Ukoloni ulivyochangia ukosefu wa imani kwa dawa za Magharibi
28 Desemba 2023Kwa nini Ujerumani ilitaka kutengeneza madawa kwenye makoloni yake?
Kwenye miaka ya 1870 na 1880, mataifa ya Ulaya yaliwania kupata maeneo kote barani Afrika.
Mabeberu hao walijuwa kwamba ili kuyadhibiti maeneo hayo, walipaswa wenyewe wawepo.
Lakini maradhi, kama vile malaria, yaliwaangamiza Wazungu wengi kwenye makoloni ya Kameruni na Togo kiasi cha kwamba ni wachache sana waliomudu kuishi mbali na mwambao.
Soma: Quane Martin Dibobe: Kutoka maonesho hadi mwanaharakati dhidi ya ukoloni
Lakini Waafrika nao walikuwa pia wameletewa maradhi mapya kwa kukutana na Wazungu hao, kama vile ungojwa wa ndui.
Kwenye kuyatibu maradhi haya, madaktari wa ukoloni wa Kijerumani waliona kuna fursa ya kujaribu matibabu na madawa ambayo hayakuwa yamewahi kujaribiwa.
Wakati huo huo, serikali ya kikoloni ilitaka kupunguza idadi ya wafanyakazi wanaopotea waliohitajika kwenye ujenzi wa makoloni hayo.
Ugonjwa wa ndui Togoland
Chanjo mujarabu kwa ugonjwa wa ndui zilishakuwepo Ulaya kwenye miaka ya 1880. Maambukizo ya ugonjwa huo nchini Togoland yalisababisha vijiji vizima kwenye eneo la Lome kupata maradhi hayo mwanzoni mwa miaka ya 1900.
Madaktari wa kikoloni walikabiliana na maambukizo hayo kwa kuwadunga watu chanjo zilizomaliza muda wake.
Soma zaidi: Togo "Koloni la Mfano"
Hata ilipofahamika wazi kwamba kampeni hiyo ya chanjo haikuwa ikifanikiwa, raia walilazimishwa kuchomwa hata kwa kutumia nguvu.
Mnamo mwaka 1911, madaktari wa kikoloni hatimaye walisimamisha, wakachunguza na kubadilisha njia za utoaji chanjo.
Kufikia mwaka 1914, kitosho cha ugonjwa wa ndui kilikuwa kimepunguwa kwa kiasi kikubwa, lakini tayari madhara yalishapatikana.
Robert Koch alikuwa na dhima gani kwenye matibabu ya kikoloni?
Dk. Robert Koch alikuwa mwanasayansi aliyeshinda Tuzo ya Nobel, na ambaye alifanikisha ugunduzi muhimu kwenye kupambana na maradhi kama vile kifua kikuu, kipindupindu na kimeta.
Wengi wanamuita baba ya maikrobaiolojia. Kwenye karne iliyofuatia, maendeleo ya tiba yaliyojikita kwenye utafiti wake yaliokowa maisha ya mamilioni ya watu ulimwenguni. Lakini kuna upande mbaya zaidi kwenye mchango wa Koch.
Soma zaidi: DW yazindua makala mpya za "Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani"
Mwaka 1906, homa ya ndorobo ilisambaa kwenye eneo la Maziwa Makuu, Afrika ya Mashariki. Uliwaathiri wanyama na wanaadamu, wenyeji na maafisa wa kikoloni.
Ulisambazwa na nzi wa ndorobo, na hakukuwa na mtu aliyejuwa namna ya kuuzuwia. Ugonjwa huo uliuwa zaidi ya watu 250,000 mwanzoni mwa karne hii na kuziathiri familia nyingi kwenye eneo hilo.
Licha ya kuwa mataifa ya kikoloni yenye ushindani, Ujerumani na Uingereza zilihofia ukosefu wa wafanyakazi ungetishia miradi yao mikubwa ya ujenzi wa miundombinu.
Koch alipelekwa Afrika Mashariki kufanya kila awezalo kupata tiba.
Kwa nini matendo ya Koch yalikuwa na utata?
Alikuwa amepewa vidonge vya kila aina na kampuni mbalimbali za madawa, ambavyo hadi hapo vilikuwa vimefanyiwa majaribio kwa wanyama katika maabara za Ulaya - ikiwa hata majaribio hayo yalifanyika.
Koch akaweka kambi yake kwenye Visiwa vya Sese katika Ziwa Viktoria. Wagonjwa wengi walikuwa wameripotiwa hapo, lakini Koch alitaka wagonjwa zaidi waliouguwa homa ya ndorobo. Na aliwapata kwa kiwango kikubwa, lakini inashukiwa kuwa wengi wao waliletwa hapo kwa nguvu.
Soma zaidi: Uporaji wa ardhi: Kuzaliwa kwa Himaya ya Ukoloni wa Ujerumani
Hali kwenye kambi hiyo ilikuwa mbaya, na Koch alianza kuwachoma wagonjwa hao sindano aina ya Atoxyl. Iliposhindwa kufanya kazi, aliongeza dozi. Matokeo yake, wagonjwa walipata maumivu makali, upofu - na mmoja katika kila kumi alipoteza maisha.
Hata baada ya kurejea Ujerumani mwaka 1907, Robert Koch aliendelea kupendekeza matumizi ya Atoxyl kwenye matibabu ya homa ya ndorobo. Serikali za kikoloni pia zilifanya hivyo na kuweka makambi Afrika Mashariki, Kameruni na Togo.
Makambi kama maeneo ya majaribio ya tiba
Robert Koch alipendekeza matumizi ya kambi zilizotengwa, mfano wa zile zilizotumiwa na Jeshi la Uingereza nchini Afrika Kusini wakati wa Vita Waingereza na Mabowa, kukabiliana na maradhi na kuwatenganisha wagonjwa na familia zao - na endapo hakuna matibabu, waache wagonjwa huko hadi mauti yawachukuwe. Koch alitetea mtazamo kama huo kwenye ujenzi wa makambi Afrika Mashariki ili kujaribu madawa mapya kwa wagonjwa.
Majaribio kama haya ya binaadamu yalikuwa hayaruhusiwi barani Ulaya, lakini sera ya kikoloni ilikuwa inawachukulia Waafrika kama watu wanaoweza kutumika tu.
Je, tiba ya homa ya ndorobo iliwahi kupatikana?
Ndiyo! Mnamo mwaka 1906, kidonge kilichoitwa Bayer 205 ama Germanin kilipatikana. Mwaka 1921, msaidizi wa zamani wa Koch, Friedrich Karl Kleine alifanya majaribio ya dawa hiyo kwa wenyeji wa Rodeshia Kaskazini, sasa Zambia. Dawa hiyo mpya ilikuwa na hadi sasa inatibu kwa asilimia 100. Sio Atoxyl iliyotumika.
Majaribio ya Koch kwenye visiwa vya Sese hayakuwa jambo geni kwenye zama za ukoloni. Ustawi wa wagonjwa haukuwa kipaumbele - bali ufanisi wa dawa fulani ndio uliozingatiwa. Na Waafrika walionekana kama watu wanaoweza kutumiliwa kwa majaribio.
Soma zaidi: Pambana! Jinsi Waafrika Mashariki walivyokabiliana na ukandamizaji wa kikoloni
Dawa zilizotengenezwa na mataifa ya kikoloni yameokowa maisha yasiyo idadi barani Afrika. Lakini utengenezaji wake ulifanyika wakati wa ukosefu mkubwa wa usawa, ambapo udhalilishaji dhidi ya Waafrika ulikuwa kila mahala.
Kumbukumbu hizi mbaya za kuwatumilia wanaadamu kwa majaribio zimetanda kiwingu kizito kwenye imani kwa dawa za mataifa ya Magharibi na bado hazijawahi kutambuliwa kikamilifu.
Mfululizo wa makala hizi za za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa masuala ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.