Watu zaidi ya 150 wajeruhiwa katika ghasia mjini Jerusalem
8 Mei 2021Takribani Wapalestina 163 wamejeruhiwa na maafisa 6 wa polisi wa Israel nao wameripotiwa kujeruhiwa katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa na kwingineko Mashariki mwa Jerusalem. Polisi wa Israel walitumia risasi za mipira kukabiliana na waumini wa Kipalestina waliokuwa wakirusha mawe, chupa na fataki.Polisi pia walilifunga lango la kuelekea msikiti wa Al-Aqsa ndani ya mji wa zamani huko Jerusalem.Watu 44 wafariki kwa kukanyagana Israel
Maelfu ya waumini wa Kiislamu walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya swala ya ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mvutano uliongezeka baada ya polisi wa Israel kuimarisha ulinzi mkali katika eneo la msikiti.
Tangu kuanza kwa mfungo wa Ramadhani, na kucheleweshwa kwa uchaguzi wa bunge wa palestina, machafuko yameibuka katika Ukingo wa Magharibu na Mashariki mwa Jerusalem.
Ghasia mjini Jerusalem na Ukingo wa Magharibi, zimeongezeka katika wiki za hivi karibuni baada ya Waplestina kupinga vizuizi vya Israel kuyafikia maeneo ya mji wa zamani wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, na pia kuongezeka kwa hasira inayotokana na uwezekano wa familia kadhaa za Kipalestina kuondolewa kwenye makaazi yao katika eneo la Sheikh Jarrah kupisha ujenzi wa makaazi ya wayahudi.
Marekani imetoa wito wa kupunguza mivutano na kusema kitisho cha kuwaondoa watu kwenye makaazi yao, kitaathiri zaidi hali katika eneo la Mashariki mwa Jerusalem, wakati Umoja wa Mataifa nao ukionya kwamba kuwoandoa watu kinguvu kunaweza kuheshabiwa kama uhalifu wa kivita.
Ghasia za Ijumaa zimetokea katika siku ya Al-Quds(Jerusalem kwa Kiarabu), ambayo huadhimishwa kila mwaka kuonyesha mshikamano na Wapalestina. Maandamano ya kuadhimisha siku hii yamefanyika nchini Iran na katika nchi tofauti zenye idadi kubwa ya Waislamu. Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema israel sio nchi bali ngome ya magaidi wakati wa sherehe hizo.
Mahakama ya juu ya Israel itatoa uamuzi juu ya kuondolewa Wapalestina eneo la Sheikh Jarrah siku ya ya Jumatatu ambayo itagongana na maadhimisho ya kila mwaka ya Israel kudhibiti Jerusalem Mashariki wakati wa vita ya Mashariki ya kati ya mwaka 1967.