Umoja wa Ulaya waipatia Ukraine mkopo wa mabilioni
20 Septemba 2024Tangazo hilo limetolewa wakati wa ziara ya kiongozi huyo wa Umoja wa Ulaya mjini Kyiv.
Bibi Von der Leyen ambaye aliwasili Ukraine mapema leo asubuhi akitokea Poland ametangaza mpango huo wa kitita cha mabilioni ya dola kwa ajili ya Ukraine muda mfupi baada ya kukutana na mwenyeji wake Rais Volodomyry Zelenskyy mjini Kyiv.
Mkuu huyo wa Umoja wa Ulaya anafanya ziara yake ya nane nchini Ukraine kwa dhamira ya kuendelea kuonesha mshikamano na taifa hilo lililo vitani pamoja na kujadili mipango ya kuivusha Ukraine katika msimu ujao wa baridi.
Akizungumza akiwa pamoja na Rais Zelenskyy, Von der Leyen amesema Ukraine inahitaji msaada wa kifedha na kijeshi kutoka mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya na washirika wengine kuendelea kuikabili Urusi.
Mkopo huo wa dola bilioni 39 utatolewa na Umoja wa Ulaya kwa dhamana kutoka kundi la mataifa tajiri la G7 ambayo yanalenga kuzipata fedha hizo kupitia mali za Urusi inazozizuia tangu kuanza kwa vita.
"Kwa hivyo, kwa haraka kabisa, mkopo huu utaingia moja kwa moja kwenye bajeti yenu ya taifa. Hii itaimarisha uthabiti wa kifedha wa Ukraine na kutoa nafasi ya kupunguza kishindo cha kutafuta fedha za bajeti. Mtaamua wenyewe namna bora ya kuzitumia fedha hizi, hali itakayowapa nafasi ya kutimiza mahitaji yenu" amesema Von der Leyen.
Rais Zelenskyy ataja vipaumbele vya matumizi ya mkopo itakaopokea
Rais Zelenskyy amesema mara moja mkopo huo utaelekezwa kwenye sekta za nishati, mifumo ya ulinzi wa anga na kukunua silaha. Ameahidi pia kuzitumia kujenga mahandaki ya wnafunzi kujificha wakati wa mashambulizi wakiwa shuleni au vyuoni.
Kundi la mataifa ya G7 linazishikilia mali za Urusi zenye thamini ya dola bilioni 300 ambazo zilizuiwa mnamo wiki za mwanzo baada ya kuzuka kwa vita. Kundi hilo limeahidi kutumia fedha hizo kuisaidia Ukraine.
Ama kuhusu suala la usalama wa nishati nchini Ukraine Bibi Von der Leyen amemwahidi rais Zelenskyy kwamba Brussels itapeleka euro milioni 160 kutoka kwenye mali za Urusi kusaidia mahitaji ya kibinadamu ya Ukraine wakati wa majira ya baridi.
Urusi imeilenga kwa makombora miundombinu ya nishati ya Ukraine na kupoteza uwezo wa kiasi gigawati 9 kutoka gridi ya taifa hilo. Kiwango hicho cha umeme uliopotea ni sawa na kile kinachozaliwa kwa jumla na mataifa matatu ya kanda ya Baltiki.
Amesema Umoja wa Ulaya umedhamiria kuisadia Ukraine kukarabati miundombinu itakayomudu kuzalisha angalau gigawati 2.5.
"Mpango wa Ushindi" wa Ukraine wapigiwa debe mazungumzo ya mjini Kyiv
Mbali ya suala la nishati na msaada wa kifedha, viongozi hao wawili walijadili pia kila kinachotiwa "Mpango wa Ushindi" wa Ukraine ulioandaliwa na Rais Zelenskyy.
Kiongozi huyo amewarai washirika wake kuuunga mkono mpango huo ambao anatarajiwa kuuwasilisha mbele ya Rais Joe Biden wa Marekani atakapokutana naye mjini Washington wiki inayokuja.
"Mpango mzima unategemea maamuzi ya haraka ya washirika wetu. Mpango huo unategemea maamuzi yanayopaswa kuchukuliwa kati ya mwezi Oktoba na Disemba, bila kuchelewa. Tunataka hilo lifanyike. Hapo ndiyo tunaamini mpango huo utafanikiwa" amesema Zeleskyy.
Zelenskyy amejizuia kutoa ufafanuzi wowote kuhusu mpango huo wala kufichua kile Ukraine inakitegemea kutoka kwa washirika wake.
Amesema maelezo ya kutosha yatapatikana baada ya mkutano wake na Biden anayeamini ataukubali mpango huo.