1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa M23 wahusishwa na makaburi ya pamoja nchini DRC

14 Juni 2023

Ripoti ya Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Right Watch imesema waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda huenda wanahusika na vifo vya watu waliozikwa kwenye makaburi ya pamoja huko Kishishe nchini Kongo.

https://p.dw.com/p/4SZ55
DR Kongo Ein M23-Rebellen
Waasi wa M23 wakielekea eneo la kaskazini kabla ya kuondoka Kibumba, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Disemba 23, 2022.Picha: GLODY MURHABAZI/AFP via Getty Images

Ripoti hiyo ya HRW imesema miili hiyo inaaminika kuwa ni ya wanavijiji na wanamgambo waliotekwa na baadae kuuliwa na waasi wa M23, kati ya Novemba 2022 na Aprili 2023, wakati kundi hilo lilipokuwa likiondoka Kishishe, katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Shirika hilo la Human Rights Watch limerekodi visa vya mateso vilivyofanywa na waasi wa M23 katika eneo hilo la Kishishe baada ya kuzungumza na mashuhuda, kutizama picha za satelaiti, za kawaida na za video. Pamoja na visa hivyo vya mateso, waasi hao wa M23 walichoma moto nyumba moja iliyokuwa imefurika miili, kutumia shule tatu kama kambi zao, ingawa baadae walichoma moja ya shule hizo, hatua iliyowanyima watoto fursa ya kusoma.

Wakazi wa Kishishe walioshuhudia mauaji ama mazishi ya miili hiyo wamesema kwamba makaburi ya pamoja yaliyorundikwa miili karibu 20 kwa kila kaburi yalichimbwa baada ya M23 kulidhibiti eneo hilo na baada ya kuondoka, baadhi ya makaburi ndipo yalipogunduliwa. Wakazi hawa wanasema, walichukua hatua ya kuchimba makaburi mapya na kuizika miili hiyo upya.

Soma Zaidi:Zaidi ya raia 130 wauawa na waasi wa M23 yasema ripoti ya UN 

Maeneo kadhaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na makundi ya waasi.
Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch lilirekodi visa vya mateso kwa watu wa Kishishe na kutaka hatua kuchukuliwa.Picha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Mmoja ya mashuhuda ameliambia shirika hilo kwamba aliiona miili minne kwenye nyumba ya jirani yake. Amesema alishuhudia waasi hao wakiwaua hasa wanaume kwa kutumia majembe. Na kwa mamcho yake aliona wakiwatoa watu karibu 20 waliokuwa wamejificha kwenye kanisa la Adventist na kumchinja mmoja baada ya mwingine.

Mmoja ya wahanga wa mauaji hayo amesema M23 walikuja nyumbani kwao, wakamburuta mjomba wake na kumtoa nje, kisha wakampiga risasi na kuutupa mwili kwenye bonde. Lakini baadae walimzika. Mmoja ya wanavijiji aliyekuwa mgonjwa mnamo mwezi Novemba, wakati huo waasi hao walipokuwa wanafanya mauaji hayo, amesema alishurutishwa kukusanya majembe na spedi kisha wakaenda kuchimba kaburi na kuwazika watu 15 na siku ya pili wakachimba makaburi mengine na kuwazika watu 17, ingawa si katika kaburi moja. Anasema aliiona baadhi yao waliuawa kwa kupigwa risasi mdomoni, vifuani na wengine wamevunjwa magoti.

HRW yataka hatua kuchukuliwa kwa kushirikisha jamii ya kimataifa.

Makaburi yalichimbwa zaidi karibu na waliko waasi hao, karibu na makanisa ambako wengi walikimbilia kujificha, kituo cha polisi ama makazi ya watu tu. Baadhi ya miili ilikutwa vyooni, kwenye mto Nyabihanda katika eneo linaloitwa Matodi na mafuvu ya vichwa 23 yaliyokutwa kwenye shimo walilochimba waasi wenyewe.

Shirika la Human Rights Watch linaiomba serikali ya Jamhuri a Kidemokrasia ya Kongo kushirikiana na jamii ya kimataifa kuwawajibisha wahusika wa visa vya mateso.
Rais Felix Tshisekedi(kushoto) wa DRC na rais Paul Kagame wa Rwanda wamekuwa katika mvutano kufuatia madai kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23.

Kijana mmoja wa miaka 22 amesema alilazimishwa kujiunga naM23, waliomwambia wanakwenda kupambana na waasi wa FDLR. Lakini anasema hakuwaona hao FDLR na badala yake waliwaua wakulima waliokuwa mashambani na kila waliyekutana nae njiani. Na aliporejea nyumbani alikuta baba na mdogo wake wameuawa. Anasema alilazimika kujifanya kama hawajui, kwa sababu waasi hao walisema hao ni wafuasi wa Mai Mai. 

Kwenye taarifa ya Disemba 3, M23 ilikana madai hayo yote na kusema watu wanane walikufa katikati ya makabiliano huko Kashishe. Na Juni 6, msemaji wa kundi hilo aliiambia Human Rights Watch kwamba hawahusiki na madai ya mauaji, kuchoma moto nyumba ama kuvamia shule.

Mtafiti wa masuala ya Afrika kwenye shirika hilo Clementine de Montjoye ameiomba serikali ya Kongo kuomba msaada kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na serikali washirika kufukua makaburi hayo na kurudisha miili kwa familia zao na kuwawajibisha wahusika. Limeomba pia baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwaingiza katika orodha ya vikwazo viongozi wa M23 na vigogo wa Rwanda wanaowasaidia.

Soma Zaidi: Mapigano mapya yazuka kati ya M23 na wapiganaji hasimu DRC

Imeiomba pia mamlaka ya Kongo, kwa kusaidiwa na washirika wa kimataifa, kuhakikisha kunafanyika uchunguzi wa haraka na usio na upendeleo wa mauaji na uhalifu mwingine uliofanywa Kishishe na matokeo ya uchunguzi yawekwe hadharani. Imeomba pia serikali hiyo kuwaalika wataalam wa Umoja wa Mataifa au wataalam huru wa kimataifa, kusaidia kuchambua ushahidi katika makaburi hayo ya pamoja.