Wengine waokolewa Uturuki baada ya saa 260
17 Februari 2023Wakati hayo yakijiri, familia ya watu saba kutoka Syria, ambao walinusurika tetemeko wamefariki leo Ijumaa baada ya nyumba walimohamia nchini Uturuki kukumbwa na moto.
Waziri wa afya wa Uturuki Fahrettin Koca, amesema kupitia mtandao wa Twitter kwamba kijana Osman mwenye umri wa miaka 14 aliokolewa masaa 260 baada ya tetemeko lenye ukubwa wa 7.8 kupiga mikoa ya kusini-mashariki mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria.
Waziri huyo alichapisha picha ya kijana huyo akiwa amefungua macho kwenye machela, na kusema Osman alipelekwa hospitalini mjini Antakya, katika mkoa ulioharibiwa na tetemeko wa Hatay.
Soma pia:Uturuki: Binti apatikana hai baada ya saa 248 chini ya kifusi
Shirika la habari la serikali ya Uturuki limeripoti kuwa waokoaji walimkuta Osman baada ya kusiki sauti katika vifusi.
Saa moja baadae, waokoaji kwingineko wakawaokoa wanaume wawili mjini Antakya, alisema waziri Koca, pia akionesha picha za wanaume hao wakipokea matibabu kutoka kwa wafanyakazi wa afya.
Shirika la habari la DHA limewataja wanaume hao kuwa Mehmeti Ali Sakiroglu mwenye umri wa miaka 26, na Mustafa Avci wa miaka 33, na kusema waliokolewa kutoka vifusi vya jengo sawa.
Wafariki baada ya kunusurika na tetemeko
vyombo vya habari vimeripoti juu ya watoto watano wa Kisyria na wazazi wao waliofariki duni hii leo, katika tukio la moto ulioikumba nyumbayo ya Uturuki walimohamia baada ya kunusurika tetemeko la wiki iliyopita.
Familia hiyo ya Wasyria ilihamia katika mkoa wa kati ya Konya ikitokea mji wa kusini-mashariki wa Nurdagi, ambao uliharibiwa vibaya na tetemeko hilo la Februari 6.
Shirika la Anadolu limesema familia hiyo ya Kisyria lilihamia Konya na ndugu zao ikifuata njia iliyochukuliwa na mamilioni ya wengine waliopoteza makaazi katika mkasa huo.
Watoto watano waliokufa kwenye moto huo walikuwa na umri wa kati ya miaka minne na 13, kwa mujibu wa Anadolu.
UN yazundua mpango wa msaada kwa Uturuki
Wakati juhudi za uokozi zikiendeleaKatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema uhitaji wa misaada ya kiutu unaongeza katika maeneo yaliokumbwa na tetemeko.
Kufuatia hatua hiyo Umoja huo umetangaza kuzinduliwa kwa mpango wa kukusanya kiasi cha fedha bilioni moja za Marekani kwa ajili ya watu wa Uturuki waliokumbwa na mkasa huo mbaya zaidi kushuhudiwa kwa kipindi cha karnwe moja.
Msemaji wa Katibu mkuu huyo Stephane Dujarric amesema Uturuki imekuwa ikiwakirimu idadi kubwa ya wakimbizi ulimwenguni hasa jirani yake Syria.
Soma pia:UN: Dola bilioni 1 zahitajika kusaidia waathirika wa Uturuki
Ameusihi ulimwengu kuonesha mshikamano kwa taifa hilo kama ambavyo imekuwa desturi yake kusaidia wengine.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York amesema ufadhili huo utakaodumu kwa miezi 3, utakwenda kuwasaidia watu milioni 5.2.
"Watu milioni 5.2 watasaidiwa katika maeneo kadhaa ikiwemo usalama wa chakula,maji safi,ulinzi,elimu pamoja na makaazi" Alisema Dujarric
Uturuki ninyumbani kwa Wasyria milioni nne, wengi wao wanaishi katika mikoa ya kusini iliyoharibiwa na vibaya na tetemeko hilo, ambalo limeua zaidi ya watu 41,000 nchini Uturuki na Syria, na kujeruhi makumi ya maelfu ya wengine na kuwaacha mamilioni bila makazi katika msimu huu wa baridi kali.
Tetemeko hilo liliikumba mikoa 11 nchini Uturuki, ambapo majengo zaidi ya 84,000 ama yameporomoka au kuharibiwa vibaya, kwa mujibu wa waziri anaehusika na mipango miji wa nchi hiyo Murat Kulum.
Maafisa nchini humo wamesema juhudi za uokozi katika mikoa mitatu ya Adana, Kilis na Sanliurfa zimekamilishwa. Hata hivyo Uturuki na Syria bado hazijataja idadi ya watu ambao bado hawajulikani uwepo wao.