Ulemavu nchini Syria: Mgogoro 'uliofichwa'
31 Julai 2023Familia ya Abd al-Hadi Miteb al-Hassan ni miongoni mwa watu waliokuwa wahanga wa mabomu ya vishada yaliyorushwa na Urusi mara mbili nchini Syria na mara zote mbili mashambulio hayo yalikuwa na athari za kutisha.
Mara ya kwanza, al-Hassan aliiambia DW, kwamba baba yake aliuawa wakati wa shambulio la ndege kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani inayodhibitiwa na wapinzani kwenye mji wa Idlib.
Familia hiyo inatokea sehemu za mashambani karibu na mji wa kati wa Syria wa Hama lakini ilihamia kwenye eneo la wapinzani la kaskazini mashariki wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Soma pia:Bomu la ardhini lauwa tisa Syria
Mara ya pili, dada wawili wadogo wa al-Hassan walikuwa wakicheza nje kidogo ya kambi wakati mabaki ya bomu la yalipolipuka. Dada yake mmoja alipoteza jicho na mwengine alipoteza mkono katika shambulio.
Al - Hassan amesema wasichana hao sasa wanajaribu kuishi maisha ya kawaida lakini hali ni ngumu kwao na kwa familia yao kwa jumla.
Ni Wasyria wangapi walio na ulemavu?
Kulingana na idadi iliyobainishwa na Umoja wa Mataifa, mnamo mwaka wa 2021 baada ya muongo mmoja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe karibu asilimia 28 ya watu wa Syria, wenye umri wa zaidi ya miaka 2, sasa wana ulemavu wa aina fulani.
Idadi hiyo ni kubwa zaidi katika sehemu za kaskazini mwa Syria eneo linalodhibitiwa na wapinzani ambako dada zake al-Hassan wanaishi. Ni eneo linalotegemea sana misaada lakini lina upungufu wa vifaa vya matibabu.
Umoja wa Mataifa umesema karibu asilimia 37 ya wakazi kaskazini mashariki mwa Syria wanakabiliwa na aina fulani ya ulemavu. Kiwango hicho ni zaidi ya mara mbili ya wastani wa dunia, ambayo ni karibu asilimia 15.
Soma pia: Miaka 10 ya mauaji, mateso na wakimbizi Syria
Mtafiti mwandamizi wa haki za walemavu wa shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch, Emina Cerimovic, amesema idadi hiyo ni ya juu sio tu kwa sababu ya vita.
Mtafiti huyo aliyeshiriki katika kutayarisha ripoti ya mwaka wa 2022 amesema ulemavu pia ni kutokana na ukosefu wa huduma za afya.
Hali hiyo imesababisha watoto na watu wazima kadhalika, kupata ulemavu ambao vinginevyo wasingekuwa nao.
Mashirika ya misaada yameiambia DW yanaamini kwamba idadi halisi ya walemavu ni kubwa zaidi kuliko utafiti wa Umoja wa Mataifa wa 2021 unavyoonesha.
Idadi pia imeongezeka baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililoikumba Uturuki na pia sehemu ya kaskazini mwa Syria mnamo mwezi wa Februari mwaka huu.
Japo ni vigumu kutoa idadi kamili, ya watu wenye ulemavu kaskazini mwa Syria, inaaminika kwamba idadi ni kubwa sasa kuliko ya hapo mwanzoni. Migogoro ya kivita inasababisha aina mpya za ulemavu na inaathiri jamii nzima kwa jumla.
Mtafiti mwandamizi wa haki za walemavu Emina Cerimovic amesema tatizo la walemavu halikupewa uzito unaostahili nchini Syria licha ya idadi ya watu hao kuwa kubwa nchini humo ameeleza kuwa vita vya ndani ya Syria vimeendelea kwa muda mrefu pia juu ya masuala ya kisiasa yaliyosababishwa na utawala wa kidikteta wa Bashar Assad.
Watafiti wa Uingereza wamesema mbali na madhara ya kimwili walemavu wanakabiliwa na unyanyapaa wa kisaikolojia na kujiona kuwa hawana manufaa kwa jamii.
Mwanaharakati al-Jabir amesema pana haja ya kuchukua hatua zaidi ili kutetea haki za walemavu na jambo muhimu zaidi amesema ni kubalidilisha mitazamo juu ya watu hao.