Urusi: Ukraine yashambulia tena Belgorod kwa makombora-droni
3 Januari 2024Gavana katika eneo hilo Vyacheslav Gladkov amesema hali bado imeendelea kuwa ya wasiwasi, ambapo Urusi iliainisha kuwa raia wapatao ishirini na tano wakiwemo watoto watano waliuwawa kufuatia mashambulizi ya Ukraine mwishoni mwa juma lililopita.
Ongezeko la mashambulizi katika eneo hilo la Belgorodkatika sherehe za mwaka mpya, yamefanyika wakati Urusi ilipovurumisha mkururo wa mashambulizi makali zaidi dhidi ya Ukraine tangu vita ilipozuka takriban miaka miwili sasa.
Serikali ya Kyiv imesema kwamba Urusi imerusha zaidi ya ndege mia tatu zisizokuwa na rubani na makombora ya aina mbalimbali katika miji yote ya Ukraine, tangu siku ya Ijumaa yakilenga miundombinu ya kiraia.
Rais Volodymyr Zelenskiykatika taarifa yake amesema hadi sasa hakuna nchi ambayo imejitokeza hadharani na kuzuia mashambulizi kama hayo yakiwemo mashambulizi ya anga, ambapo kwa siku ya leo pekee takriban makombora kumi aina ya Kanzihal yalidunguliwa na kikosi cha anga Ukraine.
"Huu ni ugaidi wa dhahiri kabisa." Alisema Zelenskiy katika aarifa yake na kuongeza kwamba katika siku chache na masiku ya mwisho kuanzia Desemba 29 hadi leo, tayari Urusi imevurumisha takriban makombora 300 na zaidi ya ndege zisizo na rubani 200 dhidi ya Ukraine.
" Leo pekee makombora 10 ya Kinzihal yalidunguliwa." Aliongeza hadi sasa hakuna nchi nyingine ambayo imezuia mashambulizi kama hayo ya ndege zisizo na rubani na makombora, yakiwemo yale ya angani.
Soma pia:Zelensky asema watu wanne wameuawa na 92 wajeruhiwa
Eneo la Belgorod kama ilivyo kwa maeneo mengine ya mpakani limekuwa likikumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya kiwango cha chini, lakini shambulizi la siku ya Jumamosi linatajwa na Moscow kuwa baya zaiditangu kuanza kwa vita ambapo rais Vladimir Putin aliapa kuwa, Ukraine italipa kwa gharama kubwa.
Mashambulizi ya Urusi katika miji ya Ukraine
Urusi ilishambulia miji miwili mikubwa ya Ukraine siku ya Jumanne, katika wimbi jipya la mashambulizi makubwa ya anga yaliyoua takriban raia watano.
Kufuatia mashambulizi hayo, Poland ambayo ni mshirika wa karibu wa Ukraine na mwananchama wa jumuiya ya kujihami ya NATO imeyatolea mwito mataifa ya Magharibi kuimarisha vikwazo dhidi ya Urusina kuipatia Ukraine makombora ya masafa marefu ili kujibu mashambulizi ya Moscow ya hivi karibuni.
Soma pia:Urusi yaongeza mashambulizi Ukraine na kuuwa watu wanne
Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland Radoslaw Sikorski ameandika katika mtandao wa kijamii wa X zamani ukijulikana kama Twitter kwamba, Jumuiya ya kimataia inapaswa kujibu mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Ukraine kwa lugha ambayo Putin anaelewa--kuimarisha vikwazo ili asiweze kutengeneza silaha zaidi.
Wakati hayo yakiendelea, shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limetolea wito kwa pande mbili zinazohasimiana kujizuia kutokana na mashambulizi yanayoendelea yaliosababisha vifo vya raia na wengine kadhaa kujeruhiwa huku miundombinu ikiharibiwa vibaya.
Kamishna wa shirika hilo Volker Türk amesema, sheria za kimataifa zinakataza mashambulizi ya kiholelana kutaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kupunguza kasi ya mashambulizi na kuwalinda raia.