Upinzani Uganda wataka mageuzi kwenye sheria za uchaguzi
2 Juni 2023Kulingana na wanasiasa wa upinzani, Uganda haiwezi kudai kutawaliwa kidemokrasia katika mazingira ya sasa ambapo katiba imefanyiwa mageuzi kwa ajili ya kuendeleza utawala wa Rais Yoweri Museveni. Museveni ametawala nchi hiyo tangu mwaka 1986.
Viongozi na wabunge wa vyama vya siasa vya upinzani wameshiriki mkutano wa siku tatu kujadili mapendekezo wanayotaka kuwasilisha bungeni ili kuboresha utawala wa kidemokrasia Uganda.
Wakiongozwa na Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine na Dkt Kizza Besigye, wanasiasa wa upinzani wametoa angalizo kuwa pana haja ya dharura kuhakikisha kuwa katiba ya nchi pamoja na sheria za uchaguzi vinachunguzwa upya.
Museveni aadhimisha miaka 37 tangu alipoingia madarakani
Kyagulanyi ambaye ni rais wa chama cha NUP amesema utawala wa rais Yoweri Museveni umetupilia mbali mamlaka za taasisi mbalimbali ambazo zingelinda haki za raia na pia kutelekeza majukumu yao bila ushawishi wa kisiasa.
Wabunge wakosolewa kuruhusu sera zinazokinzana na katiba
Lakini msomi wa masuala ya kisiasa chuoni Makerere Profesa Mwebesa Ndebesa amewakosoa wabunge wote kwa kuikubali hali ya kushinikizwa kuendeleza maslahi ya rais Museveni. Amelezea matukio ambapo wabunge wamepitisha sheria na sera zinazokinzana na katiba ya nchi baada ya kula rushwa.
Museveni amuondoa mwanae ukuu wa jeshi, ampandisha cheo
Wabunge wa upinzani watawasilisha mapendekezo ya kuifanyia mageuzi katiba ya nchi wakitaka awamu mbili za utawala wa rais zirejeshwe. Aidha wanataka umma uhusishwe katika kuwachuja majaji na maafisa wa tume ya uchaguzi kabla ya kuteuliwa katika nafasi hizo. Dkt Kizza Besigye ametoa angalizo kuwa hii ni muhimu kwa sababu katika chaguzi ambazo zimefanyika ushindi wa rais Museveni umetangazwa na mahakama wala si kutokana na matokeo ya uchaguzi.
Kwingineko, rais Museveni amewambia wabunge wa chama chake kwamba mwanawe Jenerali Muhoozi Kainerugaba amejijengea umaarufu hasa miongoni mwa vijana kutokana na udhaifu wa viongozi wa chama hicho katika kushughulikia maslahi ya wananchi. Amewakosoa kwa mienendo ya ufisadi ambayo inakwaza utoaji huduma kwa wananchi. Jenerali Muhoozi amekwisha elezea kuwa ana nia ya kugombea urais.