Ukraine yatuma msafara wa mabasi kuondoa watu Mariupol
31 Machi 2022Naibu waziri mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk, amesema katika ujumbe wa vidio kuwa mabasi 45 yatatumwa mjini Mariupol Alhamis, na kuongeza kuwa wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa mabasi hayo yanafika na kuwachukuwa watu ambao bado hawajaweza kuondoka huko.
Soma pia: Ukraine: Urusi inaendeleza mashambulizi baada ya kuahidi kusitisha mapigano
"Usiku huu tumepokea ujumbe kutoka kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu kwamba Shirikisho la Urusi linathibitisha kuwa tayari kufungua njia kwa msafara wa kimataifa kwenda mjini Mariupol, alisema Vereshchuk.
"Tumetuma mabasi 45 kwenye njia ya kwenda Mariupol. Tutafanya kila kitu kuhakikisha mabasi hayo yanafika Mariupol na kuwaondoa watu ambao hawakuweza kutoka huko mpaka sasa."
oma pia: Athari za vita kwa watoto wanaolindwa na serikali Ukraine
Msafara huo wa mabasi unakusudiwa kubeba watu kutoka Mariupol kuwapeleka Zaporizhzihia, umbali wa karibu kilomita 300, kupitia mji unaodhibitiwa na Urusi wa Berdyansk. Juhudi kadhaa za nyuma kuwaondoa raia zimeshindwa kutokana na kushindwa kuweka njia salaama za kutokea, katikati mwa mapigano.
Mji wa Mariupol, ulio kwenye bahari ya Azov, umezingiriwa na vikosi vya Urusi tangu mwanzoni mwa mwezi Machi.
Kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine, zaidi ya watu 100,000 bado wamo katika mji huo ulioharibiwa vibaya, wanakokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, dawa, joto la kupasha majumba na umeme.
Kabla ya vita, mji huo ulikuwa na wakaazi takribani laki nne.
Zelenskiy aomba msaada zaidi kutoka mataifa ya Magharibi
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, ameendelea na utaratibu wake wa kuzungumza na miji mikuu ya mataifa kupitia mfumo wa vido.
Soma pia: Wakimbizi wa Ukraine wapindukia milioni 4
Katika hotuba kwa bunge la Australia siku ya Alamisi, Zelenskiy ametoa wito kwa serikali mjini Canberra kuweka vikwazo vikali dhidi ya Urusi na kusimamisha biashara zote za taifa hilo nchini humo.
Amewashukuru wabunge wa Australia kwa msaada wao, lakini amewasihi kutuma zana zaidi za kijeshi, hasa magari ya kijeshi yaliotengenezwa nchini humo yanayojulikana kama Bushmaster, ambayo yanaweza kuisadia pakubwa Ukraine katika mapambano yake dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Zelenkiy ametoa maombi sawa na hayo kwa bunge la Uholanzi pia, ambako ameomba msaada wa silaha, ujenzi mpya na kusitisha kwa biashara zote za Urusi, na kuongeza kuwa vikwazo vikali vinahitajika ili Urusi isipate fursa ya kuendeleza vita vyake barani Ulaya.
Soma pia: Urusi na China zajadili mzozo wa Ukraine
Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison amemuambia Zelenskiy kuwa nchi yake inasimama na watu wa Ukrainena siyo kile alichokiita mahalifu wa kivitawa Moscow.
"Namjua mwanaume huyo, unamjua pia, tunamjua sote. Tunaujua utawala wake, tunawaona wanavyotenda unyama usioelezeka dhidi ya watoto wenu, hospitali zenu na makaazi. Na tunakumbuka udunguaji wa ndege ya raia iliyobeba watu 298 wakiwemo wa Australia 38," alisema Morrison akimkaribisha Zelenskiy kuhutubia bunge.
Uturuki kuwakutanisha tena Lavrov na Kuleba
Huku hayo yakijiri, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, amesema Ankara inafanya juhudi kuwakutanisha tena mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Ukraine kwa mazungumzo.
Cavusoglu amesema katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni kwamba mkutano huo unaweza kufanyika ndani ya wiki mbili.
Wakati Urusi iliahidi kupunguza mashambulizi katika mazungumzo ya wiki hii mjini Istanbul, Idara ya upepelezi wa kijeshi ya Uingereza imesema inatarajia mapigano makali katika viunga vya mji mkuu wa Ukraine Kyiv katika siku chache zijazo.
Chanzo: Mashirika