Uchambuzi: Mambo gani yamo kwenye mkakati wa Iran, Israel?
4 Oktoba 2024Kufuatia mashambulizi makubwa ya makombora ya Iran dhidi ya Israel siku ya Jumanne (Oktoba Mosi), kila upande umekuwa ukijipiga kifua na kunadi uwezo wa kumuadhibu hasimu wake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alisema mashambulizi hayo yamehitimisha ulipizaji kisasi wa Iran dhidi ya Israel, "isipokuwa," alionya, "ikiwa Israel itachagua kuendeleza mzunguko wa ulipizaji kisasi."
Kupitia mtandao wa X, waziri huyo alitishia kuwa ikiwa hilo lingetokea, jibu la Iran lingekuwa kali na lenye nguvu zaidi.
Soma zaidi: Mashambulizi ya Israel yaharibu barabara ya Lebanon-Syria
Burcu Ozcelik, mtaalamu wa masuala ya usalama wa Mashariki ya Kati katika taasisi ya United Service yenye makao mjini London, aliambia DW kuwa maelfu ya wapiganaji kutoka mataifa kadhaa ya Kiarabu na Kiislamu, ambao ni washirika wa Iran, wamekaa chonjo wakisubiri tu ishara waingie vitani.
''Kwa muda sasa, kitisho cha wapiganaji kutoka kile kinachoitwa ''Mhimili wa Kujihami'' wanaojikusanya karibu na mpaka kati ya Syria na Lebanon, kimekuwa kikiongezeka. Wanamgambo kutoka Syria, Yemen na Afghanistan wametangaza mshikamano wao na Hizbullah na utayari kupigana upande wake ikiwa watatakiwa kufanya hivyo." Alisema mtaalamu huyo.
Kwa mujibu wa Ozcelik, ikiwa operesheni za Israel ndani ya Lebanon zitaendelea kwa muda mrefu, wapiganaji hao watajipenyeza na kujiunga na mapigano.
"Hiyo ni hali ya hatari sana ambayo Israel na jeshi la Lebanon watajaribu kuiepuka.'' Aliongeza.
Netanyahu amedhamiria kuishambulia tena Iran
Lakini kitisho hicho hakionekani kuifanya Israel ifikirie kuupoza mgogoro unaotokota.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema Iran ilikuwa imefanya kosa kubwa na kwamba ingelipa kwa gharama ya juu.
Marekani, ambayo ni mshirika mkuu wa Israel, pia ilisema kuwa ingelisaidia kuhakikisha kuwa Iran inaumia kutokana na mashambulizi yake ya mwanzoni mwa wiki hii dhidi ya Israel.
Soma zaidi: Ayatullah Ali Khamenei atetea kuishambulia Israel
Hata maoni ya wengi ndani ya Israel ni kwamba hii ni fursa ya nadra kwa jeshi la nchi yao kuusambaratisha kabisa ukanda wa Mashariki ya Kati na kuidhoofisha vibaya Iran.
Simon Wolfgang Fuchs, mhadhiri wa masomo ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Kiebrania cha mjini Jerusalem, alisema kwa wakati huu Israel haiambiliki kuhusu kupunguza mivutano.
Hata hivyo, msomi huyo alionya kuwa ikiwa Israel itaishambulia miundombinu ya mafuta ya Iran kama inavyotarajiwa, basi matokeo yake hayawezi kutabirika.
''Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran limeitishia bayana Marekani, likisema ikiwa mitambo ya kusafisha mafuta ya Iran itashambuliwa, nalo pia litavishambulia mitambo ya kusafisha mafuta ya Marekani katika ukanda mzima, ikiwemo ya nchini Saudi Arabia, Azerbaijan, Kuwait, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu.'' Aliongeza.
Duru kutoka tovuti ya Axios ya nchini Marekani zinaeleza kuwa mashambulizi makubwa ya Israel dhidi ya Iran yatatokea katika siku chache zijazo, zikiwanukuu maafisa wa Israel waliosema kuwa shabaha yao itakuwa miundombinu ya mafuta na maeneo mengine ya kimkakati.
Uchambuzi huu umetafsiriwa kutoka makala ya Jennifer Holleis wa DW.