Wafichuzi wa maovu wazidi kukabiliwa na hatari Afrika
4 Septemba 2024Wafichua taarifa ni watu ambao hufichua shughuli zisizo halali, zinazoenda kinyume na maadili au zisizofaa na zinazomhusu mtu binafsi, serikali au hata mashirika. Mara nyingi watu hao hufanya hivyo na kujiweka kwenye hatari ya kudhuriwa au hata kuuawa na wale wanaohusishwa na matukio ambayo yamefichuliwa.
Watu hao wanaofahamika zaidi kama wafichua taarifa wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kazi hiyo. Mwanahabari wa Ghana anayejihusisha na upelelezi Manasseh Azure Awuni, anafahamika zaidi kwa kazi yake ya kuripoti matukio ya ufisadi katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ilimpa Awuni ulinzi wa polisi wenye silaha. Mnamo mwaka 2020, alilazimika kutoroka Ghana kuelekea Afrika Kusini baada ya kupokea vitisho vya kuuawa na kusema kwamba madhila yote hayo aliyopitia, yalimsababishia changamoto kubwa za afya ya akili.
Soma pia: Burkina Faso yamulikwa kuhusu utekaji nyara wanaharakati na waandishi
Awuni alizungumzia mauaji ya mwandishi wa habari Ahmed Suale, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi nje ya nyumba yake mnamo mwaka 2019, baada ya Mbunge wa Ghana, Kennedy Agyapong, kukasirishwa na taarifa za mwandishi huyo kuhusu rushwa katika soka la Ghana.
Mbunge huyo aliweka wazi sura ya mwandishi huyo pamoja na anakoishi huku akiahidi kutoa kitita cha pesa kwa yeyote ambaye angeliweza kumdhuru. Na hiyo ilikuwa ni kesi ya kwanza kujulikana nchini Ghana ambayo ilihusisha mwandishi wa habari kuuawa kutokana na kazi yake.
Miaka mitano baadaye, kesi hiyo bado haijatatuliwa. Awuni ameiambia DW kwamba hilo linaonyesha ni jinsi gani ilivyo hatari kufanya kazi katika mazingira ambayo unaweza kutishiwa au hata kuuawa, na hakuna anayeshughulishwa kutokana na mauaji hayo.
Ulinzi mchache kwa wafichua taarifa barani Afrika.
Hatari kwa wafichuzi kote Afrika
Matukio kama hayo hayashuhudiwi nchini Ghana pekee, lakini Ghana ni mojawapo ya nchi chache za Kiafrika ambazo zina ulinzi wa kisheria kwa wafichua taarifa.
Nchi zote za Afrika ni sehemu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Ufisadi (UNCAC), ispokuwa mataifa 10 ambayo ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cape Verde, Djibouti, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eritrea, Morocco, Mauritania, Somalia, Sudan Kusini na Eswatini ambayo hayajaidhinisha mkataba huo.
Mataifa pekee yenye sheria maalum za ulinzi kwa wafichua taarifa ni Uganda, Tanzania, Afrika Kusini, Namibia, Ghana, Ethiopia na Botswana. Lakini hata katika nchi hizo ambazo kuna sheria ya kutoa ulinzi kwa wafichua taarifa, bado kunaendelea kuripotiwa vitendo vya mauaji na vitisho.
Soma pia: Waandishi wa habari Afrika waaswa kuwasaidia wananchi
Wakati tukio la Ahmed Suale lilipoitikisa Ghana, Waafrika Kusini walishangazwa na mauaji ya mwaka 2021 ya Babita Deokaran, mfichua taarifa aliyebainisha sakata la manunuzi kwa bei ya juu zaidi ya vifaa vya kujikinga na UVIKO-19 katika kashfa ambayo iliyohusisha karibu dola milioni 22 za Kimarekani.
Mathias Shibata kutoka shirika la haki za binadamu la "Haki Africa" lenye makao yake makuu nchini Kenya anasema kuwa kwa sasa, mambo ni magumu kwenye uwanja wa kazi na inahitajika mwitikio wa haraka. Amesema nchini Kenya katika miaka 10 iliyopita, kumeshuhudiwa zaidi ya watu 300 waliotoweka au kuuawa kinyume cha sheria.
Awuni anasema kuwa hali huwa tete kwa mfichua taarifa hasa anaporipoti masuala muhimu yenye manufaa makubwa kwa taifa. Lakini wataalam kama Elijah Kandie Rottok, afisa mkuu katika Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya, anasema ni kwa manufaa ya Waafrika wote, kuanzia serikali, mashirika na hata raia kuwatia moyo wafichua taarifa ili kuboresha utumishi wa umma na kuimarisha uwajibikaji.