1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waargentina waandamana kupinga sera za serikali

25 Januari 2024

Maelfu ya Waargentina wameandama huku wengine wakigoma katika hatua inayoonekana kuipa changamoto sera ya kupunguza bajeti ya rais Javier Milei, inayopingwa na waandamanaji wiki chache baada ya kuingia madarakani.

https://p.dw.com/p/4bfzr
Maandamano ya kuipinga serikali ya Rais Javier Milei wa Argentina.
Maandamano ya kuipinga serikali ya Rais Javier Milei wa Argentina.Picha: Marcelo Endelli/Getty Images

Waandamanaji zaidi ya 80,000 walikusanyika nje ya jengo la bunge la Argentina mjini Buenos Aires, katika maandamano makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa nchini humo katika miaka ya hivi karibuni na yaliyoitishwa na chama kikuu cha wafanyakazi CGT.

Waandamanaji hao katika taifa hilo la Amerika ya Kaskazini, waliandamana huku wakibeba mabango makubwa yaliyokuwa na picha ya rais Milei yalioandikwa "Nchi yetu haiuzwi" na Mlo sio kipaumbele" huku wakipiga ngoma na kurusha fataki hewani.

CGT, mashirika mengine ya kijamii na makundi mengine ya wataalamu walishiriki maandamano hayo jana Jumatano kupinga hatua ya kubana matumizi iliyopendekezwa na serikali ya rais  Javier Milei.  Waandamanaji walilenga kuishinikiza serikali kuachana na mpango wake huo pamoja na mageuzi mapana aliyoyaweka ili kulinda uchumi wa taifa hilo.

Soma zaidi: Waargentina wagoma, waandamana kumpinga Rais Milei

Siku kumi baada ya kuingia madarakani mwezi Desemba, rais huyo mpya alitangaza msururu wa mageuzi makubwa amabyo yalipunguza ulinzi wa wafanyakazi, yakaondoa ukomo wa udhibiti wa bei za biadhaa fulani za matumizi. Maelfu ya waandamanaji wakiwemo walimu, madaktari na wafanyakazi wa serikali walijiunga na maandamano ya kupinga hatua hizo.

Polisi wakikabiliana na maandamano ya kuipinga serikali ya Rais Javier Milei wa Argentina.
Polisi wakikabiliana na maandamano ya kuipinga serikali ya Rais Javier Milei wa Argentina.Picha: Luciano Gonzalez/Anadolu/picture alliance

"Tumehuzunishwa sana na serikali hii mpya, kwa sababu siku chache baada ya kuapishwa inaweka mikakati mibaya inayotuumiza sisi na wastaafu," Remigia Caceres ni katibu wa chama cha CGT.

Maandamano hayo yalifanyika pia katika maeneo mengine mengi ya taifa hilo. Mabadiliko yaliyopendekezwa na serikali yataathiri sekta mbali mbali kama wanavyosema baadhi ya waandamanaji.

Wataalamu wa afya wasema mikakati mipya itawaathiri wagonjwa 

Chini ya miezi miwili baada ya kuapishwa kwake kama rais wa Argentina Javier Milei sasa anakabiliwa na mtihani mkubwa katika mipango yake ya kuuinua uchumi wa taifa hilo.

Tayari madaktari wamesema wameshaanza kusikia makali ya hatua hizo na kwamba sheria zilizopendekezwa na serikali zitaongeza gharama ya dawa itakayowaathiri wagonjwa.

Polisi wakikabiliana na maandamano ya kuipinga serikali ya Rais Javier Milei wa Argentina.
Polisi wakikabiliana na maandamano ya kuipinga serikali ya Rais Javier Milei wa Argentina.Picha: Luis Robayo/AFP

Kando na wanaopinga mabadiliko haya wapo pia wanaoona mpango wa rais Milei ni wa manufaa, wakisema taifa hilo linahitaji mabadiliko magumu. Baadhi wamesema ni lazima watu wa Argentina wajaribu matakwa ya serikali nyengine yatakayoleta mabadiliko na pia muda unahitajika ili mikakati iliyowekwa iweze kufanya kazi.

Soma zaidi: Rais mpya ya Argentina aanza kazi kwa onyo la kukaza mkanda

Juan Gabriel Mendez, mfanyabiashara katika mji wa Bueno Aires amesema ni lazima watu wawe na fikra tofautia akisistiza kuwa argentina imeshawahi kuwa na mageuzi ya kiuchumi yaliyowaumiza waargentina pakubwa. Rais Milei mwenyewe alikiri kuwa mageuzi ni magumu na machungu lakini yanahitajika kuufufua uchumi wa taifa hilo unaoyumba.

Viwango vya Umasikikini nchini humo vimefikia asilimia 40 na taifa hilo kwa sasa, linakabiliwa na mfumuko wa bei unaozidi asilimia 200 baada ya miongo kadhaa ya usimamizi mbaya wa fedha.      

ap/afp