hayo mawili. Duru kuhusu Wizara ya Afya ya Ujerumani imeliambia shirika la habari la AFP.

Hatua hiyo itafuata mfano wa Uholanzi, ambayo imepiga marufuku ndege zote za abiria kutoka Uingereza kuanzia Jumapili.

Kulingana na duru hiyo, serikali ya Ujerumani inatafakari marufuku hiyo kama njia muhimu ya mbadala kuepusha maambukizi zaidi.

Msemaji wa wizara ya afya Ujerumani, amesema serikali inafuatilia kwa karibu hali ilivyo Uingereza na inafanya kazi katika shinikizo kubwa kutathmini tarifa mpya pamoja na data kuhusu aina hiyo mpya ya kirusi.

Kirusi kinachoenea kwa kasi kimegunduliwa baadhi ya maeneo ya Uingereza

Msemaji huyo pia ameongeza kwamba Ujerumani inawasiliana na washirika wengine wa Ulaya kuhusu hilo.

Ubelgiji tayari imetangaza marufuku kwa ndege zote pamoja na treni zote kutoka Uingereza.

Soma pia: Ulaya yaimarisha vizuizi kukabiliana na corona

Marufuku ya Uholanzi kwa ndege kutoka Uingereza alianza kutekelezwa saa kumi na mbili asubuhi ya Jumapili majira ya nchi hiyo na itatekelezwa hadi Januari 1.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Toby Melville/Pool/AP/picture alliance

Mnamo Jumamosi, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alisema kuwa mamilioni ya Waingereza watalazimika kufuta mipango yao ya Krismasi na wasalie majumbani kwa sababu ya kirusi hicho kipya kinachosambaa kwa kasi zaidi.

Soma pia: Mataifa yapambana kudhibiti COVID-19

Uholanzi ilichukua hatua hiyo saa kadhaa baada ya Uingereza kuwataka watu kukaa majumbani katika sehemu kadhaa za nchi hiyo ili kupunguza kuenea kwa aina hiyo ya kirusi, ambacho waziri wa afya nchini humo Matt Hancock alisema ‘kiko nje ya uwezo wa kudhibitiwa''.

Hancock: Ni vigumu kudhibiti aina hiyo mpya ya kirusi

Kirusi hicho Akizungumza na kituo cha televisheni cha Sky News, Hancock alisema hali ni "sugu sana'' na itakuwa vigumu sana kukidhibiti hadi mpango wa chanjo utakapoanza kikamilifu.

Inaonekana kuwa wanasayansi waligundua kirusi hicho kipya kwenye mgonjwa mnamo mwezi Septemba. Susan Hopkins ambaye ni mhudumu wa afya ya umma alikiambia kituo cha Sky News kwamba shirika la afya liliiambia serikali kuhusu hayo siku ya Ijumaa wakati uchunguzi zaidi ulibaini hatari iliyoko.

Alithibitisha takwimu iliyotolewa na Johnson kwamba kirusi hicho kina uwezo wa kuambukiza watu kwa asilimia 70 zaidi.

Wajerumani wengi wakubaliana na vikwazo vya corona

Hata hivyo, nchini Ujerumani aina hiyo mpya ya virusi haijagunduliwa hadi sas. Hayo ni kulingana na mtaalamu mkuu wa maambukizi ya virusi katika hospital ya Charite mjini Berlin Christian Drosten aliyeandika hayo kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Maambukizi na maafa zaidi yarekodiwa Ulaya

Wiki iliyopita, Ulaya ilikuwa bara la kwanza duniani ambalo idadi yake ya vifo kutokana na Covid-1i ilipindukia watu 500,000 tangu janga hilo lianze Disemba mwaka uliopita.

Jumla ya watu milioni 1.6 duniani wamefariki kutokana na janga hilo na zaidi ya watu milioni 76.

Janga hilo pia limeathiri pakubwa uchumi ulimwenguni na kuvuruga maisha ya wengi.

Nchi kadhaa zimeweka masharti ya kupunguza kusambaa kwa virusi hivyo ikiwemo shule na maduka ambayo huuza bidhaa ambazo si za lazima katika matumizi ya kila siku.

(AFPE)