WFP: Machafuko Sudan yaweza kusababisha mgogoro wa kikanda
30 Aprili 2023Mkurugenzi wa WFP Martin Frick, ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba theluthi moja ya wakazi wa Sudan walikumbwa na njaa hata kabla ya mapigano kuanza na sasa wanakabiliwa na mfumuko wa bei, uhaba wa bidhaa zote muhimu pamoja na chakula.
Frick amesema nchi jirani za Chad na Sudan Kusini ambazo zimewapokea maelfu ya wakimbizi tangu mapigano yalipoianza nchini Sudan wiki mbili zilizopita, zinakabiliwa na ongezeko kubwa la kupanda kwa bei za bidhaa.
Mkurugenzi huyo wa WFP amesema bei za vyakula zimepanda kwa asilimia 28 katika kipindi cha muda mfupi katika nchi jirani ya Sudan Kusini ambayo inakabiliwa na mafuriko katika baadhi ya maeneo na ukame katika upande mwingine kutokana na matatizo ya hali ya hewa.
Mambo ni mabaya zaidi kutokana na hali ya wasiwasi katika Pembe ya Afrika, ambapo baada ya ukosefu wa mvua kwa misimu sita, kumekuwa na shinikizo kubwa la usambazaji wa chakula.
Kiongozi wa kijeshi wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan amekuwa akipambana na naibu wake Mohammed Hamdan Dagalo tangu Aprili 15. Dagalo ndiye kiongozi wa kundi la wanamgambo wenye ushawishi mkubwa na wanaofahamika kama Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Soma pia: Matumaini mapya ya mazungumzo yachomoza Sudan licha ya mapigano kuendelea
Majenerali hao wawili walichukua uongozi wa nchi hiyo yenye wakazi wapatao milioni 46 kupitia mapinduzi mawili ya kijeshi mwaka 2019 na 2021. Mamia ya watu wameuawa tangu kuanza kwa mapigano huku maelfu ya wengine wakiimbia nchi. Mataifa kadhaa ulimwenguni yameanzisha operesheni ya kuwahamisha raia wao kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama nchini Sudan.
Shirika hilo la Mpango wa Chakula Duniani limelazimika kusitisha misaada yake kwa watu wapatao milioni 7.6 nchini Sudan kutokana na mapigano yanayoendelea kuripotiwa na kusisitiza kuwa wakimbizi wa ndani nchini Sudan watakosa misaada muhimu bila ya usaidizi wa WFP na kwamba misaada hiyo itatolewa tena mara tu baada ya hali ya usalama itakaporejea.
Matumaini ya kufanyika mazungumzo ya amani
Wakati mapigano yakiripotiwa katika mji mkuu Khartoum na miji jirani, pande mbili pinzani za Jeshi nchini Sudan zimeshutumiana kwa ukiukaji mpya wa usitishaji mapigano ambayo yanatazamiwa kufikia tamati siku ya Jumapili wakati mzozo huu mbaya ukiendelea kwa wiki ya tatu licha ya onyo la kuelekea katika janga kubwa la vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Hadi sasa, matarajio ya mazungumzo ya amani bado ni hafifu. Kiongozi wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amesema kamwe hatokaa kwenye meza ya mazungumzo na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti. Mkuu huyo wa RSF kwa upande wake amesema atazungumza na al-Burhan mara tu baada ya jeshi lake kuacha vitendo vya uhasama.
Hata hivyo, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes, ameliambia siku ya Jumamosi shirika la habari la Reuters kwamba ameshuhudia hivi karibuni mabadiliko katika mitazamo ya pande zote na wameonekana kuwa tayari kwa mazungumzo ya amani, ila kwa vigezo kadhaa.
Soma pia: Mapigano yaendelea Sudan licha ya mkataba wa kuyasitisha
Perthes amesema pande zinazohasimiana kwenye mzozo unaoendelea nchini humo zimekubali kuwa, machafuko yaliyozuka wiki mbili zilizopita hayapaswi kuendelea.
Hatua hiyo imeleta matumaini japo kidogo hata wakati mapambano yakiendelea. Perthes amesema pande hizo mbili hasimu ziliteua wawakilishi kwa ajili ya mazungumzo yaliyopendekezwa kufanyika Jeddah nchini Saudi Arabia au Juba, huko Sudan Kusini.
Hata hivyo ameongeza kuwa, swali kubwa ni iwapo wawakilishi hao watafanikiwa kufika na kukaa kwenye moja ya mazungumzo. Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa hajaainisha ikiwa kuna muda maalumu uliotengwa kwa ajili ya mazungumzo hayo.
Kulingana na Wizara ya afya, takriban watu 528 wameuawa na wengine 4,599 wamejeruhiwa. Umoja wa Mataifa umeripoti idadi sawa na hiyo ya watu waliokufa, lakini inaamini kwamba idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi.