1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olaf Scholz ashindwa kura ya imani bungeni

16 Desemba 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amemuomba rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier kulivunja bunge baada ya kushindwa katika kura ya imani aliyoiitisha bungeni kuona iwapo wabunge bado wana imani na serikali yake.

https://p.dw.com/p/4oDQP
Deutschland Berlin 2024 | Kanzler Scholz nach Vertrauensabstimmung vor Schloss Bellevue
Picha: Annegret Hilse/REUTERS

Kansela Scholz alipeleka bungeni mswada huo wa kura ya imani baada ya serikali yake kuanguka mwanzoni mwa mwezi Novemba. Sasa, Rais Steinmeier ana muda wa siku 21 ili kuamua kulivunja bunge na baada ya hapo kutakuwa na siku 60 kabla ya kufanyika uchaguzi wa mapema. Scholz alipendekeza uchaguzi huo ufanyike tarehe 23 Februari 2025.

Wabunge 207 pekee wa chama chake cha SPD ndio waliompigia kura katika bunge la taifa lililo na wanachama 733, huku wabunge 394 wakipiga kura ya kutokuwa na imani nae na wengine 116 wakijizuwia kupiga kura. Scholz alihitaji kura 367 ili kushinda kura hiyo.

Scholz aliomba bunge kuitisha kura ya imani

Awali alipokuwa anahutubia bungeni kabla ya wabunge kushiriki mchakato huo wa upigaji kura, Scholz alielezea mipango yake ya matumizi katika masuala ya usalama, biashara na ustawi wa jamii na baade mpinzani wake  Friedrich Merz, wa kambi ya upinzani ya wahafidhina ya CDU/CSU alikuwa na masuali magumu kwa Scholz, akitaka kujua kwanini mipango hiyo hakuyaeleza mapema katika uongozi wake, akisema kansela huyo hapaswi kupigiwa kura ya kuwa na imani nae. Hata hivyo Scholz aliendelea kuitetea serikali yake akisema imepiga hatua ndani ya miaka mitatu iliyopita ikiwemo kuongeza bajeti ya ulinzi.

Mkwamo wa kisiasa Ujerumani ulishuhudiwa pale Kansela Scholz alipomfuta kazi Novemba 6, Christian Lindner, kama Waziri wa fedha, kufuatia miezi kadhaa ya mvutano juu ya bajeti ya mwaka 2025. Hatua hiyo ilikifanya chama cha Lindner cha Free Democrats, FDP kujitoa katika serikali ya muungano na kumuacha Scholz na serikali ya wachache ya vyama viwili vya Social Democrats, SPD, na kile cha Kijani.

Kura ya maoni: SPD kuwa nyuma ya kambi ya upinzani ya wahafidhina CDU/CSU

Olaf Scholz - SPD
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz wa chama cha Social Democrats SPDPicha: Matthias Gränzdörfer/pictureteam/IMAGO

Joto hili la kisiasa Ujerumani linafukuta wakati taifa hilo kubwa kiuchumi barani Ulaya, likijizatiti kufufua sekta yake ya viwanda wakati ambapo bei ya nishati ipo juu sana na pia ushindani mkali kutoka China. Ujerumani inakabiliwa na changamoto kubwa ya siasa za kilimwengu kama vita vya Urusi nchini Ukraine na kurejea kwa Donald Trump kama rais wa Marekani kunakotoa wasiwasi juu ya ushirikiano wa taifa hilo kubwa na Jumuiya ya kujihami NATO pamoja na masuala ya kibiashara.

Kulingana na kura ya maoni iliyofanyika mwezi huu wa Desemba, iliyotoa muelekeo wa uchaguzi, chama cha Scholz cha SPD kimeonekana kuwa nyuma ya kambi ya upinzani ya wahafidhina ya CDU/CSU. Chama cha siasa kali cha Alternative for Deutschland (AfD) pia kimeonekana kupata umaarufu zaidi na huenda kikaibuka cha pili au cha tatu bungeni. Kiongozi wake Alice Weidel, huenda akashinda nafasi ya Ukansela, lakini vyama vingine vimeendelea kusisitiza kuwa havitajiunga na chama hicho kuunda serikali ya muungano.

Scholz asema hatokuwa naibu kansela iwapo Merz atashinda

Nacho chama cha waliberali cha FDP kimeonekana kuwa nyuma kuvuka kihunzi cha kupata asilimia 5 inayohitajika kuingia bungeni. Chama cha mrengo wa kushoto cha (BSW) kinachoongozwa na Sahra Wagenknecht, kinatarajiwa kuingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2025.

Kura ya imani katika bunge la Ujerumani imewahi kufanyika mara tano katika historia ya nchi hiyo na mara tatu serikali ilishindwa kupata wingi wa kura na kulazimisha uchaguzi wa mapema kama ilivyofanyika mwaka 1972 wakati wa kansela Willy Brandt, Helmut Kohl mwaka 1983, na Gerhard Schröder  mwaka 2005.

afp,reuters,ap