Ujerumani: Urusi italipa ikichukua hatua kuivamia Ukraine
17 Januari 2022Annalena Baerbock amesema hatua yoyote ya uchokozi kutoka Urusi itakuwa na majibu makali kwa taifa hilo kiuchumi, kimkakati na kisiasa. Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ujerumani aliyeko Kiev kwa ziara rasmi amesema diplomasia ndio njia pekee ya kusuluhisha mgogoro uliopo.
Dmytro Kuleba, waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine, kwa upande wake amesema taifa lake na Ujerumani zimeungana pamoja kushinikiza kuundwa "Mfumo wa Normandy" ambao ni mazungumzo ya pande nne yanayowajumuisha viongozi wakuu wa Ukraine, Ufaransa, Urusi na Ujerumani kwa nia ya kumaliza vita vya Mashariki mwa Ukraine.
soma zaidi: Ukraine yalengwa katika mashambulizi ya mtandao
Mazungumzo kati ya Moscow na mataifa ya Magharibi kuhusu uwepo wa maelfu ya wanajeshi mpakani mwa Ukraine yalimazika wiki iliyopita bila ya mafanikio. Shambulio la mtandaoni dhidi ya Ukraine limezidi kuutanua mgogoro uliopo.
Hata hivyo Ujerumani imekuwa ikitoa msaada kwa Ukraine na kuiunga mkono kidiplomasia katika vita vyake na Urusi tangu Moscow ilipoinyakuwa rasi ya Krimea kutoka Ukraine na kuwaunga mkono watu wanaotaka kujitenga katika eneo la Donbass mwaka 2014.
Petro Poroshenko arejea nyumbani kutoka Poland
Huku hayo yakiarifiwa rais wa zamani wa Ukraine Petro Poroshenko amerejea mjini Kiev kutoka Poland leo jumatatu licha ya hatari ya kukamatwa akiapa kulilinda taifa hilo la zamani la kisovieti dhidi ya uwezekano wa kushambuliwa na Urusi.
Baada ya kuzungumza na wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika karibu na uwanja wa ndege baada ya kuwasili, Poroshenko alifika katika mahakama moja mjini Kiev iliokuwa iamue iwapo akamatwe akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake.
soma zaidi: NATO na Urusi zafanya mazungumzo mjini Brussels
Poroshenko aliyekuwa rais wa Ukraine kuanzia mwaka 2014 hadi 2019 alianza kuchungunzwa kwa madai ya uhaini na kuondoka Ukraine mwezi Desemba huku akikanusha madai hayo. Huenda akafungwa hadi miaka 15 jela iwapo atakutwa na hatia katika kesi hiyo ya uhaini.
Rais huyo wa zamani aliye na miaka 56 ambaye sasa ni mbunge na kiongozi wa upinzani amerejea nchini wakati Ukraine ikipitia mgogoro mbaya wakati Urusi ikiweka wanajeshi wake mpakani mwa taifa hilo na kuzua wasiwasi wa uvamizi. Poroshenko ni mkosoaji mkubwa wa rais wa sasa wa Ukraine Volodymyr Zelensky, anaedai ni msaliti na ameshinda kulilinda taifa hilo.
Chanzo: afp/ap