1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Urusi yaapa kulipiza kisasi baada ya mashambulizi ya Ukraine

4 Januari 2025

Urusi imeapa siku ya Jumamosi kulipiza kisasi baada ya kuishutumu Ukraine kushambulia eneo la mpakani la Belgorod kwa kuvurumisha makombora ya masafa marefu ya ATACMS yaliyotolewa na Marekani.

https://p.dw.com/p/4ook2
Kombora la masafa marefu la ATACMS
Kombora la masafa marefu la ATACMSPicha: picture alliance/dpa/yonhap

"Hatua hizi za serikali ya Kyiv, ambayo inaungwa mkono na washirika wa Magharibi, itakabiliwa na kisasi," ilisema taarifa ya wizara ya ulinzi ya Urusi ikiishutumu Ukraine kwa kulenga eneo la mpakani la Belgorod kwa makombora ya masafa marefu.

Hata hivyo Moscow imesema ilifanikiwa kuyadungua makombora manane ya ATACMS  na kuonya kwamba matumizi yake yanaweza kuzua shambulio la kombora la masafa marefu lenye uwezo mkubwa katikati mwa mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.

Mwishoni mwa mwaka jana, rais anayeondoka wa Marekani Joe Biden aliiruhusu Ukraine kutumia makombora hayo dhidi ya Urusi, hatua ambayo ililaaniwa na Kremlin iliyosema inavichochea vita hivyo.

"Mifumo ya ulinzi wa anga iliharibu makombora manane yaliyovurumishwa ya ATACMS pamoja na droni 72," Hii ikiwa ni kulingana na wizara ya ulinzi ya Urusi. Makombora hayo yana uwezo wa kusafiri hadi kilometa 300.

Wizara hiyo pia ilisema kuwa imechukua udhibiti wa kijiji cha Ukraine cha Nadiia, mojawapo ya maeneo machache yaliyosalia kwenye udhibiti wa Kyiv katika eneo la mashariki la Lugansk.

Shughuli zasitishwa katika uwanja wa ndege wa mjini St Petersburg

Uwanja wa Ndege wa Pulkovo katika mji wa St.Petersburg
Uwanja wa Ndege wa Pulkovo katika mji wa St.PetersburgPicha: Alexander Demianchuk/TASS/dpa/picture alliance

Mamlaka za Urusi zililazimika kusitisha kwa muda shughuli katika uwanja wa ndege wa mjini St. Petersburg, kutokana na sababu za kiusalama.

Kwa saa chache, hakukuwa na ndege iliyopaa wala kutua katika uwanja wa Ndege wa Pulkovo huku kukiwa na taarifa za uwepo wa droni za Ukraine katika eneo hilo.

Soma pia: Ukraine na Urusi zazima mashambulizi kadhaa ya droni

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema usiku wa kuamkia Jumamosi, ilidungua droni 16 za Ukraine katika mikoa ya Bryansk, Smolensk, Belgorod, Pskov na Leningrad. Mikoa ambayo inauzunguika mji wa St.Petersburg.

Mwakilishi wa shirika la uangalizi wa anga la Urusi "Rosaviatsia" amesema operesheni hizo za kiusalama zilianzishwa tena asubuhi ya Jumamosi.

Mafanikio ya Urusi kwenye uwanja wa vita

Askari wa Urusi wakipambana na vikosi vya Ukraine huko Kursk
Askari wa Urusi wakipambana na vikosi vya Ukraine huko KurskPicha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

Kulingana na uchambuzi wa shirika la habari la AFP, mwaka 2024, Moscow imekuwa ikisonga mbele kwa karibu kilomita 4,000 za mraba ndani ya ardhi ya Ukraine, wakati jeshi la  Kyiv  likipambana na uhaba na uchovu wa wanajeshi wake.

Tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2025, pande zote mbili zimeshutumiana kwa kuendesha mashambulizi mabaya dhidi ya raia na miundombinu muhimu.

Gavana wa mkoa wa Kharkiv Oleg Synegubov amesema shambulio la Urusi katika kijiji kimoja eneo la kaskazini mashariki mwa mkoa huo mapema Jumamosi lilimuua mzee wa miaka 74.

(Vyanzo: AFP, AP, RTRE, DPA)