UN: Urusi imefanya mauaji ya kikatili nchini Ukraine
29 Juni 2022Umoja wa Mataifa umesema vikosi vya Urusi vimefanya mauaji ya kikatili katika zaidi ya maeneo 30 ikiwemo Kiev, Chernihiv na Sumy kati ya mwezi Februari na Machi.
Mkuu wa ujumbe wa ufutiliaji wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine Matilda Bogner amesema leo kuwa Urusi inaendesha vita kwa kukiuka sheria za kimataifa na kwamba "raia wa kawaida ndio wanaoendelea kuumia."
Bi. Bogner ametolea mfano wa shambulio kwenye kituo cha treni katika eneo la Kramatorsk mapema mwezi Aprili, ambapo watu 60 walipoteza maisha na wengine 111 walijeruhiwa.
Soma pia: Zelensky asema Urusi ina sifa za "Dola ya Kigaidi"
Katika mkutano na waandishi habari, Mkuu huyo wa ujumbe wa ufutiliaji wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine amesema kuwa maeneo ya watu wengi nchini humo yameshambuliwa na makombora na mizinga wakati sehemu nyengine zikishambuliwa kwa mabomu ya kutega ardhini.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeweka wazi kwamba, kuna sababu za msingi za kuamini kwamba vikosi vya Urusi na makundi ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Moscow, au kwa uchache jeshi la Ukraine, lilitumia silaha nzito katika mashambulizi yao.
Umoja wa Mataifa hadi sasa umechunguza visa 28 vya ukatili wa kingono ikiwemo ubakaji wa watu wengi.
Mashirika yanaofuatilia vita hivyo yamerekodi majengo au taasisi za matibabu 202 na shule 272 zilizoharibiwa kwa vita hivyo, japo idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi tofauti na inavyoripotiwa.
UN: Zaidi ya raia 10,000 wameuawa au kujeruhiwa wakiwemo mamia ya watoto
Kufikia wiki hii, Bogner amesema zaidi ya raia 10,000 wameuawa au kujeruhiwa wakiwemo mamia ya watoto. Takwimu hizo zimekusanywa kufuatia mahojiano waliofanyiwa wahanga na mashahidi pamoja na ziara katika uwanja wa vita.
Wakati hayo yanaripotiwa, Urusi imesema imelisababishia hasara kubwa jeshi la Ukraine. Licha ya mapigano kupungua kwa kiasi kikubwa upande wa mashariki mwa Ukraine, Urusi inaripotiwa kurusha makombora na kuyashambulia maeneo ya raia.
Hata hivyo taarifa nyingi kutoka uwanja wa mapambano haziwezi kuthibishwa na vyanzo huru. Kwa mfano, Urusi imedai kuwa imewaua wanajeshi 30 wa Ukraine wakati wa mapigano kusini mwa mji wa Lysychansk.
Soma pia: Vikosi vya Ukraine vyaondoka Severodonetsk
msemaji wa mkuu wa kikosi cha wanajeshi wa Ukraine, Oleksandr Shtupun amesema "Katika eneo la kuelekea Slovyansk, Urusi imeelekeza mashambulizi yake ili kuufikia mpaka wa Bohorodychne-Krasnopillya na kutengeneza mazingira ya kufanya mashambulizi zaidi huko Barvinkove na Slovyansk. Wamewashambulia wanajeshi wetu katika maeneo ya makaazi ya Mayaky na Serebryanka."
Vikosi vya Urusi pia vimeripoti kuharibu kituo cha mafunzo ya mamluki wa kigeni karibu na mji wa Mykolaiv, pamoja na kuharibu kambi nne za kijeshi.
Mapema leo, gavana wa mkoa huo Vitaly Kim aliandika katika mtandao wa Telegram kuwa watu watatu wameuawa na watano wamejeruhiwa katika shambulio la Urusi kwenye mji huo wa kusini mwa Ukraine.
Serikali za mitaa zimewahimiza watu kusalia majumbani ili kujikinga na mashambulizi ya Urusi na pia kutochapisha picha mitandaoni za kuonyesha uharibifu wa majengo.
Urusi imedai kwamba imewaua wapiganaji 100 katika uwanja wa mapambano karibu na Pitomnik, upande wa mashariki. Vifaa vya kijeshi pia viliharibiwa. Kulingana na Moscow, huo ulikuwa ni mfululizo wa mashambulizi ya Urusi ambayo yalisababisha vifo vya wapiganaji kadhaa wa Ukraine.
Hata hivyo, licha ya Urusi kujigamba kwa kufanya mashambulizi hayo, hakukuwa na ripoti zozote za wanajeshi wake kuitia mikononi miji mengine mipya.