Ziara ya Kansela: Ujerumani yatoa ishara kwa Japan
27 Aprili 2022Kansela wa Ujerumani Olaf anaanza ziara ya siku mbili nchini Japan hii leo, likiwa taifa la kwanza la Asia kutembelewa na kiongozi huyo tangu alipoingia madarakani, ikiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano na taifa hilo ambalo ni mshirika wa kimaslahi wa Ujerumani. Hii itakuwa ziara ya tatu ya Scholz katika taifa lisilo mwanachama wa Umoja wa Ulaya baada ya Marekani na Israel.
Katika ziara hiyo inayofanyika Alhamisi na Ijumaa, kansela Scholz anataka kutilia mkazo umuhimu unaozidi kukua wa Japan kwa Ujerumani, ujumbe ukiwa hasa kwamba Ujerumani haijapoteza dira kuelekea bara la Asia kulinga na duru za kidiplomasia.
Lakini ziara hiyo ya Scholz mashariki ya mbali ina sababu nyingine rasmi; kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi wakuu wa kundi la mataifa saba yaliostawi zaidi kiuchumi G7, mwenyeji kawaida huzuru washiriki wengine.
Maadili ya pamoja
Katika ziara hiyo ya kikazi mjini Tokyo itakayodumu kwa takribani masaa 20, Scholz atakutana na waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida, kujadilia yanayojumlisha vikwazo dhidi ya Urusi, utegemezi juu ya gesi ya Urusi, usalama wa mnyororo wa ugavi wa vifaa vya teknolojia na malighafi, pamoja na siasa za kieneo.
Kansela Scholz ambaye anambatana na ujumbe wa wafanyabiashara, pia atazungumza kwenye mkutano wa chemba ya biashara na viwanda ya Ujerumani.
Kabla ya kurejea Ujerumani, ataoneshwa mradi wa mfano wa mnyororo wa ugavi wa gesi ya hydrogen mjini Kawasaki. Japan inazingatiwa kuwa mwanzilishi wa matumizi ya gesi ya hydrogen kama mafuta duniani.
Kukaribiana zaidi kwa Ujerumani na Japan kunahusiana na uhasama unaoongezeka kati ya mataifa ya kidemokrasia na tawala za kiimla. Katika mzozo wa kibiashara kati ya China na Marekani, mataifa hayo mawili yanatafuta njia za kati za kulinda maslahi yao pasina kujitenga na mshirika wao wa kiusalama, Marekani.
Kansela wa muda mrefu Angela Merkel kawaida alitoa kipaumbele kwa China katika ziara zake za Asia. Hakukuwa na ziara hata mmoja kwenda Japan wakati wake, kama ilivyo kwa Scholz hivi sasa. Lakini ushirika wa Beijing na Urusi licha ya vita dhidi ya Ukraine umelaazimisha kuimarishwa kwa usuhuba kati ya Ujerumani na Japan.
Soma pia: Maoni: Hatimaye Ujerumani yaja na msimamo dhidi ya Urusi
Mashauriano kwa ngazi ya kiserikali
Mwaka mmoja uliopita, mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi walifanya mazungumzo yaliopewa jina la "2-plus-2" kati ya nchi hizo mbili kwa mara ya kwanza. Kwa sababu ya janga la Covid-19, mkutano huo ulifanyika kwa njia ya video.
Sasa Ujerumani inataka kupandisha mazungumzo na Japan hadi kiwango cha mashauriano ya kiserikali. Mbali na wakuu wa serikali, mawaziri wengi kutoka pande zote mbili pia watakutana. Scholz anaweza tayari kutangaza utaratibu kama huo na Japan mjini Tokyo. Ujerumani huwa na mashauriano kama hayo ya mara kwa mara na Israel, India na China, miongoni mwa mataifa mengine.
Soma pia: Kansela Olaf Scholz ahimiza umoja katika salaam za mwaka mpya
"Umuhimu unaokua wa Japan tayari umeonekana wazi katika miaka miwili iliyopita kwa sababu Japan ndiyo mshirika muhimu zaidi wa thamani na maslahi wa Ujerumani barani Asia," anaelezea Profesa Patrick Köllner, mkurugenzi wa taasisi ya GIGA inayojihusisha na utafiti wa Asia yenye makao yake mjini Hamburg.
"Hata kama nchi hizi mbili hazitumii mbinu sawa za ulinzi wa hali ya hewa, kwa mfano, maeneo ya makutano ni makubwa sana na yanatoa msingi mzuri wa mipango ya ushirika."
Soma pia: Kansela Scholz akutana na Rais Erdogan
Uhusiano huu unajengwa kwenye msingi wa marudishiano, anasema Norihide Miyoshi, mwandishi wa zamani wa Ujerumani wa gazeti kubwa la kila siku la Yomiuri Shimbun.
"Kwa Japani, Ujerumani ni mojawapo ya washirika adimu wanaoaminika duniani," anasema. "Uratibu na ushirikiano na Ujerumani ni muhimu sana kwa Japan kukabiliana na Urusi na China," Miyoshi anaeleza.
Ziara hiyo inatoa fursa nzuri ya kujua mwelekeo na fikra za Scholz. Taswira ya Ujerumani nchini Japan bado inashawishiwa pakubwa na Merkel, ambaye alizingatiwa sana kama mwanasiasa "mwenye uwezo na ushawishi".
Sera ya India na Pasiki
Mnamo 2019, chini ya Merkel, serikali ya shirikisho ilichapisha miongozo ya sera ya India na Pasifiki kwa mara ya kwanza. Tangu wakati huo, Ujerumani imekuwa ikionyesha uwepo zaidi katika eneo hili.
Manowari ya Kijerumani ya "Bayern" ilikamilisha safari ya miezi sita katika eneo hilo kuanzia Agosti 2021 na pia ilitia nanga Yokohama mnamo Novemba. Septemba ijayo, ndege sita za kivita za Ujerumani maarufu Eurofighters zitashiriki katika mazoezi ya kijeshi ya kimataifa yanayojulikana kama "Pitch Black" nchini Australia.
Mkaguzi wa Jeshi la anga Luteni Jenerali Ingo Gerhartz na mwenzake wa Japan Jenerali Shunji Izutsu wamekubaliana kwamba ndege tatu zitasafiri kuelekea Japan kwa ziara fupi.