1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVietnam

Urusi na Vietnam zaapa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati

Sylvia Mwehozi
20 Juni 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin ametilia mkazo umuhimu wa ushirikiano wa kimkakati baina ya nchi yake na Vietnam wakati alipotia saini mikataba kadhaa na viongozi wa Hanoi katika ziara yake kwenye taifa hilo la Asia.

https://p.dw.com/p/4hK0L
Vietnam | Putin - Hanoi
Rais wa Vietnam To Lam na mgeni wake Rais Vladimir Putin mjini HanoiPicha: Minh Hoang/AP Photo/picture alliance

Putin ameizuru Vietnam, mshirika wa karibu wa Moscow tangu enzi ya Vita Baridi, baada ya kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, ambako alipata uungwaji mkono kamili kuhusu Ukraine na pia kusaini mkataba wa ushirikiano. Putin amekaribishwa nchini Vietnam kwa heshima ya kupigiwa mizinga 21 ya jeshi katika hafla iliyofanyika kwenye kasri la rais kabla ya kukutana na kiongozi wa chama cha Kikomunisti Nguyen Phu Trong, sambamba na Rais To Lam na waziri mkuu wa taifa hilo. Putin ameitaja Vietnam kuwa "rafiki na mshirika wa kuaminika" wa Urusi na kuongeza kuwa uhusiano wa nchi zote mbili "umevuka kipindi cha majaribu". Soma: Putin aelekea Vietnam akitokea Korea Kaskazini

Rais Putin na mwenyeji wake Rais Lam wamesaini mikataba kadhaa ya ushirikiano katika sekta tofauti kuanzia elimu, haki na miradi ya nyuklia. Baada ya kutia saini mikataba ya ushirikiano, viongozi hao wawili walifanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na kueleza kwamba ushirikiano wa kiulinzi na kiusalama haujailenga nchi yoyote bali unataka kuchangia katika "amani, utulivu na maendeleo endelevu ya kikanda". Putin anasema mazungumzo ya pande mbili yalikuwa ya kujenga na pande zote mbili zina misimamo "sawa au inayokaribiana" katika masuala muhimu ya kimataifa.

Vietnam | Putin
Putina akiwasili mjini HanoiPicha: Minh Hoang/AP Photo/picture alliance

"Wakati tukijadili hali katika kanda ya Asia-Pasifiki, tumeelezea maslahi ya pande zote ya usalama wa kuaminika katika kanda ya Asia-Pasifiki, kwa kuzingatia misingi ya kutotumia nguvu na utatuzi wa amani wa mizozo, ambayo ndani yake hakutokuwa na kambi za kijeshi na kisiasa," amesema rais Putin. Rais Vladmir Putin aiahidi ushirikiano mkubwa Korea Kaskazini wakati akianza ziara yake ya kwanza nchini humo tangu miaka 24.

Kwa upande wake Rais wa Vietnam To Lam pia hakwenda mbali na matamshi ya mgeni wake Putin kuhusu kushughulikia changamoto za kiusalama.''Pande zote mbili zinataka kuimarisha ushirikiano wa ulinzi na usalama, jinsi gani ya kushughulikia changamoto zisizo za kijadi za kiusalama kwa misingi ya sheria za kimataifa, kwa ajili ya amani na usalama katika kanda na dunia."

 Putin -Kim Jong Un
Putin akiwa na mwenyeji wake kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong UnPicha: GAVRIIL GRIGOROV/AFP/Getty Images

Urusi imekuwa muuzaji mkubwa wa silaha wa Vietnam kwa miongo mingi, ikichukua zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kati ya mwaka 1995 hadi 2023. Lakini kiwango hicho kimeshuka katika miaka ya hivi karibuni wakati vikwazo vya kimataifa vinavyohusiana na mzozo wa Ukraine vikiongezeka.

Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya zote zimetangaza vikwazo vipya mapema wiki iliyopita huku kundi la nchi zilizopiga hatua kiviwanda za G7 zikikubaliana kutumia mapato yatokanayo na mali zilizofungiwa za Urusi kuipatia Ukraine msaada mpya wa dola bilioni 50.